Utukufu na Ushindi wa Kanisa wa Wakati Ujao (continued)
710 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 “Nilijifunua kwa watu wale ambao hawakuniulizia.
Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta.
Kwa taifa lile ambalo halikuliita Jina langu,
nilisema, ‘Niko hapa, niko hapa.’
2 Mchana kutwa nimeinyoosha mikono yangu
kwa watu wakaidi,
wanaokwenda katika njia ambazo si nzuri,
wafuatao mawazo yao wenyewe:
3 taifa ambalo daima hunikasirisha
machoni pangu,
wakitoa dhabihu katika bustani
na kufukiza uvumba juu ya madhabahu za matofali;
4 watu waketio katikati ya makaburi
na kukesha mahali pa siri,
walao nyama za nguruwe,
nazo sufuria zao zina mchuzi wa nyama zilizo najisi,
5 wasemao, ‘Kaa mbali; usinikaribie,
kwa maana mimi ni mtakatifu mno kwako!’
Watu wa aina hiyo ni moshi katika pua zangu,
ni moto uwakao mchana kutwa.
6 “Tazama, jambo hili hubakia limeandikwa mbele zangu:
sitanyamaza, bali nitalipiza kwa ukamilifu;
nitalipiza mapajani mwao:
7 dhambi zenu na dhambi za baba zenu,”
asema Bwana.
“Kwa sababu walitoa dhabihu za kuteketezwa juu ya milima
na kunichokoza mimi juu ya vilima,
nitawapimia mapajani mwao
malipo makamilifu kwa matendo yao ya zamani.”
8 Hili ndilo asemalo Bwana:
“Kama vile divai mpya ingali bado inapatikana
katika kishada cha zabibu,
nao watu husema, ‘Usikiharibu,
kwa kuwa bado kuna kitu kizuri ndani yake,’
hivyo ndivyo nitakavyofanya kwa ajili ya watumishi wangu;
sitawaangamiza wote.
9 Nitawaleta wazao kutoka kwa Yakobo,
na kutoka kwa Yuda wale watakaomiliki milima yangu,
nao watu wangu wateule watairithi,
nako huko wataishi watumishi wangu.
10 Sharoni itakuwa malisho
kwa ajili ya makundi ya kondoo,
na Bonde la Akori mahali pa kupumzikia
kwa makundi ya ngʼombe,
kwa ajili ya watu wangu wanaonitafuta.
11 “Bali kwenu ninyi mnaomwacha Bwana
na kuusahau mlima wangu mtakatifu,
ninyi mnaoandaa meza kwa ajili ya Bahati,
na kujaza mabakuli ya mvinyo uliochanganywa
kwa ajili ya Ajali,
12 nitawaagiza mfe kwa upanga,
nanyi nyote mtainama chini ili kuchinjwa;
kwa kuwa niliwaita lakini hamkuitika,
nilisema lakini hamkusikiliza.
Mlitenda maovu machoni pangu,
nanyi mkachagua mambo yale yanayonichukiza.”
13 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:
“Watumishi wangu watakula,
lakini ninyi mtaona njaa;
watumishi wangu watakunywa
lakini ninyi mtaona kiu;
watumishi wangu watafurahi,
lakini ninyi mtaona haya.
14 Watumishi wangu wataimba
kwa furaha ya mioyo yao,
lakini ninyi mtalia
kutokana na uchungu wa moyoni,
na kupiga yowe kwa sababu
ya uchungu wa roho zenu.
15 Mtaliacha jina lenu
kuwa laana kwa watu wangu waliochaguliwa;
Bwana Mwenyezi atawaua ninyi,
lakini watumishi wake atawapa jina jingine.
16 Yeye aombaye baraka katika nchi
atafanya hivyo kwa Mungu wa kweli;
yeye aapaye katika nchi
ataapa kwa Mungu wa kweli.
Kwa kuwa taabu za zamani zitasahaulika
na kufichwa kutoka machoni pangu.
