Sehemu ya 7: Agano na Noa
2347 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
13 Katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza ya mwaka 601, wa kuishi kwake Noa, maji yalikuwa yamekauka duniani. Kisha Noa akafungua mlango wa safina akaona ya kuwa uso wa ardhi ulikuwa umekauka. 14 Katika siku ya ishirini na saba ya mwezi wa pili dunia ilikuwa imekauka kabisa.
15 Ndipo Mungu akamwambia Noa, 16 “Toka ndani ya safina, wewe na mkeo na wanao na wake zao. 17 Utoe nje kila aina ya kiumbe hai aliye pamoja nawe: Ndege, wanyama na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi, ili wakazae, na kuongezeka na kuijaza tena dunia.”
18 Kwa hiyo Noa akatoka nje pamoja na mkewe, wanawe na wake zao. 19 Wanyama wote na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi na ndege wote, kila kitu kiendacho juu ya nchi, aina moja baada ya nyingine vikatoka katika safina, kila aina ya kiumbe, kimoja baada ya kingine.
20 Kisha Noa akamjengea Bwana madhabahu, akachukua baadhi ya wale wanyama na ndege wote walio safi, akatoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. 21 Bwana akasikia harufu nzuri ya kupendeza, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena ardhi kwa sababu ya mwanadamu, hata ingawa kila mwelekeo wa moyo wake ni mbaya tangu ujana. Kamwe sitaangamiza tena viumbe hai vyote kama nilivyofanya.
22 “Kwa muda dunia idumupo,
wakati wa kupanda na wa kuvuna,
wakati wa baridi na wa joto,
wakati wa kiangazi na wa masika,
usiku na mchana
kamwe havitakoma.”
9:1 Ndipo Mungu akambariki Noa na wanawe, akiwaambia, “Zaeni mkaongezeke kwa idadi na mkaijaze tena dunia. 2 Wanyama wote wa duniani, ndege wote wa angani, kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi, na samaki wote wa baharini wamekabidhiwa mikononi mwenu, nao watawaogopa na kuwahofu. 3 Kila kitu chenye uhai kiendacho kitakuwa chakula chenu. Kama vile nilivyowapa mimea mbalimbali, sasa nawapa kila kitu.
4 “Lakini kamwe msile nyama ambayo bado ina damu ya uhai wake, kwa maana damu ni uhai. 5 Hakika damu ya uhai wenu nitaidai. Nitaidai kutoka kwa kila mnyama. Kutoka kwa kila mwanadamu pia nitaidai kwa ajili ya uhai wa mtu mwenzake.
6 “Yeyote amwagaye damu ya mwanadamu,
damu yake itamwagwa na mwanadamu,
kwa kuwa katika mfano wa Mungu,
Mungu alimuumba mwanadamu.
7 Kuhusu ninyi, zaeni mwongezeke kwa wingi, mzidi katika dunia na kuijaza.”
8 Ndipo Mungu akamwambia Noa na wanawe pamoja naye: 9 “Sasa mimi ninaweka Agano langu nanyi, pamoja na uzao wenu baada yenu, 10 pia na kila kiumbe hai kilichokuwa pamoja nanyi: Ndege, wanyama wa kufugwa na wanyama wote wa porini, wale wote waliotoka katika safina pamoja nanyi, kila kiumbe hai duniani. 11 Ninaweka Agano nanyi: Kamwe uhai hautafutwa tena kwa gharika, kamwe haitakuwepo tena gharika ya kuangamiza dunia.”
12 Mungu akasema, “Hii ni ishara ya Agano ninalofanya kati yangu na ninyi na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi, Agano kwa vizazi vyote vijavyo: 13 Nimeweka upinde wangu wa mvua mawinguni, nao utakuwa ishara ya Agano nifanyalo kati yangu na dunia. 14 Wakati wowote ninapotanda mawingu juu ya dunia na upinde wa mvua ukijitokeza mawinguni, 15 nitakumbuka Agano langu kati yangu na ninyi na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina. Kamwe maji hayatakuwa tena gharika ya kuangamiza uhai wote. 16 Wakati wowote upinde wa mvua unapotokea mawinguni, nitauona na kukumbuka Agano la milele kati ya Mungu na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina duniani.”
17 Hivyo Mungu akamwambia Noa, “Hii ndiyo ishara ya Agano ambalo nimelifanya kati yangu na viumbe vyote vilivyo hai duniani.”