Kutekwa kwa Ai
1451 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Lakini Waisraeli hawakuwa waaminifu kuhusu vile vitu vilivyowekwa wakfu; Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, alivichukua baadhi ya hivyo vitu. Hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Israeli.
2 Basi Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko waende Ai, karibu na Beth-Aveni mashariki ya Betheli, akawaambia, “Pandeni mkaipeleleze nchi.” Basi wale watu wakapanda wakaipeleleza Ai.
3 Waliporudi kwa Yoshua, wakasema, “Si lazima watu wote waende kupigana na Ai. Watume watu elfu mbili au tatu wakauteke huo mji. Usiwachoshe watu wote, kwa sababu huko kuna watu wachache tu.” 4 Basi wakapanda kama watu elfu tatu tu, lakini wakashambuliwa na watu wa Ai, 5 ambao waliwaua watu kama thelathini na sita miongoni mwao. Wakawafukuza Waisraeli kutoka lango la mji hadi Shebarimu, nao wakawauwa huko kwenye materemko. Kutokana na hili mioyo ya watu ikayeyuka ikawa kama maji.
6 Ndipo Yoshua akayararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya Sanduku la Bwana, na akabakia hapo mpaka jioni. Wazee wa Israeli nao wakafanya vivyo hivyo wakatia mavumbi vichwani mwao. 7 Yoshua akasema, “Ee Bwana Mwenyezi, kwa nini umewavusha watu hawa ngʼambo ya Yordani ili kututia mikononi mwa Waamori watuangamize? Laiti tungeliridhika kukaa ngʼambo ile nyingine ya Yordani! 8 Ee Bwana, niseme nini sasa, ikiwa sasa Israeli ameshafukuzwa na adui zake? 9 Wakanaani na watu wengine wa nchi watasikia habari hii, nao watatuzunguka na kutufutilia jina letu duniani. Utafanya nini basi kwa ajili ya jina lako mwenyewe lililo kuu?”
10 Bwana akamwambia Yoshua, “Simama! Unafanya nini hapo chini kifudifudi? 11 Israeli ametenda dhambi. Wamekiuka agano langu nililowaamuru kulishika. Wamechukua baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu, wameiba, wamesema uongo, wameviweka pamoja na mali zao. 12 Ndiyo sababu Waisraeli hawawezi kusimama dhidi ya adui zao. Wanawapa visogo na kukimbia kwa kuwa wanastahili maangamizi. Sitakuwa pamoja nanyi tena mpaka mwangamize kila kitu miongoni mwenu kilichotengwa kwa maangamizi.
13 “Nenda, ukawatakase watu. Waambie, ‘Jitakaseni mjiandae kwa kesho; kwa sababu hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Kitu kilichowekwa wakfu kipo katikati yenu, ee Israeli. Hamwezi kusimama dhidi ya adui zenu mpaka mtakapokiondoa.
14 “ ‘Asubuhi, mjihudhurishe kabila kwa kabila. Itakuwa kabila lile atakalolitwaa Bwana litakuja mbele ukoo kwa ukoo, ukoo ule atakaoutwaa Bwana utakuja mbele jamaa kwa jamaa, nayo jamaa ile atakayoitwaa Bwana itakuja mbele mtu kwa mtu. 15 Yule atakayekutwa na vitu vilivyowekwa wakfu, atateketezwa kwa moto, pamoja na vitu vyote alivyo navyo. Kwa kuwa amelivunja agano la Bwana na kufanya kitu cha aibu katika Israeli!’ ”
16 Kesho yake asubuhi na mapema Yoshua akawaamuru Israeli kuja mbele kabila kwa kabila; na Yuda akatwaliwa. 17 Koo za Yuda zikaja mbele, naye akawatwaa Wazera. Akaamuru ukoo wa Wazera kuja mbele jamaa kwa jamaa, nayo jamaa ya Zabdi ikatwaliwa. 18 Yoshua akaamuru watu wa jamaa ya Zabdi kuja mbele mtu kwa mtu, naye Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, akatwaliwa.
