Sehemu ya 7: Dhambi ya Solomoni

980 hadi 975 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Wafalme 11:1–14

1 Hata hivyo, Mfalme Solomoni akawapenda wanawake wengi wa kigeni zaidi, mbali na binti Farao: wanawake wa Wamoabu, Waamoni, Waedomu, Wasidoni na Wahiti. 2 Walitoka katika mataifa ambayo Bwana aliwaambia Waisraeli, “Msije mkaoana nao, kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu mgeukie miungu yao.” Hata hivyo, Solomoni akakaza kuwapenda. 3 Alikuwa na wake 700 mabinti wa uzao wa kifalme, na masuria 300, nao wake zake wakampotosha. 4 Kadiri Solomoni alivyozidi kuzeeka, wake zake wakaugeuza moyo wake kuelekea miungu mingine, na moyo wake haukujitolea kikamilifu kwa Bwana Mungu wake, kama ulivyokuwa moyo wa Daudi baba yake. 5 Solomoni akafuata Ashtorethi mungu mke wa Wasidoni, na Moleki mungu aliyekuwa chukizo la Waamoni. 6 Kwa hiyo Solomoni akafanya uovu machoni pa Bwana; hakumfuata Bwana kikamilifu kama alivyofanya Daudi baba yake.

7 Kwenye kilima mashariki mwa Yerusalemu, Solomoni akajenga mahali pa juu kwa ajili ya Kemoshi chukizo la Wamoabu, na kwa Moleki mungu chukizo la Waamoni. 8 Akafanya hivyo kwa wake zake wote wa kigeni, ambao walifukiza uvumba na kutoa dhabihu kwa miungu yao.

9 Bwana akamkasirikia Solomoni kwa sababu moyo wake uligeuka mbali na Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye alikuwa amemtokea mara mbili. 10 Ingawa alikuwa amemkataza Solomoni kufuata miungu mingine, Solomoni hakutii amri ya Bwana. 11 Kwa hiyo Bwana akamwambia Solomoni, “Kwa kuwa hii ndiyo hali yako na hukushika Agano langu na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme kutoka kwako na kumpa mmoja wa walio chini yako. 12 Hata hivyo, kwa ajili ya Daudi baba yako, sitafanya jambo hili wakati wa uhai wako. Nitaurarua kutoka mikononi mwa mwanao. 13 Lakini pia sitaurarua ufalme wote kutoka kwake, bali nitampa kabila moja kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu na kwa ajili ya Yerusalemu, ambao nimeuchagua.”

14 Kisha Bwana akamwinua adui dhidi ya Solomoni, Hadadi, Mwedomu, kutoka ukoo wa ufalme wa Edomu.

1 Wafalme 11:23–40

23 Mungu akamwinua adui mwingine dhidi ya Solomoni, Rezoni mwana wa Eliada, ambaye alikuwa amemkimbia bwana wake Hadadezeri, mfalme wa Soba. 24 Akawakusanya watu, naye akawa kiongozi wa kundi la waasi, wakati Daudi alipoangamiza majeshi ya Soba; waasi walikwenda Dameski, mahali walipokaa na kumiliki. 25 Rezoni alikuwa adui wa Israeli kwa muda wote alioishi Solomoni, ukiongezea matatizo yaliyosababishwa na Hadadi. Kwa hiyo Rezoni akatawala katika Aramu na alikuwa mkatili kwa Israeli.

26 Pia, Yeroboamu mwana wa Nebati aliasi dhidi ya mfalme. Alikuwa mmoja wa maafisa wa Solomoni, Mwefraimu kutoka Sereda, ambaye mama yake alikuwa mjane aliyeitwa Serua.

27 Haya ndiyo maelezo ya jinsi alivyomwasi mfalme: Solomoni alikuwa amejenga Milo naye akawa ameziba mwanya katika ukuta wa mji wa Daudi baba yake. 28 Basi Yeroboamu alikuwa mtu shujaa na hodari, naye Solomoni alipoona jinsi kijana alivyofanya kazi yake, akamweka kuwa kiongozi wa kazi yote ya mikono ya nyumba ya Yosefu.

29 Karibu na wakati ule Yeroboamu alikuwa anatoka nje ya Yerusalemu, Ahiya nabii Mshiloni akakutana naye njiani, akiwa amevaa joho jipya. Hawa wawili walikuwa peke yao mashambani, 30 naye Ahiya akachukua joho jipya alilokuwa amevaa akalirarua vipande kumi na viwili. 31 Kisha akamwambia Yeroboamu, “Chukua vipande kumi kwa ajili yako, kwa kuwa hivi ndivyo Bwana, Mungu wa Israeli asemavyo: ‘Tazama, ninakwenda kuuchana ufalme kutoka mikononi mwa Solomoni na kukupa wewe makabila kumi. 32 Lakini kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi na mji wa Yerusalemu, ambao nimeuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli, atakuwa na kabila moja. 33 Nitafanya hivi kwa sababu wameniacha mimi na kuabudu Ashtorethi mungu mke wa Wasidoni, Kemoshi mungu wa Wamoabu, na Moleki mungu wa Waamoni, nao hawakwenda katika njia zangu ili kufanya yaliyo sawa machoni pangu, wala kushika amri na sheria zangu kama Daudi, babaye Solomoni, alivyofanya.

