Sheria ya Urithi

1451 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Hesabu 36:1–12

1 Viongozi wa jamaa ya ukoo wa Gileadi mwana wa Makiri, mwana wa Manase, waliokuwa wametoka katika koo za wazao wa Yosefu, walikuja na kuzungumza mbele ya Mose na viongozi, wakuu wa jamaa ya Waisraeli. 2 Wakasema, “Bwana alipomwamuru bwana wangu kuwapa Waisraeli nchi kama urithi kwa kura, alikuamuru kutoa urithi wa ndugu yetu Selofehadi kwa binti zake. 3 Sasa ikiwa wataolewa na watu wa makabila mengine ya Kiisraeli, itakuwa kwamba urithi wao utaondolewa kutoka urithi wa mababu zetu na kuongezwa katika urithi wa kabila ambalo dada hao wameolewa. Kwa hiyo sehemu ya urithi tuliyogawiwa itachukuliwa kutoka kwetu. 4 Wakati mwaka wa Yubile kwa Waisraeli utafika, urithi wao utaongezwa kwa lile kabila ambalo wameolewa, na mali yao itaondolewa kutoka urithi wa kabila la mababu zetu.”

5 Ndipo kwa agizo la Bwana Mose akatoa amri ifuatayo kwa Waisraeli: “Kile wazao wa kabila la Yosefu wanachosema ni kweli. 6 Hivi ndivyo Bwana anavyoamuru kwa binti za Selofehadi: Wanaweza kuolewa na mtu yeyote wampendaye, mradi tu waolewe miongoni mwa koo za kabila za baba yao. 7 Hakuna urithi katika Israeli utakaohamishwa kutoka kabila moja kwenda kabila jingine, kwa kuwa kila Mwisraeli atatunza ardhi ya kabila lake aliyoirithi kutoka kwa baba zake. 8 Kila binti atakayerithi ardhi katika kabila lolote la Israeli ni lazima aolewe na mtu kutoka kabila na ukoo wa baba yake, ili kila Mwisraeli amiliki urithi wa baba zake. 9 Hakuna urithi uwezao kuhamishwa kutoka kabila moja kwenda kabila jingine, kwa kuwa kila kabila la Israeli litatunza nchi linayorithi.”

10 Kwa hiyo binti za Selofehadi wakafanya kama Bwana alivyomwamuru Mose. 11 Binti za Selofehadi, ambao ni Mahla, Tirsa, Hogla, Milka na Noa, wakaolewa na waume, wana wa ndugu za baba yao. 12 Waliolewa ndani ya koo za wazao wa Manase mwana wa Yosefu, na urithi wao ukabaki katika ukoo na kabila la baba yao.

Sheria za Sadaka

Sheria za sadaka, pamoja na mambo mengine.

Hesabu 28

1 Bwana akamwambia Mose, 2 “Wape Waisraeli agizo hili na uwaambie: ‘Hakikisheni kwamba mnaniletea mimi kwa wakati uliowekwa chakula kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa kwa moto, kama harufu nzuri ya kupendeza.’ 3 Waambie: ‘Hii ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto mnayomtolea Bwana: wana-kondoo wawili wa mwaka mmoja wasio na dosari, kama sadaka ya kawaida ya kuteketezwa kila siku. 4 Andaa mwana-kondoo mmoja asubuhi na mwingine jioni, 5 kila mmoja atolewe pamoja na sadaka ya nafaka sehemu ya kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa pamoja na robo ya hini ya mafuta ya zeituni. 6 Hii ni sadaka ya kawaida ya kuteketezwa iliyoanzishwa katika Mlima Sinai kama harufu nzuri ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto. 7 Sadaka ya kinywaji itakayotolewa pamoja na kila mwana-kondoo ni robo ya hini ya kinywaji kilichochachuka. Mimina sadaka ya kinywaji kwa Bwana mahali patakatifu. 8 Andaa yule mwana-kondoo wa pili jioni, pamoja na sadaka ya nafaka na sadaka ya kinywaji kama ulivyofanya kwa ile sadaka nyingine ya asubuhi. Hii ni sadaka iliyotolewa kwa kuteketezwa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Bwana.

