Ufalme wa Israeli

Shalmanesa Avamia Ufalme wa Hoshea

Utawala wa Hoshea, mfalme wa Israeli, uliendelea. Shalmanesa anavamia nchi za Hoshea.

karibu 725 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Wafalme 17:3–4

3 Mfalme Shalmanesa wa Ashuru akainuka dhidi ya Mfalme Hoshea, ambaye hapo mbeleni alikuwa mtumwa wake na kumlipa ushuru. 4 Lakini mfalme wa Ashuru akagundua kuwa Hoshea alikuwa msaliti, kwa kuwa alikuwa ametuma wajumbe kwa So mfalme wa Misri, naye hakuendelea kulipa ushuru kwa mfalme wa Ashuru tena kama alivyokuwa anafanya kila mwaka. Kwa hiyo Shalmanesa akamkamata na kumtia gerezani.

Hosea Atabiri Utumwa wa Makabila Kumi 725 KK

Hosea anatabiri utumwa wa makabila kumi, na kuwasihi watu watubu.

Hosea 7–8

1 kila mara nilipotaka kumponya Israeli,

dhambi za Efraimu zinafichuliwa

na maovu ya Samaria yanafunuliwa.

Wanafanya udanganyifu,

wevi huvunja nyumba,

maharamia hunyangʼanya barabarani,

2 lakini hawafahamu kwamba

ninakumbuka matendo yao yote mabaya.

Dhambi zao zimewameza,

ziko mbele zangu siku zote.

3 “Wanamfurahisha sana mfalme kwa maovu yao,

wakuu wao kwa uongo wao.

4 Wote ni wazinzi,

wanawaka kama tanuru

ambayo moto wake mwokaji hana haja ya kuuchochea

kuanzia kukanda unga

hadi umekwisha kuumuka.

5 Katika sikukuu ya mfalme wetu

wakuu wanawaka kwa mvinyo,

naye anawaunga mkono wenye mizaha.

6 Mioyo yao ni kama tanuru,

wanamwendea kwa hila.

Hasira yao inafoka moshi usiku kucha,

wakati wa asubuhi inalipuka

kama miali ya moto.

7 Wote ni moto kama tanuru;

wanawaangamiza watawala wao.

Wafalme wake wote wanaanguka,

wala hakuna yeyote kati yao aniitaye mimi.

8 “Efraimu anajichanganya na mataifa;

Efraimu ni mkate ambao haukuiva.

9 Wageni wananyonya nguvu zake,

lakini hafahamu hilo.

Nywele zake zina mvi hapa na pale,

lakini hana habari.

10 Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yake,

lakini pamoja na haya yote

harudi kwa Bwana Mungu wake

wala kumtafuta.

11 “Efraimu ni kama hua,

hudanganywa kwa urahisi na hana akili:

mara anaita Misri,

mara anageukia Ashuru.

12 Wakati watakapokwenda,

nitatupa wavu wangu juu yao;

nitawavuta chini waanguke

kama ndege wa angani.

Nitakaposikia wakikusanyika pamoja,

nitawanasa.

13 Ole wao, kwa sababu

wamepotoka kutoka kwangu!

Maangamizi ni yao

kwa sababu wameniasi!

Ninatamani kuwakomboa,

lakini wanasema uongo dhidi yangu.

14 Hawanililii mimi kutoka mioyoni mwao,

bali wanaomboleza vitandani mwao.

Hukusanyika pamoja kwa ajili ya nafaka na divai mpya,

lakini hugeukia mbali nami.

15 Niliwafundisha na kuwatia nguvu,

lakini wanapanga mabaya dhidi yangu.

16 Hawamgeukii Yeye Aliye Juu Sana,

wako kama upinde wenye kasoro.

Viongozi wao wataanguka kwa upanga

kwa sababu ya maneno yao ya jeuri.

Kwa ajili ya hili watadhihakiwa

katika nchi ya Misri.

8:1 “Wekeni tarumbeta midomoni mwenu!

Tai yuko juu ya nyumba ya Bwana

kwa sababu watu wamevunja Agano langu,

wameasi dhidi ya sheria yangu.

2 Israeli ananililia,

‘Ee Mungu wetu, tunakukubali!’

3 Lakini Israeli amekataa lile lililo jema,

adui atamfuatia.

4 Wanaweka wafalme bila idhini yangu,

wamechagua wakuu bila kibali changu.

Kwa fedha zao na dhahabu

wamejitengenezea sanamu kwa ajili

ya maangamizi yao wenyewe.

5 Ee Samaria, tupilieni mbali sanamu yenu ya ndama!

Hasira yangu inawaka dhidi yao.

Watakuwa najisi mpaka lini?

6 Zimetoka katika Israeli!

Ndama huyu: ametengenezwa na fundi, si Mungu.

Atavunjwa vipande vipande,

yule ndama wa Samaria.

7 “Wanapanda upepo

na kuvuna upepo wa kisulisuli.

Bua halina suke,

halitatoa unga.

Kama lingetoa nafaka,

wageni wangeila yote.

8 Israeli amemezwa;

sasa yupo miongoni mwa mataifa

kama kitu kisicho na thamani.

9 Kwa kuwa wamepanda kwenda Ashuru

kama punda-mwitu anayetangatanga peke yake.

Efraimu amejiuza mwenyewe

kwa wapenzi.

10 Ingawa wamejiuza wenyewe miongoni mwa mataifa,

sasa nitawakusanya pamoja.

Wataanza kudhoofika chini ya uonevu

wa mfalme mwenye nguvu.

11 “Ingawa Efraimu alijenga madhabahu nyingi

kwa ajili ya sadaka za dhambi,

hizi zimekuwa madhabahu

za kufanyia dhambi.

12 Nimeandika kwa ajili yao mambo mengi

kuhusu sheria yangu,

lakini wameziangalia

kama kitu cha kigeni.

13 Wanatoa dhabihu nilizopewa mimi

nao wanakula hiyo nyama,

lakini Bwana hapendezwi nao.

Sasa ataukumbuka uovu wao

na kuadhibu dhambi zao:

Watarudi Misri.

14 Israeli amemsahau Muumba wake

na kujenga majumba ya kifalme,

Yuda amejengea miji mingi ngome.

Lakini nitatuma moto kwenye miji yao

utakaoteketeza ngome zao.”