Uasi wa Sheba, na Njaa
1022 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Basi, kulikuwa na mtu mbaya sana aliyeitwa Sheba mwana wa Bikri, Mbenyamini, aliyekuwako huko. Akapiga tarumbeta na kupaza sauti,
“Hatuna fungu katika Daudi,
wala hatuna sehemu
katika mwana wa Yese!
Kila mtu aende hemani mwake,
enyi Israeli!”
2 Kwa hiyo watu wote wa Israeli wakamwacha Daudi na kumfuata Sheba mwana Bikri. Lakini watu wa Yuda wakawa karibu na mfalme wao katika safari yote kutoka Yordani mpaka Yerusalemu.
4 Ndipo mfalme akamwambia Amasa, “Waite watu wa Yuda waje kwangu katika muda wa siku tatu, nawe mwenyewe uwepo hapa.” 5 Lakini Amasa alipokwenda kuwaita Yuda, alichukua muda mrefu zaidi ya ule mfalme aliokuwa amemwekea.
6 Daudi akamwambia Abishai, “Sasa Sheba mwana wa Bikri atatuletea madhara zaidi kuliko alivyofanya Absalomu. Wachukue watu wa bwana wako na umfuatie, la sivyo atapata mji wenye ngome na kututoroka.” 7 Hivyo watu wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, pamoja na wapiganaji mashujaa wote wakaondoka chini ya uongozi wa Abishai. Wakatoka Yerusalemu ili kumfuata Sheba mwana wa Bikri.
8 Wakati walikuwa kwenye mwamba mkubwa huko Gibeoni, Amasa alikuja kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa mavazi yake ya kijeshi; juu yake alifunga mkanda kwenye kiuno wenye upanga ndani ya ala. Alipokuwa akienda mbele, ule upanga ukaanguka kutoka kwenye ala.
9 Yoabu akamwambia Amasa, “U hali gani, ndugu yangu?” Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kuume ili ambusu. 10 Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu, naye Yoabu akamchoma nao tumboni, nayo matumbo yake yakamwagika chini. Pasipo kuchomwa mara ya pili, Amasa akafa. Basi Yoabu na Abishai nduguye wakamfuatia Sheba mwana wa Bikri.
11 Mmoja wa watu wa Yoabu akasimama kando ya Amasa, akasema, “Yeyote ampendaye Yoabu na yeyote aliye upande wa Daudi, na amfuate Yoabu!” 12 Amasa alikuwa akigaagaa katika damu yake katikati ya barabara; mtu mmoja akaona kwamba vikosi vyote vilikuwa vinasimama pale. Huyo mtu alipotambua kwamba kila aliyefika pale Amasa alipokuwa alisimama, alimburuta Amasa kutoka barabarani mpaka kwenye shamba na kutupia nguo juu yake. 13 Baada ya Amasa kuondolewa kutoka barabarani, watu wote walienda pamoja na Yoabu kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.
14 Sheba akapita katika makabila yote ya Israeli hadi Abel-Beth-Maaka na kupitia eneo lote la Waberi ambao walijikusanya pamoja na kumfuata. 15 Vikosi vyote vya Yoabu vikaja na kumhusuru Sheba mwana wa Bikri huko Abel-Beth-Maaka. Wakauzingira mji kwa kuweka vikosi vya askari, ili kukabiliana na ngome ya mji. Walipokuwa wanagongagonga ukuta ili kuubomoa na kuuangusha chini, 16 mwanamke mmoja mwenye busara akaita kutoka ndani ya mji, akisema, “Sikilizeni! Sikilizeni! Mwambieni Yoabu aje hapa ili niweze kuzungumza naye.” 17 Yoabu alikwenda mbele yake, akamuuliza, “Wewe ni Yoabu?”
Akamjibu, “Ndiye mimi.”
Yule mwanamke akamwambia, “Sikiliza kile mtumishi wako atakachokuambia.” Akamwambia, “Ninasikiliza.”
18 Huyo mwanamke akaendelea kusema, “Zamani za kale walikuwa wakisema, ‘Wakaulize ushauri huko Abeli,’ hivyo kulimaliza lile shauri. 19 Sisi ni watu wa amani na waaminifu katika Israeli. Wewe unajaribu kuharibu mji ambao ni mama katika Israeli. Kwa nini unataka kumeza urithi wa Bwana?”
20 Yoabu akajibu, “Hilo liwe mbali nami. Hilo liwe mbali nami kumeza au kuharibu. 21 Hivyo sivyo ilivyo. Mtu mmoja jina lake Sheba mwana wa Bikri, kutoka nchi ya vilima vya Efraimu, ameinua mkono wake dhidi ya mfalme, dhidi ya Daudi. Nikabidhini mtu huyu mmoja, nami nitajiondoa katika mji huu.”