19 Ndipo Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, mtukuze Bwana, Mungu wa Israeli, nawe ukiri kwake. Niambie ni nini ulichotenda; usinifiche.”
20 Akani akamjibu Yoshua, “Ni kweli! Nimetenda dhambi dhidi ya Bwana, Mungu wa Israeli. Hili ndilo nililofanya: 21 Nilipoona katika nyara joho zuri la kutoka Babeli, shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu ya uzito wa shekeli hamsini, nikavitamani na nikavichukua. Tazama, vimefichwa ardhini ndani ya hema langu, pamoja na hiyo fedha chini yake.”
22 Kwa hiyo Yoshua akatuma wajumbe, nao wakapiga mbio mpaka hemani, tazama, vile vitu vilikuwa vimefichwa hemani mwake, pamoja na ile fedha chini yake. 23 Wakavichukua vile vitu toka mle hemani, wakamletea Yoshua pamoja na Waisraeli wote, na wakavitandaza mbele za Bwana.
24 Basi Yoshua, pamoja na Israeli yote, wakamchukua Akani mwana wa Zera, pamoja na ile fedha, lile joho, ile kabari ya dhahabu, wanawe na binti zake, ngʼombe, punda na kondoo wake, hema yake pamoja na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta katika Bonde la Akori. 25 Yoshua akasema, “Kwa nini umeleta taabu hii juu yetu? Bwana ataleta taabu juu yako leo hii.”
Ndipo Israeli yote ikampiga Akani kwa mawe, na baada ya kuwapiga jamaa yake yote kwa mawe, wakawateketeza kwa moto. 26 Wakakusanya lundo la mawe juu ya Akani, ambalo lipo mpaka leo. Naye Bwana akageuka kutoka hasira yake kali. Kwa hiyo mahali pale pakaitwa Bonde la Akori tangu siku hiyo.
8:1 Ndipo Bwana akamwambia Yoshua, “Usiogope, wala usivunjike moyo. Chukua jeshi lote la vita uende pamoja nalo kuishambulia Ai. Kwa kuwa nimeshamweka mikononi mwako mfalme wa Ai, pamoja na watu wake, mji wake na nchi yake. 2 Utafanya Ai na mfalme wake kama ulivyofanya kwa mji wa Yeriko na mfalme wake, isipokuwa mnaweza kuchukua mateka wake na mifugo wake, kwa ajili yenu. Weka waviziaji upande wa nyuma ya mji.”
3 Basi Yoshua na jeshi lote wakainuka kushambulia Ai. Akachagua watu mashujaa elfu thelathini walio bora miongoni mwa wapiganaji wake, akawapeleka wakati wa usiku 4 akiwaagiza: “Sikilizeni kwa makini. Mtavizia nyuma ya mji. Msiende mbali sana na mji. Wote kuweni macho. 5 Mimi na watu walio pamoja nami, tutaukabili mji, kisha itakuwa hapo watu watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo kwanza, sisi tutawakimbia. 6 Watatufuatilia mpaka tutakapokuwa tumewavuta mbali na mji kwa kuwa watasema, ‘Wanatukimbia, kama walivyofanya hapo awali.’ Hivyo tutakapowakimbia, 7 ninyi inawapasa mwinuke mtoke huko mafichoni na kuuteka mji. Bwana Mungu wenu atautia mkononi mwenu. 8 Mtakapokuwa mmeuteka mji, uteketezeni kwa moto. Fanyeni kama vile Bwana alivyoamuru. Angalieni, nimewaagiza.”
9 Ndipo Yoshua akawatuma watu, nao wakaenda mahali pa kujificha, wakawa wanavizia kati ya Betheli na Ai, kuelekea upande wa magharibi wa Ai, lakini Yoshua akalala miongoni mwa watu usiku huo.
