Sheria ya Mahakama (continued)

1491 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Kutoka 23

1 “Usieneze habari za uongo. Usimsaidie mtu mwovu kwa kuwa shahidi mwenye nia ya kudhuru wengine.

2 “Usifuate umati wa watu katika kutenda mabaya. Unapotoa ushahidi kwenye mashtaka, usipotoshe haki ukijumuika na umati wa watu, 3 nawe usimpendelee mtu maskini katika mashtaka yake.

4 “Kama ukikutana na maksai au punda wa adui yako anapotea, hakikisha umemrudisha kwake. 5 Ukiona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, usimwache hapo alipoangukia; hakikisha kuwa umemsaidia.

6 “Usiwanyime haki watu wako walio maskini katika mashtaka yao. 7 Ujiepushe na mashtaka ya uongo, wala usimuue mtu asiye na hatia au mtu mwaminifu, kwa maana sitamhesabia hana hatia yeye aliye na hatia.

8 “Usipokee rushwa, kwa kuwa rushwa hupofusha wale waonao, na kupinda maneno ya wenye haki.

9 “Usimwonee mgeni; ninyi wenyewe mnajua jinsi mgeni anavyojisikia, kwa sababu mlikuwa wageni Misri.

10 “Kwa muda wa miaka sita mtapanda mashamba yenu na kuvuna mazao, 11 lakini katika mwaka wa saba usiilime ardhi wala kuitumia, ili watu walio maskini miongoni mwenu waweze kupata chakula kutoka kwenye hayo mashamba, nao wanyama pori wapate chakula kwa yale mabaki watakayobakiza. Utafanya hivyo katika shamba lako la mizabibu na la mizeituni.

12 “Kwa siku sita fanya kazi zako, lakini siku ya saba usifanye kazi, ili maksai wako na punda wako wapate kupumzika, naye mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwako, pamoja na mgeni, wapate kustarehe.

13 “Uzingatie kutenda kila kitu nilichokuambia. Usiombe kwa majina ya miungu mingine, wala usiyaruhusu kusikika kinywani mwako.

14 “Mara tatu kwa mwaka utanifanyia sikukuu.

15 “Utaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu; kwa siku saba utakula mikate isiyotiwa chachu kama nilivyokuagiza. Fanya jambo hili kwa wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, ndio mwezi wa nne, kwa sababu katika mwezi huo ulitoka Misri.

“Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu.

16 “Utaadhimisha Sikukuu ya Mavuno kwa malimbuko ya mazao yako uliyopanda katika shamba lako.

“Utaadhimisha Sikukuu ya Kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka, unapokusanya mavuno yako toka shambani.

17 “Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakuja mbele za Bwana Mwenyezi.

18 “Msitoe damu ya dhabihu kwangu pamoja na kitu chochote kilicho na chachu.

“Mafuta ya mnyama wa sadaka ya sikukuu yangu yasibakizwe mpaka asubuhi.

19 “Utaleta malimbuko bora ya ardhi yako katika nyumba ya Bwana Mungu wako.

“Usimchemshe mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.

20 “Tazama, ninamtuma malaika akutangulie mbele yako akulinde njiani na kukuleta mpaka mahali nilipoandaa. 21 Mtamtii na kusikiliza kile anachokisema. Usiasi dhidi yake; hatakusamehe uasi wako, kwa maana Jina langu limo ndani yake. 22 Kama ukitii kweli kweli kile asemacho na kufanya yote nisemayo, nitakuwa adui wa adui zako, na nitawapinga wale wakupingao. 23 Malaika wangu atatangulia mbele yako na kukuleta katika nchi ya Waamori, Wahiti, Waperizi, Wakanaani, Wahivi na Wayebusi, nami nitawafutilia mbali. 24 Usiisujudie miungu yao, au kuiabudu, wala kufuata desturi yao. Utayabomoa kabisa na kuvunjavunja mawe yao ya ibada vipande vipande. 25 Utamwabudu Bwana Mungu wako, na baraka zake zitakuwa juu ya vyakula vyako na maji yako. Nami nitaondoa maradhi miongoni mwako, 26 na hakuna atakayeharibu mimba wala atakayekuwa tasa katika nchi yako. Nami nitakupa maisha makamilifu.

