Watumwa wa Jamii ya Mwebrania Wanarudishwa Utumwani
Wakaldayo wanapoondoka, watumwa wa jamii ya Mwebrania wanarudishwa utumwani.
589 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
11 Lakini baadaye wakabadili mawazo yao, na kuwarudisha wale watumwa waliokuwa wamewaacha huru, wakawafanya tena watumwa.
12 Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia kusema: 13 “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Nilifanya agano na baba zenu nilipowatoa Misri, kutoka nchi ya utumwa. Nilisema, 14 ‘Kila mwaka wa saba, kila mmoja wenu ni lazima amwache huru mtumwa ambaye ni Mwebrania mwenzenu aliyejiuza kwenu. Baada ya kukutumikia kwa miaka sita, ni lazima umwache huru aende zake.’ Hata hivyo baba zenu hawakunisikiliza wala kunijali. 15 Hivi karibuni tu mlitubu na kufanya yaliyo sawa machoni pangu: Kila mmoja wenu aliwatangazia uhuru Waebrania wake. Hata mlifanya agano mbele zangu ndani ya nyumba iitwayo kwa Jina langu. 16 Lakini sasa mmegeuka na kulinajisi jina langu. Kila mmoja wenu amemrudisha mtumwa wa kiume na wa kike ambao mlikuwa mmewaacha huru waende zao walikotaka. Mmewalazimisha kuwa watumwa wenu tena.
17 “Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana: Hamkunitii mimi. Hamkutangaza uhuru kwa ndugu zenu. Hivyo sasa, ninawatangazia ninyi ‘uhuru,’ asema Bwana: ‘uhuru’ ili kuanguka kwa upanga, tauni na njaa. Nitawafanya mwe chukizo kwa falme zote za dunia. 18 Watu waliovunja agano langu, na ambao hawakutunza masharti ya agano walilofanya mbele zangu, nitawafanya kama ndama waliyemkata vipande viwili, kisha wakatembea kati ya vile vipande vya huyo ndama. 19 Viongozi wa Yuda na Yerusalemu, maafisa wa mahakama, makuhani na watu wote wa nchi waliopita kati ya vile vipande vya ndama, 20 nitawatia mikononi mwa adui zao wanaotafuta uhai wao. Maiti zao zitakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi.
21 “Nitamtia Sedekia mfalme wa Yuda na maafisa wake mikononi mwa adui zao wanaotafuta uhai wao, kwa jeshi la mfalme wa Babeli, lililokuwa limeondoka kwenu. 22 Nitatoa amri, asema Bwana, nami nitawarudisha tena katika mji huu. Watapigana dhidi yake, wautwae na kuuteketeza kwa moto. Nami nitaiangamiza miji ya Yuda hivyo pasiwe na yeyote atakayeweza kuishi humo.”
Yeremia Anafungwa Gerezani Tena
Yeremia anajaribu kutoroka Yerusalemu, na anafungwa gerezani tena.
11 Baada ya jeshi la Wakaldayo kujiondoa kutoka Yerusalemu kwa sababu ya jeshi la Farao, 12 Yeremia akaanza kuondoka mjini ili kwenda nchi ya Benyamini ili akapate sehemu yake ya milki miongoni mwa watu huko. 13 Lakini alipofika kwenye Lango la Benyamini, mkuu wa walinzi, ambaye jina lake lilikuwa Iriya mwana wa Shelemia mwana wa Hanania, akamkamata Yeremia na kusema, “Wewe unakwenda kujiunga na Wakaldayo!”
14 Yeremia akasema, “Hiyo si kweli, mimi sijiungi na Wakaldayo.” Lakini Iriya hakumsikiliza; badala yake, akamkamata Yeremia na kumpeleka kwa maafisa. 15 Wakamkasirikia Yeremia, wakaamuru apigwe, na akafungwa katika nyumba ya Yonathani mwandishi waliyokuwa wameifanya gereza.
16 Yeremia akawekwa kwenye chumba kilichofukuliwa chini, kilichojengwa kwa zege ndani ya gereza chini ya ngome, akakaa huko kwa muda mrefu. 17 Kisha Mfalme Sedekia akatumana aletwe katika jumba la kifalme, mahali alipomuuliza kwa siri, “Je, kuna neno lolote kutoka kwa Bwana?”
