Zaburi za Dhiki, Hasa za Wakati wa Uhamisho (continued)

Zaburi zilizoandikwa wakati wa dhiki na mateso ya kanisa, hasa wakati wa uhamisho wa Babeli.

539 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Zaburi 26–27

Zaburi ya Daudi.

1 Ee Bwana, nithibitishe katika haki,

maana nimeishi maisha yasiyo na lawama;

nimemtumainia Bwana

bila kusitasita.

2 Ee Bwana, unijaribu, unipime,

uuchunguze moyo wangu

na mawazo yangu;

3 kwa maana upendo wako

uko mbele yangu daima,

nami natembea siku zote

katika kweli yako.

4 Siketi pamoja na watu wadanganyifu,

wala siandamani na wanafiki,

5 ninachukia kusanyiko la watenda mabaya

na ninakataa kuketi pamoja na waovu.

6 Ninanawa mikono yangu kwa kuwa sina hatia,

naikaribia madhabahu yako, Ee Bwana,

7 nikitangaza sifa yako kwa sauti kubwa,

huku nikisimulia matendo yako ya ajabu.

8 Ee Bwana, naipenda nyumba yako mahali unakoishi,

mahali ambapo utukufu wako hukaa.

9 Usiiondoe nafsi yangu pamoja na watenda dhambi,

wala uhai wangu pamoja na wamwagao damu,

10 ambao mikononi mwao kuna mipango miovu,

ambao mikono yao ya kuume imejaa rushwa.

11 Bali mimi ninaishi maisha yasiyo na lawama;

nikomboe na unihurumie.

12 Miguu yangu imesimama katika uwanja tambarare;

katika kusanyiko kuu nitamsifu Bwana.

Zaburi ya Daudi.

27:1 Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,

nimwogope nani?

Bwana ni ngome ya uzima wangu,

nimhofu nani?

2 Waovu watakaposogea dhidi yangu

ili wanile nyama yangu,

adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia,

watajikwaa na kuanguka.

3 Hata jeshi linizunguke pande zote,

moyo wangu hautaogopa;

hata vita vitokee dhidi yangu,

hata hapo nitakuwa na ujasiri.

4 Jambo moja ninamwomba Bwana,

hili ndilo ninalolitafuta:

niweze kukaa nyumbani mwa Bwana

siku zote za maisha yangu,

niutazame uzuri wa Bwana

na kumtafuta hekaluni mwake.

5 Kwa kuwa siku ya shida,

atanihifadhi salama katika maskani yake,

atanificha uvulini mwa hema yake

na kuniweka juu kwenye mwamba.

6 Kisha kichwa changu kitainuliwa

juu ya adui zangu wanaonizunguka.

Katika maskani yake nitatoa dhabihu kwa kelele za shangwe;

nitamwimbia Bwana na kumsifu.

7 Isikie sauti yangu nikuitapo, Ee Bwana,

unihurumie na unijibu.

8 Moyo wangu unasema kuhusu wewe,

“Utafute uso wake!”

Uso wako, Bwana “Nitautafuta.”

9 Usinifiche uso wako,

usimkatae mtumishi wako kwa hasira;

wewe umekuwa msaada wangu.

Usinikatae wala usiniache,

Ee Mungu Mwokozi wangu.

10 Hata kama baba yangu na mama wakiniacha,

Bwana atanipokea.

11 Nifundishe njia yako, Ee Bwana,

niongoze katika njia iliyonyooka

kwa sababu ya watesi wangu.

12 Usiniachilie kwa nia za adui zangu,

kwa maana mashahidi wa uongo

wameinuka dhidi yangu,

wakipumua ujeuri.

13 Nami bado nina tumaini hili:

nitauona wema wa Bwana

katika nchi ya walio hai.

14 Mngojee Bwana,

uwe hodari na mwenye moyo mkuu,

nawe, umngojee Bwana.

Zaburi 36

Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi mtumishi wa Bwana.

1 Kuna neno moyoni mwangu

kuhusu hali ya dhambi ya mwovu.

Hakuna hofu ya Mungu

mbele ya macho yake.

2 Kwa kuwa machoni pake mwenyewe hujisifu mno

hata hawezi kugundua au kuichukia dhambi yake.

3 Maneno ya kinywa chake ni maovu na ya udanganyifu,

ameacha kuwa mwenye hekima na kutenda mema.

4 Hata kitandani mwake hupanga hila mbaya,

hujitia katika njia ya dhambi

na hakatai lililo baya.

5 Upendo wako, Ee Bwana, unafika hadi mbinguni,

uaminifu wako hadi kwenye anga.

6 Haki yako ni kama milima mikubwa,

hukumu zako ni kama kilindi kikuu.

Ee Bwana, wewe huwahifadhi

mwanadamu na mnyama.

7 Upendo wako usiokoma

ni wa thamani mno!

Watu wakuu na wadogo

hujificha uvulini wa mbawa zako.

8 Wanajifurahisha katika wingi nyumbani mwako,

nawe utawanywesha katika mto wa furaha zako.

9 Kuwa pamoja nawe ni kijito cha uzima,

katika nuru yako twaona nuru.

10 Dumisha upendo wako kwa wale wanaokujua wewe,

haki yako kwa wale walio wanyofu wa moyo.

11 Mguu wa mwenye kiburi usije dhidi yangu,

wala mkono wa mwovu usinifukuze.

12 Angalia jinsi watenda mabaya walivyoanguka:

wametupwa chini, hawawezi kuinuka!