9 “ ‘Siku ya Sabato, utatoa sadaka ya wana-kondoo wawili wa mwaka mmoja wasiokuwa na dosari pamoja na sadaka yake ya kinywaji na sadaka ya nafaka yenye uzito wa sehemu mbili za kumi za efa za unga laini uliochanganywa na mafuta. 10 Hii ni sadaka ya kuteketezwa itakayotolewa kwa ajili ya kila Sabato, pamoja na sadaka ya kawaida ya kuteketezwa na sadaka yake ya kinywaji.

11 “ ‘Siku ya kwanza ya kila mwezi, mtamletea Bwana sadaka ya kuteketezwa ya fahali wawili wachanga, kondoo dume mmoja na wana-kondoo saba wa mwaka mmoja, wote wasiokuwa na dosari. 12 Pamoja na kila fahali, kutakuwa na sadaka ya nafaka ya unga laini sehemu tatu za kumi za efa, uliochanganywa na mafuta, pamoja na kondoo dume mmoja, sadaka ya nafaka ya unga laini uliochanganywa na mafuta; 13 pamoja na kila mwana-kondoo, sadaka ya nafaka yenye uzito wa sehemu ya kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta. Hii ni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri, sadaka ya kuteketezwa iliyotolewa kwa moto kwa Bwana. 14 Pamoja na kila fahali kutakuwa na sadaka ya kinywaji nusu ya hini ya divai; pamoja na kila kondoo dume, theluthi moja ya hini, na pamoja na kila mwana-kondoo robo hini. Hii ni sadaka ya kuteketezwa ya kila mwezi itakayotolewa kila mwandamo wa mwezi kwa mwaka. 15 Zaidi ya sadaka ya kawaida ya kuteketezwa pamoja na sadaka yake ya kinywaji, mbuzi mmoja dume atatolewa kwa Bwana kama sadaka ya dhambi.

16 “ ‘Katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, itafanyika Pasaka ya Bwana. 17 Katika siku ya kumi na tano ya mwezi huo itakuwa sikukuu; kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu. 18 Katika siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu, msifanye kazi za kawaida. 19 Leteni mbele za Bwana sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya kuteketezwa ya mafahali wawili wachanga, kondoo dume mmoja na wana-kondoo dume saba wenye umri wa mwaka mmoja, wote wasio na dosari. 20 Pamoja na kila fahali, andaa sadaka ya nafaka sehemu tatu za kumi za efa za unga laini uliochanganywa na mafuta; pamoja na kondoo dume, andaa sehemu mbili za kumi za efa; 21 pia pamoja na kila mmoja wa wale wana-kondoo saba, andaa sehemu ya kumi ya efa. 22 Pia mtoe beberu mmoja kama sadaka ya dhambi ambaye atafanya upatanisho kwa ajili yenu. 23 Andaa hizi licha ya zile sadaka za kawaida za kuteketezwa za kila asubuhi. 24 Kwa njia hii andaa chakula cha sadaka ya kuteketezwa kila siku, kwa siku saba kama harufu nzuri impendezayo Bwana. Hii itaandaliwa licha ya ile sadaka ya kawaida ya kuteketezwa ya kila siku pamoja na sadaka yake ya kinywaji. 25 Siku ya saba mwe na kusanyiko takatifu na msifanye kazi zenu za kawaida.

26 “ ‘Siku ya malimbuko, mnapomletea Bwana sadaka ya nafaka mpya wakati wa Sikukuu ya Majuma, mwe na kusanyiko takatifu na msifanye kazi zenu za kawaida. 27 Mlete sadaka ya kuteketezwa ya mafahali wawili wachanga, kondoo dume mmoja, na pia wana-kondoo saba wenye umri wa mwaka mmoja, kama harufu nzuri ya kumpendeza Bwana. 28 Pamoja na kila fahali itatolewa sadaka ya nafaka ya unga laini sehemu tatu za kumi za efa uliochanganywa na mafuta; pamoja na kondoo dume, andaa sehemu mbili za kumi za efa za unga laini; 29 na sehemu ya kumi ya efa ya unga laini kwa kila mmoja wa wana-kondoo saba. 30 Ongeza beberu mmoja kwa kufanya upatanisho kwa ajili yenu. 31 Andaa hizi sadaka pamoja na sadaka zake za vinywaji, kuwa nyongeza ya sadaka za kawaida za kuteketezwa, pamoja na sadaka yake ya nafaka. Hakikisha kuwa wanyama hao hawana dosari.