17 “Tazama, nitaumba
mbingu mpya na dunia mpya.
Mambo ya zamani hayatakumbukwa,
wala hayatakuja akilini.
18 Lakini furahini na kushangilia daima
katika hivi nitakavyoumba,
kwa kuwa nitaumba Yerusalemu uwe wa kupendeza,
nao watu wake wawe furaha.
19 Nami nitaifurahia Yerusalemu
na kuwafurahia watu wangu;
sauti ya maombolezo na ya kilio
haitasikika humo tena.
20 “Kamwe hatakuwepo tena ndani yake
mtoto mchanga atakayeishi siku chache tu,
au mzee ambaye hataishi akatimiza miaka yake.
Yeye atakayekufa akiwa na umri wa miaka mia moja
atahesabiwa kwamba ni kijana tu,
yeye ambaye hatafika miaka mia moja,
atahesabiwa kuwa amelaaniwa.
21 Watajenga nyumba na kuishi ndani yake;
watapanda mashamba ya mizabibu na kula matunda yake.
22 Hawatajenga nyumba, nao watu wengine waishi ndani yake,
au kupanda mazao na wengine wale.
Kwa kuwa kama zilivyo siku za mti,
ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu,
wateule wangu watafurahia kwa siku nyingi
kazi za mikono yao.
23 Hawatajitaabisha kwa kazi bure,
wala hawatazaa watoto ili wapatwe na majanga,
kwa kuwa watakuwa taifa lililobarikiwa na Bwana,
wao na wazao wao pamoja nao.
24 Kabla hawajaita, nitajibu,
nao wakiwa katika kunena, nitasikia.
25 Mbwa mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja,
naye simba atakula nyasi kama maksai,
lakini mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka.
Hawatadhuru wala kuharibu
katika mlima wangu mtakatifu wote,”
asema Bwana.
66:1 Hili ndilo asemalo Bwana,
“Mbingu ni kiti changu cha enzi,
nayo dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu.
Iko wapi nyumba mtakayoijenga kwa ajili yangu?
Mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi?
2 Je, mkono wangu haukufanya vitu hivi vyote,
hivyo vikapata kuwepo?”
asema Bwana.
“Mtu huyu ndiye ninayemthamini:
yeye ambaye ni mnyenyekevu
na mwenye roho yenye toba,
atetemekaye asikiapo neno langu.
3 Lakini yeyote atoaye dhabihu ya fahali
ni kama yeye auaye mtu,
na yeyote atoaye sadaka ya mwana-kondoo,
ni kama yule avunjaye shingo ya mbwa.
Yeyote atoaye sadaka ya nafaka,
ni kama yule aletaye damu ya nguruwe,
na yeyote afukizaye uvumba wa kumbukumbu,
ni kama yule aabuduye sanamu.
Wamejichagulia njia zao wenyewe,
nazo nafsi zao zinafurahia machukizo yao.
4 Hivyo, mimi pia nitawachagulia mapigo makali,
nami nitaleta juu yao kile wanachokiogopa.
Kwa maana nilipoita, hakuna yeyote aliyejibu,
niliposema, hakuna yeyote aliyesikiliza.
Walifanya maovu machoni pangu
na kuchagua lile linalonichukiza.”
5 Sikieni neno la Bwana,
ninyi mtetemekao kwa neno lake:
“Ndugu zenu wanaowachukia ninyi
na kuwatenga ninyi kwa sababu ya Jina langu, wamesema,
‘Bwana na atukuzwe,
ili tupate kuona furaha yenu!’
Hata sasa wataaibika.
6 Sikieni hizo ghasia kutoka mjini,
sikieni hizo kelele kutoka hekaluni!
Ni sauti ya Bwana ikiwalipa adui zake
yote wanayostahili.
7 “Kabla hajasikia utungu, alizaa;
kabla hajapata maumivu,
alizaa mtoto mwanaume.
8 Ni nani amepata kusikia jambo kama hili?
Ni nani amepata kuona mambo kama haya?