27 “Nitapeleka utisho wangu mbele yako na kufadhaisha kila taifa utakalolifikia. Nitafanya adui zako wote wakupe kisogo na kukimbia. 28 Nitatanguliza manyigu mbele yako kuwafukuza Wahivi, Wakanaani na Wahiti waondoke njiani mwako. 29 Lakini sitawafukuza kwa mara moja, kwa sababu nchi itabaki ukiwa na wanyama pori watakuwa wengi mno kwako. 30 Nitawafukuza kidogo kidogo mbele yako, mpaka uwe umeongezeka kiasi cha kutosha kuimiliki nchi.

31 “Nitaweka mipaka ya nchi yako kuanzia Bahari ya Shamu hadi Bahari ya Wafilisti, na kuanzia jangwani hadi Mto Frati. Nitawatia watu wanaoishi katika nchi hizo mikononi mwako, nawe utawafukuza watoke mbele yako. 32 Usifanye agano lolote nao wala na miungu yao. 33 Usiwaache waishi katika nchi yako, la sivyo watakusababisha utende dhambi dhidi yangu, kwa sababu ibada ya miungu yao hakika itakuwa mtego kwako.”

Mose Anapanda Mlimani

Kutoka 24

1 Kisha Mungu akamwambia Mose, “Njooni huku juu kwa Bwana, wewe na Aroni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli. Mniabudu kwa mbali, 2 lakini Mose peke yake ndiye atakayemkaribia Bwana; wengine wasije karibu. Nao watu wasije wakapanda pamoja naye.”

3 Mose alipokwenda na kuwaambia watu maneno yote na sheria zote za Bwana, wakaitikia kwa sauti moja, “Kila kitu alichosema Bwana tutakifanya.” 4 Ndipo Mose akaandika kila kitu Bwana alichokuwa amesema.

Akaamka kesho yake asubuhi na mapema na kujenga madhabahu chini ya mlima na kusimamisha nguzo kumi na mbili za mawe kuwakilisha makabila kumi na mawili ya Israeli. 5 Kisha akawatuma vijana wanaume wa Kiisraeli, nao wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu za mafahali wachanga kuwa sadaka za amani kwa Bwana. 6 Mose akachukua nusu ya damu ya wale wanyama na kuiweka kwenye mabakuli na nusu nyingine akainyunyiza juu ya madhabahu. 7 Kisha akachukua kile Kitabu cha Agano na kuwasomea watu. Nao wakajibu, “Tutafanya kila kitu alichosema Bwana, nasi tutatii.”

8 Ndipo Mose akachukua ile damu, akawanyunyizia wale watu, akasema, “Hii ni damu ya agano ambalo Bwana amelifanya nanyi kufuatana na maneno haya yote.”

9 Mose na Aroni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli wakapanda mlimani, 10 nao wakamwona Mungu wa Israeli. Chini ya miguu yake kulikuwa na kitu kama sakafu ya mawe ya yakuti samawi, iliyo safi kama anga angavu. 11 Lakini Mungu hakuinua mkono wake dhidi ya hawa viongozi wa Waisraeli; walimwona Mungu, nao wakala na kunywa.

12 Bwana akamwambia Mose, “Panda uje kwangu huku mlimani na ukae hapa, nami nitakupa vibao vya mawe, vyenye sheria na amri ambazo nimeziandika ziwe mwongozo wao.”

13 Basi Mose akaondoka na Yoshua mtumishi wake, naye Mose akapanda juu kwenye mlima wa Mungu. 14 Mose akawaambia wazee wa Israeli, “Tungojeni hapa mpaka tutakapowarudia. Aroni na Huri wako pamoja nanyi, na kila aliye na neno aweza kuwaendea wao.”

15 Mose alipopanda juu mlimani, wingu liliufunika huo mlima, 16 nao utukufu wa Bwana ukatua juu ya Mlima Sinai. Kwa muda wa siku sita wingu lilifunika mlima, na siku ya saba Bwana akamwita Mose kutoka katikati ya lile wingu. 17 Kwa Waisraeli utukufu wa Bwana ulionekana kama moto uteketezao juu ya mlima. 18 Kisha Mose akaingia ndani ya lile wingu alivyokuwa akipanda mlimani. Naye akakaa huko mlimani kwa muda wa siku arobaini, usiku na mchana.