Mithali Zaidi za Solomoni (continued)

984 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mithali 26–27

1 Kama theluji wakati wa kiangazi au mvua wakati wa mavuno,

ndivyo asivyostahili heshima mpumbavu.

2 Kama shomoro apigapigavyo mabawa yake

au mbayuwayu katika kuruka kwake kasi,

ndivyo ilivyo laana isiyo na sababu haimpati mtu.

3 Mjeledi kwa farasi, lijamu kwa punda,

nayo fimbo kwa migongo ya wapumbavu!

4 Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake,

ama wewe mwenyewe utakuwa kama yeye.

5 Mjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake,

ama atakuwa mwenye hekima machoni pake mwenyewe.

6 Kama vile ilivyo kujikata miguu au kunywa hasara,

ndivyo ilivyo kutuma ujumbe kwa mkono wa mpumbavu.

7 Kama miguu ya kiwete inavyoningʼinia

ndivyo ilivyo mithali katika kinywa cha mpumbavu.

8 Kama kufunga jiwe kwenye kombeo,

ndivyo ilivyo kumpa mpumbavu heshima.

9 Kama mwiba kwenye mkono wa mlevi

ndivyo ilivyo mithali kinywani mwa mpumbavu.

10 Kama mpiga upinde ambaye hujeruhi ovyo,

ndivyo alivyo yeye aajiriye mpumbavu au yeyote apitaye njiani.

11 Kama mbwa ayarudiavyo matapiko yake,

ndivyo mpumbavu arudiavyo upumbavu wake.

12 Je, unamwona mtu ajionaye mwenye hekima

machoni pake mwenyewe?

Liko tumaini zaidi kwa mpumbavu kuliko kwake.

13 Mvivu husema, “Yuko simba barabarani,

simba mkali anazunguka mitaa!”

14 Kama vile mlango ugeukavyo kwenye bawaba zake,

ndivyo mvivu ajigeuzavyo kitandani mwake.

15 Mtu mvivu hutumbukiza mkono wake kwenye sahani,

naye huchoka kuupeleka kwenye kinywa chake.

16 Mtu mvivu ni mwenye hekima machoni pake mwenyewe,

kuliko watu saba wawezao kujibu kwa busara.

17 Kama yeye amkamataye mbwa kwa masikio,

ndivyo alivyo mtu apitaye njiani na kujiingiza kwenye ugomvi usiomhusu.

18 Kama mtu mwendawazimu

atupaye vijinga vya moto au mishale ya kufisha,

19 ndivyo alivyo mtu amdanganyaye jirani yake na kusema,

“Nilikuwa nikifanya mzaha tu!”

20 Bila kuni moto huzimika;

pasipo uchongezi ugomvi humalizika.

21 Kama makaa juu ya makaa yanayowaka, na kama kuni kwenye moto,

ndivyo alivyo mtu mgomvi kwa kuchochea ugomvi.

22 Maneno ya mchongezi ni kama chakula kitamu;

huingia sehemu za ndani sana za mtu.

23 Kama rangi ingʼaayo iliyopakwa kwenye vyombo vya udongo

ndivyo ilivyo midomo laini pamoja na moyo mbaya.

24 Mtu mwenye nia ya kudhuru wengine hujificha kwa maneno ya midomo yake,

lakini moyoni mwake huficha udanganyifu.

25 Ingawa maneno yake huvutia, usimwamini,

kwa maana machukizo saba hujaza moyo wake.

26 Nia yake ya kudhuru wengine inaweza kufichwa na udanganyifu,

lakini uovu wake utafichuliwa kwenye kusanyiko.

27 Kama mtu akichimba shimo, atatumbukia ndani yake,

kama mtu akivingirisha jiwe, litamrudia.

28 Ulimi wa uongo, huwachukia wale unaowaumiza,

nacho kinywa cha kujipendekeza hutenda uharibifu.

27:1 Usijisifu kwa ajili ya kesho,

kwa kuwa hujui ni nini kitakachozaliwa kwa siku moja.

2 Mwache mwingine akusifu,

wala si kinywa chako mwenyewe;

mtu mwingine afanye hivyo

na si midomo yako mwenyewe.

3 Jiwe ni zito na mchanga ni mzigo,

lakini kukasirishwa na mpumbavu ni kuzito kuliko vyote viwili.

4 Hasira ni ukatili na ghadhabu kali ni gharika,

lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu?

5 Afadhali karipio la wazi

kuliko upendo uliofichika.

6 Majeraha kutoka kwa rafiki yaonyesha uaminifu,

bali kubusu kwa adui ni kwingi sana.

7 Yeye aliyeshiba huchukia kabisa asali,

bali kwa mwenye njaa

hata kile kilicho kichungu

kwake ni kitamu.

8 Kama ndege atangatangavyo mbali na kiota chake,

ndivyo alivyo mtu atangatangaye

mbali na nyumbani mwake.

9 Manukato na uvumba huleta furaha moyoni,

nao uzuri wa rafiki huchipuka

kutoka kwenye ushauri wake wa uaminifu.

10 Usimwache rafiki yako wala rafiki wa baba yako,

tena usiende nyumbani mwa ndugu yako

wakati umepatwa na maafa.

Bora jirani wa karibu

kuliko ndugu aliye mbali.

11 Mwanangu, uwe na hekima,

nawe ulete furaha moyoni mwangu,

ndipo nitakapoweza kumjibu yeyote

anitendaye kwa dharau.

12 Mtu mwenye busara huona hatari na kujificha,

bali mjinga huendelea mbele nayo ikamtesa.

13 Chukua vazi la yule awekaye dhamana

kwa ajili ya mgeni;

lishikilie iwe dhamana kama anafanya hivyo

kwa ajili ya mwanamke mpotovu.

14 Kama mtu akimbariki jirani yake kwa sauti kuu

asubuhi na mapema,

itahesabiwa kama ni laana.

15 Mke mgomvi ni kama

matone yasiyokoma ya siku ya mvua.

16 Kumzuia yeye ni kama kuuzuia upepo

au kukamata mafuta kwa kiganja cha mkono.

17 Kama vile chuma kinoavyo chuma,

ndivyo mtu amnoavyo mwenzake.

18 Yeye autunzaye mtini atakula tunda lake,

naye amtunzaye bwana wake ataheshimiwa.

19 Kama uso uonekanavyo kwenye maji,

ndivyo hivyo moyo wa mtu humwonyesha alivyo.

20 Kuzimu na Uharibifu havishibi

kadhalika macho ya mwanadamu.

21 Kalibu ni kwa ajili ya fedha

na tanuru kwa ajili ya dhahabu,

bali mtu hupimwa kwa sifa azipokeazo.

22 Hata ukimtwanga mpumbavu kwenye kinu,

ukimtwanga kama nafaka kwa mchi,

hutauondoa upumbavu wake.

23 Hakikisha kuwa unajua hali ya makundi yako

ya kondoo na mbuzi,

angalia kwa bidii ngʼombe zako.

24 Kwa kuwa utajiri haudumu milele,

nayo taji haidumu vizazi vyote.

25 Wakati majani makavu yameondolewa

na mapya yamechipua,

nayo majani toka milimani yamekusanywa,

26 wana-kondoo watakupatia mavazi

na mbuzi thamani ya shamba.

27 Utakuwa na maziwa mengi ya mbuzi

kukulisha wewe na jamaa yako,

na kuwalisha watumishi wako wa kike.