Je, nchi yaweza kuzaliwa kwa siku moja,
au taifa laweza kutokea mara?
Mara Sayuni alipoona utungu,
alizaa watoto wake.
9 Je, nilete mwana hadi wakati wa kuzaliwa
na nisizalishe?” asema Bwana.
“Je, nifunge tumbo la uzazi
wakati mimi ndiye nizalishaye?”
asema Mungu wako.
10 “Shangilieni pamoja na Yerusalemu na mfurahi kwa ajili yake,
ninyi nyote mnaompenda,
shangilieni kwa nguvu pamoja naye,
ninyi nyote mnaoomboleza juu yake.
11 Kwa kuwa mtanyonya na kutosheka
katika faraja ya matiti yake;
mtakunywa sana,
na kuufurahia wingi wa mafuriko ya ustawi wake.”
12 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana:
“Nitamwongezea amani kama mto,
nao utajiri wa mataifa kama kijito kifurikacho;
utanyonya na kuchukuliwa mikononi mwake
na kubembelezwa magotini pake.
13 Kama mama anavyomfariji mtoto wake,
ndivyo nitakavyokufariji wewe,
nawe utafarijiwa huko Yerusalemu.”
14 Wakati mtakapoona jambo hili, mioyo yenu itashangilia,
nanyi mtastawi kama majani;
mkono wa Bwana utajulikana kwa watumishi wake,
bali ghadhabu yake kali
itaonyeshwa kwa adui zake.
15 Tazama, Bwana anakuja na moto,
magari yake ya vita ni kama upepo wa kisulisuli,
atateremsha hasira yake kwa ghadhabu kali,
na karipio lake pamoja na miali ya moto.
16 Kwa maana kwa moto na kwa upanga wake
Bwana atatekeleza hukumu juu ya watu wote,
nao wengi watakuwa ni wale
waliouawa na Bwana.
17 “Watu wote wanaojiweka wakfu na kujitakasa wenyewe ili kwenda bustanini, wakimfuata aliye katikati ya wale ambao hula nyama za nguruwe na panya pamoja na vitu vingine vilivyo machukizo, watafikia mwisho wao pamoja,” asema Bwana.
18 “Nami, kwa sababu ya matendo yao na mawazo yao, niko karibu kuja na kukusanya mataifa yote na lugha zote, nao watakuja na kuuona utukufu wangu.
19 “Nitaweka ishara katikati yao, nami nitapeleka baadhi ya hao walionusurika kwa mataifa, hadi Tarshishi, kwa Puli na Waludi (wanaojulikana kama wapiga upinde), kwa Tubali na Uyunani, hadi visiwa vya mbali ambavyo havijasikia juu ya sifa zangu au kuuona utukufu wangu. Watatangaza utukufu wangu miongoni mwa mataifa. 20 Nao watawaleta ndugu zenu wote, kutoka mataifa yote, mpaka kwenye mlima wangu mtakatifu katika Yerusalemu kama sadaka kwa Bwana, juu ya farasi, katika magari ya vita na magari makubwa, juu ya nyumbu na ngamia,” asema Bwana. “Watawaleta, kama Waisraeli waletavyo sadaka zao za nafaka, katika Hekalu la Bwana, katika vyombo safi kwa kufuata desturi za ibada. 21 Nami nitachagua baadhi yao pia wawe makuhani na Walawi,” asema Bwana.
22 “Kama vile mbingu mpya na nchi mpya ninazozifanya zitakavyodumu mbele zangu,” asema Bwana, “ndivyo jina lenu na wazao wenu watakavyodumu. 23 Kutoka Mwezi Mpya hata mwingine, na kutoka Sabato hadi nyingine, wanadamu wote watakuja na kusujudu mbele zangu,” asema Bwana. 24 “Nao watatoka nje na kuona maiti za wale walioniasi mimi. Funza wao hawatakufa, wala moto wao hautazimika, nao watakuwa kitu cha kuchukiza sana kwa wanadamu wote.”