Kifo cha Yosia

610 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Nyakati 35:20–24

20 Baada ya haya yote, Yosia alipomaliza kulitengeneza vizuri Hekalu, Neko mfalme wa Misri, akapanda ili kupigana huko Karkemishi katika Mto Frati, naye Yosia akatoka kwenda kupigana naye. 21 Lakini Neko akamtumia wajumbe kusema, “Kuna ugomvi gani kati yangu mimi na wewe, Ee Mfalme wa Yuda? Si wewe ninayekushambulia wakati huu, bali ile nyumba ambayo nina vita nayo, Mungu ameniambia niharakishe, kwa hivyo acha kumpinga Mungu, ambaye yuko pamoja nami, la sivyo atakuangamiza.”

22 Lakini hata hivyo, Yosia hakukubali kumwacha, bali alijibadilisha ili kupigana naye vita. Hakusikiliza yale Neko aliyokuwa amemwambia kwa agizo la Mungu bali alikwenda kupigana naye katika tambarare ya Megido.

23 Wapiga upinde wakampiga Mfalme Yosia, naye akawaambia maafisa wake, “Niondoeni, nimejeruhiwa vibaya sana.” 24 Kwa hiyo wakamshusha kutoka kwenye gari lake la farasi, wakamweka kwenye gari lingine alilokuwa nalo na kumleta Yerusalemu, ambako alifia. Akazikwa katika makaburi ya baba zake, nayo Yuda yote na Yerusalemu wakamwombolezea Yosia.

2 Wafalme 23:25–27

25 Kabla wala baada ya Mfalme Yosia hapakuwepo na mfalme mwingine yeyote ambaye alimpenda Bwana kwa moyo wake wote, kwa roho yake yote, na kwa nguvu zake zote, sawasawa na Sheria yote ya Mose.

26 Hata hivyo, Bwana hakuacha ghadhabu yake iliyowaka dhidi ya Yuda kwa sababu ya yale yote ambayo Manase alikuwa amefanya kumghadhibisha. 27 Hivyo Bwana akasema, “Nitamwondoa Yuda mbele zangu kama nilivyomwondoa Israeli, nami nitaukataa Yerusalemu, mji niliouchagua, na Hekalu hili, ambalo nilisema, ‘Jina langu litakaa humo.’ ”

2 Nyakati 35:25–27

25 Nabii Yeremia akatunga maombolezo kwa ajili ya kifo chake, nao waimbaji wote, wanaume kwa wanawake, hufanya ukumbusho wa Yosia katika maombolezo hadi leo. Haya yakafanywa desturi katika Israeli, nayo yameandikwa katika Maombolezo.

26 Matukio mengine ya utawala wa Yosia na matendo yake mema, kulingana na yale yaliyoandikwa katika sheria ya Bwana: 27 matukio yote, kuanzia mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda.

2 Nyakati 34:1–2

1 Yosia alikuwa na miaka minane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka thelathini na mmoja. 2 Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana na kuenenda katika njia za Daudi baba yake, hakugeuka upande wa kuume wala wa kushoto.

2 Wafalme 22:3–23:3

3 Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, Mfalme Yosia akamtuma mwandishi Shafani mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, kwenda katika Hekalu la Bwana. Akasema: 4 “Panda uende kwa Hilkia, kuhani mkuu, umwambie ahesabu zile fedha ambazo zimeletwa katika Hekalu la Bwana, ambazo mabawabu wamekusanya kutoka kwa watu. 5 Waambie waikabidhi kwa watu walioteuliwa kusimamia kazi ya Hekalu. Waamuru watu hawa wawalipe wafanyakazi ambao wanakarabati Hekalu la Bwana: 6 wale maseremala, wajenzi na waashi. Waambie pia wanunue mbao na mawe yaliyochongwa ili kukarabati Hekalu. 7 Lakini hawahitajiki kutoa hesabu ya fedha walizokabidhiwa, kwa sababu wanafanya kwa uaminifu.”

8 Hilkia kuhani mkuu akamwambia Shafani mwandishi, “Nimekipata Kitabu cha Sheria ndani ya Hekalu la Bwana.” Akampa Shafani, ambaye alikisoma. 9 Kisha Shafani mwandishi akamwendea mfalme na kumpa taarifa akisema: “Maafisa wako wametoa ile fedha ambayo ilikuwa ndani ya Hekalu la Bwana na imekabidhiwa mikononi mwa wasimamizi wa marekebisho ya Hekalu.” 10 Ndipo Shafani mwandishi akampasha mfalme habari kwamba: “Hilkia kuhani amenipa kitabu hiki.” Naye Shafani akakisoma kile kitabu mbele ya mfalme.

