Zaburi za Dhiki, Hasa za Wakati wa Uhamisho (continued)
Zaburi zilizoandikwa wakati wa dhiki na mateso ya kanisa, hasa wakati wa uhamisho wa Babeli.
539 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Zaburi. Wimbo wa siku ya Sabato.
1 Ni vyema kumshukuru Bwana
na kuliimbia jina lako, Ee Uliye Juu Sana,
2 kuutangaza upendo wako asubuhi,
na uaminifu wako wakati wa usiku,
3 kwa zeze yenye nyuzi kumi
na kwa sauti ya kinubi.
4 Ee Bwana, kwa kuwa matendo yako yamenifurahisha,
nitaziimba kwa shangwe kazi za mikono yako.
5 Ee Bwana, tazama jinsi yalivyo makuu matendo yako,
tazama jinsi yalivyo ya kina mawazo yako!
6 Mjinga hafahamu,
mpumbavu haelewi,
7 ingawa waovu huchipua kama majani
na wote watendao mabaya wanastawi,
wataangamizwa milele.
8 Bali wewe, Ee Bwana,
utatukuzwa milele.
9 Ee Bwana, hakika adui zako,
hakika adui zako wataangamia.
Wote watendao mabaya watatawanyika.
10 Umeitukuza pembe yangu kama ile ya nyati dume,
mafuta mazuri yamemiminwa juu yangu.
11 Macho yangu yamewaona adui zangu wakishindwa,
masikio yangu yamesikia maangamizi ya adui zangu waovu.
12 Wenye haki watastawi kama mtende,
watakuwa kama mwerezi wa Lebanoni,
13 waliopandwa katika nyumba ya Bwana,
watastawi katika nyua za Mungu wetu.
14 Wakati wa uzee watakuwa bado wanazaa matunda,
watakuwa wabichi tena wamejaa nguvu,
15 wakitangaza, “Bwana ni mkamilifu;
yeye ni Mwamba wangu,
na ndani yake hamna uovu.”
93:1 Bwana anatawala, amejivika utukufu;
Bwana amejivika utukufu
tena amejivika nguvu.
Dunia imewekwa imara,
haitaondoshwa.
2 Kiti chako cha enzi kimekuwa thabiti tangu zamani;
wewe umekuwako tangu milele.
3 Bahari zimeinua, Ee Bwana,
bahari zimeinua sauti zake;
bahari zimeinua sauti za mawimbi yake.
4 Yeye ni mkuu kuliko ngurumo ya maji makuu,
ni mkuu kuliko mawimbi ya bahari:
Bwana aishiye juu sana ni mkuu.
5 Ee Bwana, sheria zako ni imara;
utakatifu umepamba nyumba yako
pasipo mwisho.
Wimbo wa kwenda juu.
1 Ninayainua macho yangu kwako,
kwako wewe ambaye kiti chako cha enzi kiko mbinguni.
2 Kama vile macho ya watumwa
yatazamavyo mkono wa bwana wao,
kama vile macho ya mtumishi wa kike
yatazamavyo mkono wa bibi yake,
ndivyo macho yetu yamtazamavyo Bwana Mungu wetu,
mpaka atakapotuhurumia.
3 Uturehemu, Ee Bwana, uturehemu,
kwa maana tumevumilia dharau nyingi.
4 Tumevumilia dhihaka nyingi kutoka kwa wenye kiburi,
dharau nyingi kutoka kwa wenye majivuno.