10 Asubuhi na mapema siku iliyofuatia, Yoshua akawakutanisha watu wake, na yeye na viongozi wa Israeli wakawa mbele ya watu kwenda Ai. 11 Watu wote wa vita waliokuwa pamoja naye walipanda, wakakaribia na kufika mbele ya mji. Wakapiga kambi kaskazini mwa Ai, pakiwa na bonde kati yao na huo mji. 12 Yoshua alikuwa amewachukua watu wapatao elfu tano, akawaweka katika uavizi kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa mji. 13 Wakawaweka askari katika maeneo yao: wale wote waliokuwa kambini wakawa kaskazini ya mji na wale waliokuwa wakivizia wakawa upande wa magharibi. Usiku huo Yoshua akaenda katika lile bonde.
14 Mfalme wa Ai alipoona jambo hili, yeye pamoja na watu wote wa mji wakatoka kwa haraka asubuhi na mapema, ili kukutana na Israeli katika vita mahali fulani panapotazamana na Araba. Lakini hakujua kwamba kulikuwa kumewekwa waviziaji dhidi yake nyuma ya mji. 15 Yoshua na Israeli wote wakaruhusu kurudishwa nyuma mbele yao, na kuelekea jangwani. 16 Watu wote wa Ai wakaitwa ili kuwafuatia, nao wakavutwa kumfuatia Yoshua mbali na mji. 17 Hakuna hata mwanaume mmoja aliyebakia Ai wala Betheli ambaye hakufuatia Israeli. Wakauacha mji wazi na kuwafuatia Israeli.
18 Ndipo Bwana akamwambia Yoshua, “Inua huo mkuki ulio mkononi mwako kuuelekeza Ai, kwa kuwa nitautia huo mji mkononi mwako.” Hivyo Yoshua akauelekeza mkuki wake Ai. 19 Mara tu alipofanya hivi, wale watu waliokuwa mavizioni wakaondoka upesi kutoka mahali pao na kukimbilia mbele. Wakaingia ndani ya mji, wakauteka na kuutia moto kwa haraka.
20 Watu wa Ai wakaangalia nyuma, wakauona moshi wa huo mji ukielekea angani lakini hawakuwa na nafasi ya kutoroka kwa upande wowote, kwa kuwa wale Waisraeli waliokuwa wanawakimbia kuelekea jangwani walikuwa wamegeuka nyuma kuwakabili wakimbizaji wao. 21 Basi Yoshua na Israeli wote walipoona kwamba waviziaji wameshauteka mji na moshi ulikuwa unapaa juu kutoka kwenye mji, wakawageukia watu wa Ai na kuwashambulia. 22 Wale waviziaji nao pia wakatoka nje ya mji dhidi yao, hivi kwamba wakashikiwa katikati, Waisraeli wakiwa pande zote mbili. Israeli wakawaua, bila kuwaachia yeyote aliyenusurika wala aliyetoroka. 23 Lakini wakamchukua mfalme wa Ai akiwa hai na kumleta kwa Yoshua.
24 Israeli ilipomaliza kuwaua wanaume wote wa Ai katika mashamba na jangwani walipokuwa wamewafukuzia, na baada ya kila mmoja wao kuuawa kwa upanga, Waisraeli wote wakarudi Ai na kuwaua wale waliokuwa wamebakia mjini. 25 Watu kumi na mbili elfu, waume kwa wake, waliangamia siku ile, yaani watu wote wa Ai. 26 Kwa maana Yoshua hakuurudisha ule mkono wake uliokuwa umeuinua mkuki hadi alipomaliza kuwaangamiza wote walioishi Ai. 27 Lakini Israeli wakajichukulia mifugo na nyara za mji huu, kama vile Bwana alivyokuwa amemwagiza Yoshua.
28 Kwa hiyo Yoshua akauchoma moto mji wa Ai na kuufanya kuwa lundo la magofu la kudumu, mahali pa ukiwa hadi leo. 29 Akamwangika mfalme wa Ai kwenye mti na kumwacha hapo mpaka jioni. Wakati wa jua kutua, Yoshua akawaamuru wautoe mwili wake kwenye mti na kuutupa kwenye ingilio la lango la mji. Kisha wakalundika mawe makubwa mengi juu yake, ambayo yamesalia mpaka leo.