11 Mfalme aliposikia maneno ya kile Kitabu cha Sheria, akararua mavazi yake. 12 Akatoa maagizo haya kwa Hilkia kuhani, Ahikamu mwana wa Shafani, Akbori mwana wa Mikaya, Shafani mwandishi, na Asaya mtumishi wa mfalme: 13 “Nendeni mkamuulize Bwana kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu na Yuda wote kuhusu yale yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki ambacho kimepatikana. Hasira ya Bwana ni kubwa inayowaka dhidi yetu kwa sababu baba zetu hawakuyatii maneno ya kitabu hiki. Hawajatenda kulingana na yale yote yaliyoandikwa humo kutuhusu sisi.”

14 Hilkia kuhani, Ahikamu, Akbori, Shafani na Asaya wakaenda kuongea na nabii mke Hulda, ambaye alikuwa mke wa Shalumu mwana wa Tikwa, mwana wa Harhasi mtunzaji wa chumba cha mavazi. Hulda aliishi Yerusalemu katika Mtaa wa Pili.

15 Akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: Mwambieni yule mtu aliyewatuma ninyi kwangu, 16 ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Nitaleta maafa juu ya mahali hapa na watu wake, kulingana na kila kitu kilichoandikwa katika kitabu hicho mfalme wa Yuda alichosoma. 17 Kwa sababu wameniacha mimi na kufukiza uvumba kwa miungu mingine, na kunighadhibisha kwa sanamu zote zilizotengenezwa kwa mikono yao, hasira yangu itawaka dhidi ya mahali hapa, wala haitatulizwa.’ 18 Mwambieni mfalme wa Yuda, ambaye amewatuma kumuuliza Bwana, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli, kuhusu maneno uliyoyasikia: 19 Kwa kuwa moyo wako ulikuwa msikivu na ulijinyenyekeza mbele za Bwana uliposikia kile nilichosema dhidi ya mahali hapa na watu wake, kwamba wangelaaniwa na kuachwa ukiwa, basi kwa sababu uliyararua mavazi yako na kulia mbele zangu, nimekusikia, asema Bwana. 20 Kwa hiyo nitakukusanya kwa baba zako, nawe utazikwa kwa amani. Macho yako hayataona maafa yote nitakayoleta juu ya mahali hapa.’ ”

Basi wakapeleka jibu lake kwa mfalme.

23:1 Kisha mfalme akawaita pamoja wazee wote wa Yuda na Yerusalemu. 2 Akapanda kwenda hekaluni mwa Bwana pamoja na watu wa Yuda, watu wa Yerusalemu, makuhani na manabii, watu wote wakubwa kwa wadogo. Akasoma wakiwa wanasikia maneno yote ya Kitabu cha Agano, ambacho kilikuwa kimepatikana katika Hekalu la Bwana. 3 Mfalme akasimama karibu na nguzo, na kufanya upya agano mbele za Bwana: yaani kumfuata Bwana na kuzishika amri zake, maagizo na sheria kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, hivyo kuyathibitisha maneno ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Kisha watu wote wakajifunga wenyewe kwa kiapo katika agano.

2 Wafalme 23:22–24

22 Hapakuwahi kuwepo na adhimisho lingine la Pasaka kama hilo tangu nyakati za Waamuzi walioongoza Israeli, wala katika nyakati zote za wafalme wa Israeli na wafalme wa Yuda. 23 Lakini katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Yosia, Pasaka hii iliadhimishwa kwa Bwana huko Yerusalemu.

24 Zaidi ya hayo, Yosia akawaondoa waaguzi, wanaoabudu mizimu, sanamu za kuagulia, sanamu za kuabudiwa, na vitu vingine vyote vya machukizo vilivyoonekana huko Yuda na Yerusalemu. Aliyafanya haya ili kutimiza matakwa ya sheria iliyoandikwa ndani ya kile kitabu ambacho Hilkia kuhani alikipata ndani ya Hekalu la Bwana.

2 Wafalme 23:28–30

28 Matukio mengine ya utawala wa Yosia na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?

29 Yosia alipokuwa mfalme, Farao Neko mfalme wa Misri akapanda mpaka Mto Frati kumsaidia mfalme wa Ashuru. Mfalme Yosia akatoka kwenda kupigana naye, lakini Neko akamkabili na kumuua huko Megido. 30 Watumishi wa Yosia wakauleta mwili wake katika gari la vita kutoka Megido hadi Yerusalemu, wakamzika kwenye kaburi lake mwenyewe. Nao watu wa nchi wakamchukua Yehoahazi mwana wa Yosia, wakamtia mafuta na kumfanya mfalme mahali pa baba yake.