Yeremia akajibu, “Ndiyo, utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli.”
18 Kisha Yeremia akamwambia Mfalme Sedekia, “Nimefanya kosa gani dhidi yako na maafisa wako au watu hawa, hata ukanitia gerezani? 19 Wako wapi manabii wako waliokutabiria wakisema, ‘Mfalme wa Babeli hatakushambulia wewe wala nchi hii?’ 20 Lakini sasa, bwana wangu mfalme, tafadhali sikiliza. Niruhusu nilete maombi yangu mbele yako, usinirudishe kwenye nyumba ya Yonathani mwandishi, nisije nikafia humo.”
21 Ndipo Mfalme Sedekia akatoa maagizo Yeremia awekwe katika ua wa walinzi, na apewe mkate kutoka mitaa ya waokaji kila siku mpaka mikate yote katika mji itakapokwisha. Kwa hiyo Yeremia akabaki katika ua wa walinzi.
Yeremia Anarudia Tabiri Zake kwa Mfalme 588 KK
Mfalme anapomsihi, Yeremia anarudia tabiri zake za awali.
1 Neno lilimjia Yeremia kutoka kwa Bwana wakati Mfalme Sedekia alipowatuma Pashuri mwana wa Malkiya, na kuhani Sefania mwana wa Maaseya kwake, kusema: 2 “Tuulizie sasa kwa Bwana, kwa sababu Nebukadneza mfalme wa Babeli anatushambulia. Labda Bwana atatenda maajabu kwa ajili yetu kama nyakati zilizopita, ili Nebukadneza atuondokee.”
3 Lakini Yeremia akawajibu, “Mwambieni Sedekia, 4 ‘Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, asemalo: Ninakaribia kuwageuzia silaha za vita zilizo mikononi mwenu, ambazo mnatumia kupigana na mfalme wa Babeli na Wakaldayo ambao wako nje ya ukuta wakiwazunguka kwa jeshi. Nami nitawakusanya ndani ya mji huu. 5 Mimi mwenyewe nitapigana dhidi yenu kwa mkono wangu ulionyooshwa na mkono wa nguvu, kwa hasira na ghadhabu kali na ukali mwingi. 6 Nitawaangamiza waishio katika mji huu, watu na wanyama, nao watauawa kwa tauni ya kutisha. 7 Baada ya hayo, nitamtia Sedekia mfalme wa Yuda, maafisa wake na watu wa mji huu ambao walinusurika tauni, upanga na njaa, mkononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, na kwa adui zao wale wanaotafuta uhai wao. Atawaua kwa upanga; hatakuwa na rehema juu yao au huruma wala kuwasikitikia,’ asema Bwana.
8 “Zaidi ya hayo, waambie watu hawa, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Tazama, naweka mbele yenu njia ya uzima, na njia ya mauti. 9 Yeyote atakayekaa katika mji huu atakufa kwa upanga, njaa au tauni. Lakini yeyote atakayetoka na kujisalimisha kwa Wakaldayo ambao wameuzunguka mji huu kwa jeshi, atanusurika, naye ataishi. 10 Nimekusudia kuufanyia mji huu jambo baya, wala si jema. Utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteketeza kwa moto, asema Bwana.’
11 “Zaidi ya hayo, ambia nyumba ya mfalme ya Yuda, ‘Sikia neno la Bwana, 12 Ewe nyumba ya Daudi, hili ndilo Bwana asemalo:
“ ‘Hukumuni kwa haki kila asubuhi,
mwokoeni mikononi mwa mdhalimu
yeye aliyetekwa nyara,
la sivyo ghadhabu yangu italipuka
na kuwaka kama moto
kwa sababu ya uovu mlioufanya:
itawaka na hakuna wa kuizima.
13 Niko kinyume nawe, ee Yerusalemu,
wewe uishiye juu ya bonde hili
kwenye uwanda wa juu wa miamba,
asema Bwana,
wewe usemaye, “Ni nani awezaye kuja kinyume chetu?
Nani ataingia mahali pa kimbilio letu?”
14 Nitawaadhibu kama istahilivyo matendo yenu,
asema Bwana.
Nitawasha moto katika misitu yenu
ambao utateketeza kila kitu kinachowazunguka.’ ”