Sehemu ya 7: Dhambi ya Solomoni (continued)

980 hadi 975 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mhubiri 8–9

1 Ni nani aliye kama mtu mwenye hekima?

Ni nani ajuaye maelezo ya mambo?

Hekima hungʼarisha uso wa mtu na kubadili ugumu wa uso wake.

2 Nawaambia, Tii amri ya mfalme, kwa sababu uliapa mbele za Mungu. 3 Usiharakishe kuondoka mbele ya mfalme. Usiendelee kutenda lililo baya, kwa maana mfalme atafanya lolote apendalo. 4 Kwa kuwa neno la mfalme ndilo lenye mamlaka ya mwisho, nani awezaye kumwambia, “Je, wewe unafanya nini?”

5 Yeyote anayetii agizo lake hatadhurika,

moyo wa hekima utajua wakati muafaka

na jinsi ya kutenda.

6 Kwa maana kuna wakati muafaka

na utaratibu wa kila jambo,

ingawa huzuni ya mwanadamu

huwa nzito juu yake.

7 Kwa vile hakuna mtu ajuaye siku zijazo,

ni nani awezaye kumwambia linalokuja?

8 Hakuna mwanadamu

awezaye kushikilia roho yake asife,

wala hakuna mwenye uwezo

juu ya siku ya kufa kwake.

Kama vile hakuna yeyote arudishwaye nyuma wakati wa vita,

kadhalika uovu hautawaweka huru wale wautendao.

9 Yote haya niliyaona, nilipokuwa natafakari kila kitu kinachotendeka chini ya jua. Kuna wakati ambapo mtu hujifanya bwana juu ya wengine kwa madhara yake mwenyewe. 10 Ndipo pia, nikaona waovu wakizikwa, wale ambao walizoea kuingia na kutoka mahali patakatifu na kupewa sifa katika mji ambapo walikuwa wamefanya haya. Hili nalo ni ubatili.

11 Wakati hukumu juu ya tendo ovu haitekelezwi upesi, mioyo ya watu hujaa mipango ya kutenda maovu. 12 Ingawa mtu mwovu hufanya maovu mia moja na akaendelea kuishi maisha marefu, najua kwamba itakuwa bora zaidi kwa watu wanaomwogopa Mungu, wamchao Mungu. 13 Lakini kwa sababu waovu hawamwogopi Mungu, hawatafanikiwa, maisha yao hayatarefuka kama kivuli.

14 Kuna kitu kingine ambacho ni ubatili kinachotokea duniani: Watu waadilifu kupata yale yanayowastahili waovu, nao waovu kupata yale yanayowastahili waadilifu. Hili nalo pia, nasema ni ubatili. 15 Kwa hiyo mimi ninasifu kufurahia maisha, kwa sababu hakuna kitu bora zaidi kwa mwanadamu chini ya jua kuliko kula, kunywa na kufurahi. Kisha furaha itafuatana naye kazini mwake siku zote za maisha yake ambazo amepewa na Mungu chini ya jua.

16 Nilipotafakari akilini mwangu ili nijue hekima na kuangalia kazi ya mwanadamu duniani, jinsi ambavyo macho yake hayapati usingizi mchana wala usiku, 17 ndipo nikaona yale yote ambayo Mungu ameyafanya. Hakuna yeyote awezaye kuelewa yale yanayotendeka chini ya jua. Licha ya juhudi zake zote za kutafuta, mtu hawezi kugundua maana yake. Hata ingawa mtu mwenye hekima anadai kuwa anafahamu, kwa hakika hawezi kutambua.

9:1 Kwa hiyo niliyatafakari yote haya nikafikia uamuzi kwamba waadilifu na wenye hekima na yale wanayoyafanya yako mikononi mwa Mungu, lakini hakuna mtu ajuaye kama anangojewa na upendo au chuki. 2 Wote wanayo hatima inayofanana, mwadilifu na mwovu, mwema na mbaya, aliye safi na aliye najisi, wale wanaotoa dhabihu na wale wasiotoa.

Kama ilivyo kwa mtu mwema,

ndivyo ilivyo kwa mtu mwenye dhambi;

kama ilivyo kwa wale wanaoapa,

ndivyo ilivyo kwa wale wasioapa.

3 Huu ni ubaya ulio katika kila kitu kinachotendeka chini ya jua: Mwisho unaofanana huwapata wote. Zaidi ya hayo, mioyo ya watu, imejaa ubaya na kuna wazimu mioyoni mwao wangali hai, hatimaye huungana na waliokufa. 4 Yeyote aliye miongoni mwa walio hai analo tumaini, hata mbwa hai ni bora kuliko simba aliyekufa!

5 Kwa maana walio hai wanajua kwamba watakufa,

lakini wafu hawajui chochote,

hawana tuzo zaidi,

hata kumbukumbu yao imesahaulika.

6 Upendo wao, chuki yao na wivu wao

vimetoweka tangu kitambo,

kamwe hawatakuwa tena na sehemu

katika lolote linalotendeka chini ya jua.

7 Nenda, kula chakula chako kwa furaha, unywe divai yako kwa moyo wa shangwe, kwa maana sasa Mungu anakubali unachofanya. 8 Daima uvae nguo nyeupe na daima upake kichwa chako mafuta. 9 Furahia maisha na mke wako, umpendaye, siku zote za maisha ya ubatili uliyopewa na Mungu chini ya jua, siku zote za ubatili. Kwa maana hili ndilo fungu lako katika maisha na katika kazi yako ya taabu chini ya jua. 10 Lolote mkono wako upatalo kufanya, fanya kwa nguvu zako zote, kwa kuwa huko kuzimu, unakokwenda, hakuna kufanya kazi wala mipango wala maarifa wala hekima.

11 Nimeona kitu kingine tena chini ya jua:

Si wenye mbio washindao mashindano

au wenye nguvu washindao vita,

wala si wenye hekima wapatao chakula

au wenye akili nyingi wapatao mali,

wala wenye elimu wapatao upendeleo,

lakini fursa huwapata wote.

12 Zaidi ya hayo, hakuna mwanadamu ajuaye wakati saa yake itakapokuja:

Kama vile samaki wavuliwavyo katika wavu mkatili,

au ndege wanaswavyo kwenye mtego,

vivyo hivyo wanadamu hunaswa na nyakati mbaya

zinazowaangukia bila kutazamia.

13 Pia niliona chini ya jua mfano huu wa hekima ambao ulinivutia sana: 14 Palikuwa na mji mdogo uliokuwa na watu wachache ndani yake. Mfalme mwenye nguvu akainuka dhidi yake, akauzunguka akaweka jeshi kubwa dhidi yake. 15 Katika mji huo kulikuwepo mtu mmoja maskini lakini mwenye hekima, naye akauokoa ule mji kwa hekima yake. Lakini hakuna aliyemkumbuka yule maskini. 16 Kwa hiyo, nikasema, “Hekima ni bora kuliko nguvu.” Lakini hekima ya maskini imedharauliwa, wala hakuna anayesikiliza maneno yake.

17 Maneno ya utulivu ya mwenye hekima

husikiwa kuliko makelele ya mtawala wa wapumbavu.

18 Hekima ni bora kuliko silaha za vita,

lakini mwenye dhambi mmoja

huharibu mema mengi.