34 “ ‘Lakini sitauondoa ufalme wote kutoka mikononi mwa Solomoni, nimemfanya mtawala siku zote za maisha yake kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, niliyemchagua na ambaye aliyatunza maagizo na amri zangu. 35 Nitauondoa ufalme kutoka mikononi mwa mwanawe na kukupa wewe makabila kumi. 36 Nitampa mwanawe kabila moja ili kwamba Daudi mtumishi wangu awe na taa mbele zangu daima katika Yerusalemu, mji ambao nimeuchagua kuweka Jina langu. 37 Hata hivyo, kukuhusu wewe Yeroboamu, nitakutwaa, nawe utatawala juu ya yote yale moyo wako unayotamani, utakuwa mfalme juu ya Israeli. 38 Ikiwa utafanya kila nitakalokuamuru, kuenenda katika njia zangu na kufanya yaliyo sawa mbele za macho yangu kwa kuzishika amri zangu na maagizo yangu kama alivyofanya Daudi mtumishi wangu, nitakuwa pamoja nawe. Nitakujengea ufalme utakaodumu kama ule niliomjengea Daudi, nami nitakupa Israeli. 39 Nitawatesa wazao wa Daudi kwa ajili ya hili, lakini siyo milele.’ ”

40 Solomoni akajaribu kumuua Yeroboamu, lakini Yeroboamu akakimbilia Misri, kwa Mfalme Shishaki, naye akakaa huko mpaka Solomoni alipofariki.

Mhubiri 1

1 Maneno ya Mhubiri, mwana wa Daudi, mfalme huko Yerusalemu:

2 “Ubatili mtupu! Ubatili mtupu!”

Mhubiri anasema.

“Ubatili mtupu!

Kila kitu ni ubatili.”

3 Mwanadamu anafaidi nini kutokana na kazi yake yote

anayotaabikia chini ya jua?

4 Vizazi huja na vizazi hupita,

lakini dunia inadumu milele.

5 Jua huchomoza na jua huzama,

nalo huharakisha kurudi mawioni.

6 Upepo huvuma kuelekea kusini

na kugeukia kaskazini,

hurudia mzunguko huo huo,

daima ukirudia njia yake.

7 Mito yote hutiririka baharini,

hata hivyo bahari kamwe haijai.

Mahali mito inapotoka,

huko hurudi tena.

8 Vitu vyote vinachosha,

zaidi kuliko mtu anavyoweza kusema.

Jicho kamwe halitosheki kutazama,

wala sikio halishibi kusikia.

9 Kile kilichokuwepo kitakuwepo tena,

kile kilichofanyika kitafanyika tena,

hakuna kilicho kipya chini ya jua.

10 Kuna kitu chochote ambacho mtu anaweza kusema,

“Tazama! Kitu hiki ni kipya”?

Kilikuwepo tangu zamani za kale,

kilikuwepo kabla ya wakati wetu.

11 Hakuna kumbukumbu ya watu wa zamani,

hata na wale ambao hawajaja bado

hawatakumbukwa

na wale watakaofuata baadaye.

12 Mimi, Mhubiri, nilikuwa mfalme wa Israeli katika Yerusalemu. 13 Nilitumia muda wangu wote kujifunza na kuvumbua kwa hekima yote yanayofanyika chini ya mbingu. Jinsi gani Mungu ameweka mzigo mzito juu ya wanadamu! 14 Nimeshaona mambo yote yanayotendeka chini ya jua, hayo yote ni ubatili, hii ni kukimbiza upepo.

15 Kilichopindika hakiwezi kunyooshwa,

kile ambacho hakipo haiwezekani kukihesabu.

16 Niliwaza mwenyewe, “Tazama, nimekua na kuongezeka katika hekima kuliko yeyote aliyewahi kutawala Yerusalemu kabla yangu. Nimekuwa na uzoefu mkubwa wa hekima na maarifa.” 17 Ndipo nilipojitahidi kufahamu kutofautisha hekima, wazimu na upumbavu, lakini nikatambua hata hili nalo ni kukimbiza upepo.

18 Kwa kuwa hekima nyingi huleta huzuni kubwa;

maarifa yanapoongezeka, masikitiko yanaongezeka.