Sehemu ya 7: Dhambi ya Solomoni (continued)

980 hadi 975 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mhubiri 4–5

1 Nikatazama tena nikaona uonevu wote uliokuwa unafanyika chini ya jua:

Nikaona machozi ya walioonewa,

wala hawana wa kuwafariji;

uwezo ulikuwa upande wa wale wanaowaonea,

wala hawana wa kuwafariji.

2 Nami nikasema kwamba wafu,

waliokwisha kufa,

wana furaha kuliko watu walio hai,

ambao bado wanaishi.

3 Lakini aliye bora kuliko hao wawili

ni yule ambaye hajazaliwa bado,

ambaye hajaona ule uovu

unaofanyika chini ya jua.

4 Tena nikaona kuwa kazi zote na mafanikio yote huchipuka kutokana na wivu wa mtu kwa jirani yake. Hili nalo ni ubatili, ni kukimbiza upepo.

5 Mpumbavu hukunja mikono yake

na kujiangamiza mwenyewe.

6 Afadhali konzi moja pamoja

na utulivu kuliko konzi mbili pamoja na taabu

na kukimbiza upepo.

7 Tena nikaona kitu kingine kilicho ubatili chini ya jua:

8 Kulikuwepo mwanadamu aliye peke yake,

hakuwa na mwana wala ndugu.

Hapakuwa na mwisho wa kazi yake,

hata hivyo macho yake

hayakutosheka na utajiri wake.

Aliuliza, “Ninajitaabisha hivi kwa ajili ya nani,

nami kwa nini ninajinyima kufurahia?”

Hili pia ni ubatili,

ni shughuli yenye taabu!

9 Wawili ni afadhali kuliko mmoja,

kwa sababu wana malipo mazuri kwa kazi yao:

10 Kama mmoja akianguka,

mwenzake atamwinua.

Lakini ni jambo la kuhuzunisha

kwa mtu yule aangukaye

naye hana wa kumwinua!

11 Pia, kama wawili wakilala pamoja

watapashana joto.

Lakini ni vipi mtu aweza

kujipasha joto mwenyewe?

12 Ingawa mtu mmoja aweza kushindwa,

watu wawili wanaweza

kumkabili adui na kumshinda.

Kamba ya nyuzi tatu

haikatiki kwa urahisi.

13 Afadhali kijana maskini mwenye hekima kuliko mfalme mzee mpumbavu ambaye hajui tena kupokea maonyo. 14 Kijana huyo angeweza kutokea gerezani akapata ufalme, au angeweza kuwa amezaliwa katika umaskini kwenye huo ufalme. 15 Nikaona kwamba wote walioishi na kutembea chini ya jua walimfuata kijana, aliyepokea ufalme. 16 Hapakuwa na kikomo cha watu wote aliowatawala. Lakini wale waliokuja baadaye hawakufurahia kazi ya yule aliyepokea ufalme. Hili nalo pia ni ubatili, ni kukimbiza upepo.

5:1 Linda hatua zako uendapo katika nyumba ya Mungu. Karibia usikilize kuliko kutoa dhabihu ya wapumbavu, ambao hawajui kuwa wanafanya kosa.

2 Usiwe mwepesi kuzungumza,

usiwe na haraka katika moyo wako

kuzungumza lolote mbele za Mungu.

Mungu yuko mbinguni

nawe uko duniani,

kwa hiyo maneno yako

na yawe machache.

3 Kama vile ndoto huja

wakati kuna shughuli nyingi,

ndivyo yalivyo mazungumzo ya mpumbavu

wakati kuna maneno mengi.

4 Wakati unapomwekea Mungu nadhiri, usikawie kuitimiza. Yeye hafurahii wapumbavu; timiza nadhiri yako. 5 Ni afadhali usiweke nadhiri kuliko kuiweka na usiitimize. 6 Usiruhusu kinywa chako kukuingiza dhambini. Tena usijitetee mbele ya huyo mjumbe wa hekaluni, ukisema, “Niliweka nadhiri kwa makosa.” Kwa nini Mungu akasirike kwa ajili ya yale unayosema na kuiharibu kazi ya mikono yako? 7 Kuota ndoto kwingi na maneno mengi ni ubatili. Kwa hiyo simama katika kicho cha Mungu.

8 Kama ukiona maskini wanaonewa katika nchi, hukumu na haki vikipotoshwa, usishangazwe na mambo hayo, kwa maana afisa mmoja anaangaliwa na aliye juu yake zaidi na juu ya hao wawili kuna wengine walio juu zaidi yao. 9 Mafanikio ya nchi ni kwa ajili ya wote, hata mfalme mwenyewe hufaidi kutoka mashambani.

10 Yeyote apendaye fedha kamwe

hatosheki na fedha;

yeyote apendaye utajiri kamwe

hatosheki na kipato chake.

Hili nalo pia ni ubatili.

11 Mali ikiongezeka, ndivyo walaji

wanavyoongezeka.

Hii nayo inamfaidia nini mwenye mali

isipokuwa ni kushibisha macho yake?

12 Usingizi wa kibarua ni mtamu,

awe amekula kidogo au kingi,

lakini wingi wa mali

humnyima tajiri usingizi.

13 Nimeshaona uovu mzito chini ya jua:

Utajiri uliolimbikizwa kwa kujinyima

na kuleta madhara kwa mwenye mali,

14 au utajiri uliopotea kwa bahati mbaya,

hivyo kwamba wakati akiwa na mwana

hakuna chochote kilichobaki kwa ajili yake.

15 Mtu hutoka tumboni mwa mama yake uchi,

naye jinsi alivyokuja vivyo hivyo huondoka.

Hachukui chochote kutokana na kazi yake

ambacho anaweza kukibeba mkononi mwake.

16 Hili nalo ni baya la kusikitisha:

Kama vile mtu ajavyo, vivyo hivyo huondoka,

naye anapata faida gani,

maadamu hutaabika kwa ajili ya upepo?

17 Siku zake zote hula gizani,

pamoja na fadhaa kubwa,

mateso na hasira.

18 Ndipo nikatambua kwamba ni vyema na sahihi kwa mtu kula na kunywa na kutosheka katika kazi yake ngumu chini ya jua katika siku chache za maisha yake Mungu alizompa, kwa maana hili ndilo fungu lake. 19 Zaidi ya yote, Mungu anapompa mtu yeyote utajiri na milki, humwezesha kuvifurahia, kukubali fungu lake na kuwa na furaha katika kazi yake, hii ni karama ya Mungu. 20 Mara chache mtu huzifikiri siku za maisha yake, kwa sababu Mungu humfanya ashikwe na furaha ya moyoni.