Zaburi za Wakati wa Utawala wa Daudi, Tarehe Hazina Uhakika (continued)
Zaburi zilizoandikwa na Daudi baada ya kuwa mfalme, ambazo tarehe na mazingira ya kuandikwa kwazo hayana uhakika.
1015 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Wimbo wa kwenda juu.
1 Katika dhiki yangu namwita Bwana,
naye hunijibu.
2 Ee Bwana, uniokoe kutoka midomo ya uongo
na ndimi za udanganyifu.
3 Atakufanyia nini,
au akufanyie nini zaidi, ewe ulimi mdanganyifu?
4 Atakuadhibu kwa mishale mikali ya shujaa,
kwa makaa yanayowaka ya mti wa mretemu.
5 Ole wangu kwa kuwa naishi Mesheki,
kwamba naishi katikati ya hema za Kedari!
6 Nimeishi muda mrefu mno
miongoni mwa wale wanaochukia amani.
7 Mimi ni mtu wa amani;
lakini ninaposema, wao wanataka vita.
Wimbo wa kwenda juu.
121:1 Nayainua macho yangu nitazame vilima,
msaada wangu utatoka wapi?
2 Msaada wangu hutoka kwa Bwana,
Muumba wa mbingu na dunia.
3 Hatauacha mguu wako uteleze,
yeye akulindaye hatasinzia,
4 hakika, yeye alindaye Israeli
hatasinzia wala hatalala usingizi.
5 Bwana anakulinda,
Bwana ni uvuli wako mkono wako wa kuume,
6 jua halitakudhuru mchana,
wala mwezi wakati wa usiku.
7 Bwana atakukinga na madhara yote,
atayalinda maisha yako,
8 Bwana atakulinda unapoingia na unapotoka,
tangu sasa na hata milele.
Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.
122:1 Nilishangilia pamoja na wale walioniambia,
“Twende nyumbani ya Bwana.”
2 Ee Yerusalemu, miguu yetu imesimama
malangoni mwako.
3 Yerusalemu imejengwa vyema kama mji
ambao umeshikamanishwa pamoja.
4 Huko ndiko makabila hukwea,
makabila ya Bwana,
kulisifu jina la Bwana kulingana na maagizo
waliopewa Israeli.
5 Huko viti vya enzi vya hukumu hukaa,
viti vya enzi vya nyumba ya Daudi.
6 Omba kwa ajili ya amani ya Yerusalemu:
“Wote wakupendao na wawe salama.
7 Amani na iwepo ndani ya kuta zako
na usalama ndani ya ngome zako.”
8 Kwa ajili ya ndugu zangu na marafiki,
nitasema, “Amani iwe ndani yako.”
9 Kwa ajili ya nyumba ya Bwana Mungu wetu,
nitatafuta mafanikio yako.
Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.
1 Kama Bwana asingalikuwa upande wetu;
Israeli na aseme sasa:
2 kama Bwana asingalikuwa upande wetu,
wakati watu walipotushambulia,
3 wakati hasira yao ilipowaka dhidi yetu,
wangalitumeza tungali hai,
4 mafuriko yangalitugharikisha,
maji mengi yangalitufunika,
5 maji yaendayo kasi
yangalituchukua.
6 Bwana asifiwe,
yeye ambaye hakuruhusu turaruliwe kwa meno yao.
7 Tumeponyoka kama ndege
kutoka mtego wa mwindaji;
mtego umevunjika,
nasi tukaokoka.
8 Msaada wetu ni katika jina la Bwana,
Muumba wa mbingu na dunia.
Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.
1 Moyo wangu hauna kiburi, Ee Bwana,
macho yangu hayajivuni;
sijishughulishi na mambo makuu kunizidi
wala mambo ya ajabu mno kwangu.
2 Lakini nimetuliza na kunyamazisha nafsi yangu;
kama mtoto aliyeachishwa kunyonya na mama yake,
kama mtoto aliyeachishwa kunyonya
ndivyo ilivyo nafsi iliyoko ndani yangu.
3 Ee Israeli, mtumaini Bwana
tangu sasa na hata milele.
Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.
1 Tazama jinsi ilivyo vyema na kupendeza
wakati ndugu wanapoishi pamoja katika umoja!
2 Ni kama mafuta ya thamani yaliyomiminwa kichwani,
yakitiririka kwenye ndevu,
yakitiririka kwenye ndevu za Aroni,
mpaka kwenye upindo wa mavazi yake.
3 Ni kama vile umande wa Hermoni
unavyoanguka juu ya Mlima Sayuni.
Kwa maana huko ndiko Bwana alikoamuru baraka yake,
naam, hata uzima milele.