Pambano Kuu la Kanisa na Adui Zake
Unabii kuhusu mapambano makuu yajayo kati ya kanisa na maadui wake, na kuhusu kuongoka kwa Wayahudi katika siku za mwisho.
587 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, kaza uso wako dhidi ya Gogu, katika nchi ya Magogu, mkuu wa Roshi, Mesheki na Tubali, tabiri dhidi yake 3 na useme: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ee Gogu, mimi ni kinyume nawe, mtawala mkuu wa Roshi, Mesheki na Tubali. 4 Nitakugeuza kuelekea ulikotoka na kukutia ndoana kwenye mataya yako na kukutoa nje wewe pamoja na jeshi lako lote, yaani, farasi wako, wapanda farasi wako waliojiandaa tayari kwa vita, pamoja na kundi kubwa la wajeuri wakiwa na ngao na vigao, wote wakipunga panga zao. 5 Uajemi, Kushi na Putu watakuwa pamoja nao, wote wakiwa na ngao na kofia za chuma, 6 pia Gomeri pamoja na vikosi vyake vyote, na Beth-Togarma kutoka kaskazini ya mbali pamoja na vikosi vyake vyote, mataifa mengi wakiwa pamoja nawe.
7 “ ‘Jiandae, uwe tayari, wewe na makundi yako yote ya wajeuri yaliyokusanyika pamoja nawe, nawe waamrishe. 8 Baada ya siku nyingi utaitwa vitani. Katika miaka ijayo, utaivamia nchi ile ambayo imepona kutoka vita, ambayo watu wake walikusanywa kutoka mataifa mengi kuja katika milima ya Israeli, ambayo kwa muda mrefu ilikuwa imeachwa ukiwa. Wameletwa kutoka mataifa na sasa wote wanaishi katika hali ya salama. 9 Wewe na vikosi vyako vyote na mataifa mengi yaliyo pamoja nawe mtapanda juu, mtawazoa kama tufani na kuifunika nchi kama wingu.
10 “ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Katika siku ile mawazo yataingia moyoni mwako nawe utapanga mipango mibaya. 11 Utasema, “Nitapigana vita na nchi ambayo vijiji vyake havina maboma. Nitawashambulia watu wanaoishi kwa amani na wasiotarajia vita: wote wanaishi bila maboma na bila malango na makomeo. 12 Nitateka mateka na kuchukua nyara mali za wale waliorudi kuishi katika mahame na wale watu waliokusanywa kutoka kwa mataifa, ambao sasa wana mifugo na mali nyingi, wanaoishi katikati ya nchi.” 13 Sheba na Dedani pamoja na wafanyabiashara wa Tarshishi na vijiji vyake vyote watakuambia, “Je, umekuja kuteka mateka? Je, umekusanya makundi yako ya wajeuri ili kuchukua nyara mali, kutwaa fedha na dhahabu, kutunyangʼanya mifugo na mali na kuteka nyara nyingi zaidi?” ’
14 “Kwa hiyo, mwanadamu, tabiri na umwambie Gogu: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Katika siku ile, watu wangu Israeli watakapokuwa wanaishi salama, Je, wewe mwenyewe hutalijua hilo? 15 Utakuja kutoka kwako huko kaskazini ya mbali, ukiwa pamoja na mataifa mengi, wote wakiwa wamepanda farasi, kundi kubwa, jeshi kuu. 16 Utakuja dhidi ya watu wangu Israeli kama wingu lifunikavyo nchi. Siku zijazo, ee Gogu, nitakuleta wewe dhidi ya nchi yangu, ili kwamba mataifa wapate kunijua Mimi nitakapojionyesha mtakatifu kwa kukupitia wewe mbele ya macho yao.
17 “ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Je, wewe si yule niliyenena juu yako katika siku za zamani kwa kupitia kwa watumishi wangu manabii wa Israeli? Wakati ule walitabiri kwa miaka mingi kwamba ningekuleta upigane nao. 18 Hili ndilo litakalotokea katika siku ile: Gogu atakaposhambulia nchi ya Israeli, hasira yangu kali itaamka, asema Bwana Mwenyezi. 19 Katika wivu wangu na ghadhabu yangu kali ninasema kuwa wakati ule patakuwepo tetemeko kuu katika nchi ya Israeli. 20 Samaki wa baharini, ndege wa angani, wanyama wa kondeni, kila kiumbe kitambaacho ardhini, na watu wote walio juu ya uso wa nchi watatetemeka mbele zangu. Milima itapinduka, majabali yatapasuka na kila ukuta utaanguka chini. 21 Nitaita upanga vita dhidi ya Gogu juu ya milima yangu yote, asema Bwana Mwenyezi. Upanga wa kila mtu utakuwa dhidi ya ndugu yake. 22 Nitatekeleza hukumu juu yake kwa tauni na kwa umwagaji wa damu. Nitaifanya mvua ya mafuriko kunyesha, mvua ya mawe na moto wa kiberiti juu yake na juu ya vikosi vyake na juu ya mataifa mengi walio pamoja naye. 23 Nami hivyo ndivyo nitakavyoonyesha ukuu wangu na utakatifu wangu, nami nitajijulisha mbele ya macho ya mataifa mengi. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.’