Huyu mwanamke akamwambia Yoabu, “Kichwa chake mtatupiwa kupitia juu ya ukuta.”
22 Ndipo huyo mwanamke akaenda kwa watu wote akiwa na ushauri wake wa busara, nao wakakata kichwa cha Sheba mwana wa Bikri na kumtupia Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wake wakatawanyika kutoka mjini, kila mmoja akirejea nyumbani kwake. Naye Yoabu akarudi kwa mfalme huko Yerusalemu.
23 Yoabu alikuwa jemadari wa jeshi lote la Israeli; Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi; 24 Adoramu alikuwa kiongozi wa wale waliofanya kazi ya kulazimishwa; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mweka kumbukumbu; 25 Sheva alikuwa mwandishi; Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani; 26 na Ira, Myairi, alikuwa kuhani wa Daudi.
21:1 Wakati wa utawala wa Daudi kulikuwa na njaa kwa miaka mitatu mfululizo, kwa hiyo Daudi akautafuta uso wa Bwana. Bwana akasema, “Ni kwa sababu ya Sauli na nyumba yake iliyotiwa madoa ya damu, kwa sababu aliwaua Wagibeoni.”
2 Mfalme akawaita Wagibeoni na kuzumgumza nao. (Wagibeoni hawakuwa wa wana wa Israeli, ila walikuwa mabaki ya Waamori. Waisraeli walikuwa wameapa kuwaacha hai, lakini Sauli katika wivu wake kwa ajili ya Israeli na Yuda, alikuwa amejaribu kuwaangamiza.) 3 Daudi akawauliza Wagibeoni, “Niwatendee nini? Nitawaridhishaje ili mbariki urithi wa Bwana?”
4 Wagibeoni wakamjibu, “Hatuna haki ya kudai fedha wala dhahabu kutoka kwa Sauli au jamaa yake, wala hatuna haki ya kumuua mtu yeyote katika Israeli.”
Daudi akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”
5 Wakamjibu mfalme, “Kwa habari ya mtu aliyetuangamiza na kufanya hila mbaya dhidi yetu ili kwamba tuangamizwe na tusiwe na yeyote katika Israeli, 6 tupatieni wazao wake saba wa kiume tuwaue hadharani mbele za Bwana huko Gibea ya Sauli, aliyekuwa amechaguliwa na Bwana.”
Basi mfalme akasema, “Nitawakabidhi kwenu.”
7 Mfalme akamhifadhi Mefiboshethi mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, kwa sababu ya kile kiapo mbele za Bwana kati ya Daudi na Yonathani. 8 Lakini mfalme akamchukua Armoni na Mefiboshethi, wana wawili wa Rispa binti Aiya, ambao alikuwa amemzalia Sauli, pamoja na wana watano wa Merabu binti Sauli, aliokuwa amemzalia Adrieli mwana wa Barzilai, Mmeholathi. 9 Akawakabidhi kwa Wagibeoni, ambao waliwaua na kuwaweka wazi juu ya kilima mbele za Bwana. Wote saba walianguka kwa pamoja; waliuawa katika siku za kwanza za mavuno, mara tu uvunaji wa shayiri ulipokuwa unaanza.
10 Rispa binti Aiya akachukua nguo ya gunia, akajitandikia juu ya mwamba. Kuanzia mwanzo wa mavuno mpaka mvua ziliponyesha juu ya miili ya hao waliouawa, Rispa hakuruhusu ndege wa angani kuwagusa wakati wa mchana, wala wanyama wa mwitu wakati wa usiku. 11 Daudi alipoambiwa kile Rispa binti Aiya, suria wa Sauli, alichokuwa amekifanya, 12 alikwenda akachukua mifupa ya Sauli na mwanawe Yonathani kutoka kwa watu wa Yabeshi-Gileadi. (Walikuwa wameichukua kwa siri kutoka uwanja wa watu wote huko Beth-Shani, mahali ambapo Wafilisti walikuwa wamewatundika baada ya kumuua Sauli huko Gilboa.) 13 Daudi akaileta mifupa ya Sauli na ya mwanawe Yonathani kutoka huko, pia mifupa ya wale waliokuwa wameuawa na kutupwa ilikusanywa.
14 Wakazika mifupa ya Sauli na ya mwanawe Yonathani katika kaburi la Kishi, babaye Sauli, huko Sela katika nchi ya Benyamini, nao wakafanya kila kitu mfalme alichoagiza. Baada ya hayo, Mungu akajibu maombi kwa ajili ya nchi.