Zaburi za Daudi, Tarehe Hazijulikani

Zaburi zilizoandikwa na Daudi ambazo tarehe na mazingira ya kuandikwa kwazo hayajulikani.

1015 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Zaburi 40–41

Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

1 Nilimngoja Bwana kwa saburi,

naye akaniinamia, akasikia kilio changu.

2 Akanipandisha kutoka shimo la uharibifu,

kutoka matope na utelezi;

akaiweka miguu yangu juu ya mwamba

na kunipa mahali imara pa kusimama.

3 Akaweka wimbo mpya kinywani mwangu,

wimbo wa sifa kwa Mungu wetu.

Wengi wataona na kuogopa

na kuweka tumaini lao kwa Bwana.

4 Heri mtu yule amfanyaye Bwana kuwa tumaini lake,

asiyewategemea wenye kiburi,

wale wenye kugeukia miungu ya uongo.

5 Ee Bwana Mungu wangu,

umefanya mambo mengi ya ajabu.

Mambo uliyopanga kwa ajili yetu

hakuna awezaye kukuhesabia;

kama ningesema na kuyaelezea,

yangekuwa mengi mno kuyaelezea.

6 Dhabihu na sadaka hukuvitaka,

lakini umefungua masikio yangu;

sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi

hukuzihitaji.

7 Ndipo niliposema, “Mimi hapa, nimekuja:

imeandikwa kunihusu katika kitabu.

8 Ee Mungu wangu,

natamani kuyafanya mapenzi yako;

sheria yako iko ndani ya moyo wangu.”

9 Nimehubiri haki katika kusanyiko kubwa,

sikufunga mdomo wangu,

Ee Bwana, kama ujuavyo.

10 Sikuficha haki yako moyoni mwangu;

ninasema juu ya uaminifu wako na wokovu wako.

Sikuficha upendo wako na kweli yako

mbele ya kusanyiko kubwa.

11 Ee Bwana, usizuilie huruma zako,

upendo wako na kweli yako daima vinilinde.

12 Kwa maana taabu zisizo na hesabu zimenizunguka,

dhambi zangu zimenikamata, hata nisiweze kuona.

Zimekuwa nyingi kuliko nywele za kichwa changu,

nao moyo unazimia ndani yangu.

13 Ee Bwana, uwe radhi kuniokoa;

Ee Bwana, njoo hima unisaidie.

14 Wote wanaotafuta kuuondoa uhai wangu,

waaibishwe na kufadhaishwa;

wote wanaotamani kuangamizwa kwangu,

warudishwe nyuma kwa aibu.

15 Wale waniambiao, “Aha! Aha!”

wafadhaishwe na iwe aibu yao.

16 Lakini wote wakutafutao

washangilie na kukufurahia,

wale wapendao wokovu wako siku zote waseme,

“Bwana atukuzwe!”

17 Lakini bado mimi ni maskini na mhitaji;

Bwana na anifikirie.

Wewe ndiwe msaada wangu na Mwokozi wangu;

Ee Mungu wangu, usikawie.

Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

41:1 Heri mtu yule anayemjali mnyonge,

Bwana atamwokoa wakati wa shida.

2 Bwana atamlinda na kuyahifadhi maisha yake,

atambariki katika nchi

na hatamwacha katika tamaa ya adui zake.

3 Bwana atamtegemeza awapo mgonjwa kitandani,

atamwinua kutoka kitandani mwake.

4 Nilisema, “Ee Bwana nihurumie,

niponye, maana nimekutenda dhambi wewe.”

5 Adui zangu wanasema kwa hila,

“Lini atakufa, na jina lake litokomee kabisa.”

6 Kila anapokuja mtu kunitazama,

huzungumza uongo,

huku moyo wake hukusanya masingizio;

kisha huondoka na kuyasambaza huku na huko.

7 Adui zangu wote hunongʼonezana dhidi yangu,

hao huniwazia mabaya sana, wakisema,

8 “Ugonjwa mbaya sana umempata,

kamwe hatainuka tena kitandani mwake.”

9 Hata rafiki yangu wa karibu niliyemwamini,

yule aliyekula chakula changu

ameniinulia kisigino chake.

10 Lakini wewe, Ee Bwana, nihurumie,

ukaniinue tena, ili niweze kuwalipiza kisasi.

11 Najua kwamba wapendezwa nami,

kwa kuwa adui yangu hanishindi.

12 Katika uadilifu wangu unanitegemeza

na kuniweka kwenye uwepo wako milele.

13 Msifuni Bwana, Mungu wa Israeli,

tangu milele na hata milele.

Amen na Amen.

Zaburi 61

Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za uimbaji. Zaburi ya Daudi.

1 Ee Mungu, sikia kilio changu,

usikilize maombi yangu.

2 Kutoka miisho ya dunia ninakuita,

ninaita huku moyo wangu unadhoofika;

uniongoze kwenye mwamba

ule ulio juu kuliko mimi.

3 Kwa kuwa umekuwa kimbilio langu,

ngome imara dhidi ya adui.

4 Natamani kukaa hemani mwako milele,

na kukimbilia chini ya uvuli wa mbawa zako.

5 Ee Mungu, kwa kuwa umesikia nadhiri zangu,

umenipa urithi wa wale wanaoliogopa jina lako.

6 Mwongezee mfalme siku za maisha yake,

miaka yake kwa vizazi vingi.

7 Yeye na atawazwe kwenye kiti cha enzi mbele za Mungu milele;

amuru upendo wako na uaminifu wako vimlinde.

8 Ndipo daima nitaliimbia sifa jina lako

na kuzitimiza nadhiri zangu siku baada ya siku.