39:1 “Mwanadamu, tabiri dhidi ya Gogu useme: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ee Gogu mimi ni kinyume nawe, mtawala mkuu wa Roshi, Mesheki na Tubali. 2 Nitakugeuza kuelekea ulikotoka na kukuburuta. Nitakuleta kutoka kaskazini ya mbali na kukupeleka wewe dhidi ya milima ya Israeli. 3 Kisha nitaupiga upinde wako kutoka mkono wako wa kushoto na kuifanya mishale ianguke kutoka mkono wako wa kuume. 4 Utaanguka kwenye milima ya Israeli, wewe pamoja na vikosi vyako vyote na yale mataifa yaliyo pamoja nawe. Nitakutoa uwe chakula cha ndege wa aina zote walao nyama na cha wanyama wa mwituni. 5 Utaanguka katika uwanja, kwa kuwa nimenena, asema Bwana Mwenyezi. 6 Nitatuma moto juu ya Magogu na kwa wale wanaoishi kwa salama huko pwani, nao watajua kwamba Mimi ndimi Bwana.
7 “ ‘Nitalifanya Jina langu takatifu lijulikane miongoni mwa watu wangu Israeli. Sitaliacha tena Jina langu takatifu litiwe unajisi, nayo mataifa watajua kuwa Mimi Bwana ndimi Aliye Mtakatifu wa Israeli. 8 Hili jambo linakuja! Hakika litatokea, asema Bwana Mwenyezi. Hii ndiyo siku ile niliyosema habari zake.
9 “ ‘Ndipo wale wanaoishi katika miji ya Israeli watakapotoka na kutumia hizo silaha kuwashia moto na kuziteketeza, yaani, kigao na ngao, pinde na mishale, rungu za vita na mikuki. Kwa miaka saba watavitumia kama kuni. 10 Hawatahitaji kukusanya kuni kutoka mashambani wala kukata kuni kutoka kwenye misitu, kwa sababu watatumia silaha kuwa kuni. Nao watawateka mateka wale waliowateka na kuchukua nyara mali za wale waliochukua mali zao nyara, asema Bwana Mwenyezi.
11 “ ‘Siku ile nitampa Gogu mahali pa kuzikia katika Israeli, katika bonde la wale wasafirio upande wa mashariki kuelekea baharini. Jambo hili litazuia njia ya wasafiri kwa sababu Gogu na makundi yake yote ya wajeuri watazikwa huko. Kwa hiyo litaitwa Bonde la Hamon-Gogu.
12 “ ‘Kwa miezi saba nyumba ya Israeli itakuwa ikiwazika ili kuisafisha nchi. 13 Watu wote wa nchi watawazika, nayo siku nitakayotukuzwa itakuwa siku ya kumbukumbu kwa ajili yao, asema Bwana Mwenyezi.
14 “ ‘Watu wataajiriwa mara kwa mara kuisafisha nchi. Baadhi yao watapita nchini kote na zaidi yao hao wengine, watawazika wale waliosalia juu ya uso wa nchi. Mwisho wa hiyo miezi saba wataanza upekuzi wao. 15 Wakati wanapopita nchini kote na mmoja wao akaona mfupa wa mwanadamu, ataweka alama kando yake mpaka wachimba kaburi wawe wameuzika katika Bonde la Hamon-Gogu. 16 (Pia mji uitwao Hamona utakuwa humo.) Hivyo ndivyo watakavyoisafisha nchi.’
17 “Mwanadamu, hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ita kila aina ya ndege na wanyama wote wa mwituni, waambie: ‘Kusanyikeni mje pamoja kutoka pande zote kwa ajili ya dhabihu ninayowaandalia, dhabihu kuu katika milima ya Israeli. Huko mtakula nyama na kunywa damu. 18 Mtakula nyama za watu mashujaa na kunywa damu za wakuu wa dunia kana kwamba ni za kondoo dume na kondoo wake, mbuzi na mafahali, wote walionona kutoka Bashani. 19 Katika dhabihu ninayoandaa kwa ajili yenu, mtakula mafuta mpaka mkinai na kunywa damu mpaka mlewe. 20 Kwenye meza yangu watajishibisha kwa farasi na wapanda farasi, watu mashujaa na askari wa kila aina,’ asema Bwana Mwenyezi.
21 “Nitauonyesha utukufu wangu miongoni mwa mataifa, nayo mataifa yote wataiona adhabu nitakayotoa na mkono wangu nitakaouweka juu yao. 22 Kuanzia siku ile na kuendelea nyumba ya Israeli itajua kuwa Mimi ndimi Bwana, Mungu wao. 23 Na mataifa watajua kuwa nyumba ya Israeli walikwenda utumwani kwa ajili ya dhambi yao, kwa sababu hawakuwa waaminifu kwangu. Hivyo niliwaficha uso wangu na kuwatia mikononi mwa adui zao, nao wote wakaanguka kwa upanga. 24 Niliwatendea sawasawa na uchafu wao na makosa yao, nami nikawaficha uso wangu.
25 “Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Sasa nitamrudisha Yakobo kutoka utumwani, nami nitawahurumia watu wote wa Israeli, nami nitakuwa na wivu kwa ajili ya Jina langu takatifu. 26 Wataisahau aibu yao na jinsi walivyoonyesha kutokuwa waaminifu kwangu mimi wakati waliishi salama katika nchi yao, bila kuwa na mtu yeyote wa kuwatia hofu. 27 Nitakapokuwa nimewarudisha kutoka mataifa na kuwakusanya kutoka nchi za adui zao, mimi nitajionyesha kuwa mtakatifu kwa kupitia kwao machoni mwa mataifa mengi. 28 Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana, Mungu wao, ingawa niliwapeleka uhamishoni miongoni mwa mataifa, nitawakusanya tena katika nchi yao wenyewe, bila kumwacha yeyote nyuma. 29 Sitawaficha tena uso wangu, kwa maana nitamimina Roho wangu juu ya nyumba ya Israeli, asema Bwana Mwenyezi.”