Hotuba Njiani Kuelekea Gethsemane
Huenda barabarani
30 au 29 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Yohana 15:1–16:33
15:1 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli na Baba yangu ndiye mkulima. 2 Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata, nalo kila tawi lizaalo, hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi. 3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililonena nanyi. 4 Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda lisipokaa ndani ya mzabibu, vivyo hivyo ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kuzaa matunda.
5 “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lolote. 6 Mtu yeyote asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi kama hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea. 7 Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo, nanyi mtatendewa. 8 Kwa hiyo Baba yangu hutukuzwa, kwa vile mzaavyo matunda mengi, nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.
9 “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, hivyo ndivyo mimi nilivyowapenda ninyi. Basi kaeni katika pendo langu. 10 Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. 11 Nimewaambia mambo haya ili furaha yangu iwe ndani yenu na furaha yenu iwe kamili. 12 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi. 13 Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. 14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. 15 Siwaiti ninyi watumishi tena, kwa sababu watumishi hawajui bwana wao analofanya, bali nimewaita ninyi rafiki, kwa maana nimewajulisha mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu. 16 Si ninyi mlionichagua, bali mimi ndiye niliyewachagua ninyi na kuwaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kudumu. Ili nalo lolote mtakalomwomba Baba katika Jina langu, awape ninyi. 17 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane.
18 “Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba ulinichukia mimi kabla yenu. 19 Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungeliwapenda kama vile unavyowapenda walio wake. Kwa sababu ninyi si wa ulimwengu, lakini mimi nimewachagua kutoka ulimwengu, hii ndiyo sababu ulimwengu unawachukia. 20 Kumbukeni lile neno nililowaambia, ‘Hakuna mtumishi aliye mkuu kuliko bwana wake.’ Kama wamenitesa mimi, nanyi pia watawatesa. Kama wamelishika neno langu, watalishika na neno lenu pia. 21 Watawatendea ninyi haya yote kwa ajili ya Jina langu, kwa sababu hawamjui yeye aliyenituma. 22 Kama sikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa hawana udhuru kwa ajili ya dhambi zao. 23 Yeyote anayenichukia mimi, anamchukia pia na Baba yangu. 24 Kama sikuwa nimefanya miujiza ambayo haijapata kufanywa na mtu mwingine yeyote, wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa wameiona miujiza hii na bado wakatuchukia mimi na Baba yangu. 25 Lakini hii ni kutimiza lile neno lililoandikwa kwenye Sheria kwamba, ‘Walinichukia pasipo sababu.’
26 “Lakini atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, yaani, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi. 27 Ninyi nanyi itawapasa kushuhudia kwa sababu mmekuwa pamoja nami tangu mwanzo.
16:1 “Nimewaambia mambo haya yote ili msije mkaiacha imani. 2 Watawatenga na masinagogi. Naam, saa yaja ambayo mtu yeyote atakayewaua atadhani kwa kufanya hivyo anamtumikia Mungu. 3 Nao watawatenda haya kwa sababu hawamjui Baba wala mimi. 4 Lakini nimewaambia ninyi mambo haya, ili saa hiyo ikiwadia mpate kukumbuka ya kuwa nilikuwa nimewaambia. Sikuwaambia mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi.
5 “Sasa mimi ninakwenda kwake yeye aliyenituma, lakini hakuna hata aniulizaye, ‘Unakwenda wapi?’ 6 Kwa sababu nimewaambia mambo haya, mioyo yenu imejawa na huzuni. 7 Lakini nawaambia kweli, yafaa mimi niondoke, kwa kuwa nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu, lakini nikienda nitamtuma kwenu. 8 Naye atakapokuja, atauthibitishia ulimwengu kuhusu dhambi, haki na hukumu. 9 Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi, 10 kwa habari ya haki, kwa sababu ninakwenda kwa Baba, nanyi hamtaniona tena, 11 kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.
12 “Bado ninayo mambo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili sasa. 13 Atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza awatie katika kweli yote. Yeye hatanena kwa ajili yake mwenyewe, bali atanena yale yote atakayosikia, naye atawaonyesha mambo yajayo. 14 Atanitukuza mimi, kwa maana atayachukua yaliyo yangu na kuwajulisha ninyi. 15 Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu. Ndiyo maana nimesema Roho atachukua yaliyo yangu na kuwajulisha ninyi.
16 “Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona.”
17 Baadhi ya wanafunzi wakaulizana, “Ana maana gani asemapo, ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona’? Naye ana maana gani asemapo, ‘Kwa sababu ninakwenda kwa Baba’?” 18 Wakaendelea kuulizana, “Ana maana gani asemapo, ‘Kitambo kidogo’? Hatuelewi hilo analosema.”
19 Yesu akatambua kuwa walitaka kumuuliza juu ya hilo, hivyo akawaambia, “Je, mnaulizana nina maana gani niliposema, ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona’? 20 Amin, amin nawaambia, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi. Ninyi mtahuzunika, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. 21 Mwanamke anapokuwa na utungu wa kuzaa huwa na maumivu kwa sababu saa yake imewadia. Lakini mtoto akiisha kuzaliwa, yule mwanamke husahau maumivu hayo kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtoto ulimwenguni. 22 Hivyo ninyi mna maumivu sasa, lakini nitawaona tena, nayo mioyo yenu itafurahi na furaha yenu hakuna awaondoleaye. 23 Katika siku hiyo hamtaniuliza neno lolote. Amin, amin nawaambia, kama mkimwomba Baba jambo lolote kwa jina langu, yeye atawapa. 24 Mpaka sasa hamjaomba jambo lolote kwa Jina langu. Ombeni nanyi mtapewa, ili furaha yenu ipate kuwa kamili.
25 “Nimewaambia mambo haya kwa mafumbo. Saa yaja ambapo sitazungumza nanyi tena kwa mafumbo bali nitawaeleza waziwazi kuhusu Baba. 26 Siku hiyo mtaomba kwa Jina langu. Wala sitawaambia kwamba nitamwomba Baba kwa ajili yenu, 27 kwa maana Baba mwenyewe anawapenda, kwa sababu mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu. 28 Nilitoka kwa Baba na kuja ulimwenguni, sasa naondoka ulimwenguni na kurudi kwa Baba.”
29 Ndipo wanafunzi wake wakasema, “Sasa unazungumza waziwazi, wala si kwa mafumbo. 30 Sasa tumejua kwamba wewe unajua mambo yote, wala hakuna haja ya mtu kukuuliza maswali. Kwa jambo hili tunaamini kwamba ulitoka kwa Mungu.”
31 Yesu akawajibu, “Je, sasa mnaamini? 32 Saa inakuja, naam, imekwisha kuwadia, mtakapotawanyika kila mmoja kwenda nyumbani kwake na kuniacha peke yangu. Lakini mimi siko peke yangu kwa sababu Baba yu pamoja nami. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”