Unabii kwa Wazee wa Wayahudi (continued)

593 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ezekieli 21–22

1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, uelekeze uso wako juu ya Yerusalemu na uhubiri dhidi ya mahali patakatifu. Tabiri dhidi ya nchi ya Israeli 3 uiambie: ‘Hili ndilo Bwana asemalo: Mimi niko kinyume nawe. Nitautoa upanga wangu kwenye ala yake na kumkatilia mbali mwenye haki na mwovu. 4 Kwa sababu nitamkatilia mbali mwenye haki na mwovu, upanga wangu utakuwa wazi dhidi ya kila mmoja kuanzia kusini mpaka kaskazini. 5 Ndipo watu wote watajua ya kuwa Mimi Bwana nimeutoa upanga wangu kwenye ala yake, nao hautarudi humo tena.’

6 “Kwa hiyo lia kwa uchungu, mwanadamu! Lia kwa uchungu mbele yao kwa moyo uliopondeka na kwa huzuni nyingi. 7 Nao watakapokuuliza, ‘Kwa nini unalia kwa uchungu?’ Utasema hivi, ‘Kwa sababu ya habari zinazokuja. Kila moyo utayeyuka na kila mkono utalegea, kila roho itazimia na kila goti litalegea kama maji.’ Habari hizo zinakuja! Hakika zitatokea, asema Bwana Mwenyezi.”

8 Neno la Bwana likanijia, kusema: 9 “Mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo Bwana asemalo:

“ ‘Upanga, upanga,

ulionolewa na kusuguliwa:

10 umenolewa kwa ajili ya mauaji,

umesuguliwa ili ungʼae

kama umeme wa radi!

“ ‘Je, tuifurahie fimbo ya utawala ya mwanangu Yuda? Upanga unaidharau kila fimbo ya namna hiyo.

11 “ ‘Upanga umewekwa tayari ili kusuguliwa,

ili upate kushikwa mkononi,

umenolewa na kusuguliwa,

umewekwa tayari kwa mkono wa muuaji.

12 Piga kelele na uomboleze, ee mwanadamu,

kwa kuwa upanga u dhidi ya watu wangu;

u dhidi ya wakuu wote wa Israeli.

Wametolewa wauawe kwa upanga

pamoja na watu wangu.

Kwa hiyo pigapiga kifua chako.

13 “ ‘Kwa maana upanga huu umejaribiwa na kuhakikishwa, itakuwaje basi fimbo ya ufalme ya Yuda inayoudharau kama haitakuwepo tena, bali itakuwa imeondolewa kabisa? asema Bwana Mwenyezi.’

14 “Hivyo basi, mwanadamu, tabiri

na ukapige makofi.

Upanga wako na upige mara mbili,

naam, hata mara tatu.

Ni upanga wa kuchinja,

upanga wa mauaji makuu,

ukiwashambulia kutoka kila upande.

15 Ili mioyo ipate kuyeyuka

na wanaouawa wawe wengi,

nimeweka upanga wa kuchinja

kwenye malango yao yote.

Lo! Umetengenezwa

umetemete kama umeme wa radi,

umeshikwa kwa ajili ya kuua.

16 Ee upanga, kata upande wa kuume,

kisha upande wa kushoto,

mahali popote makali yako

yatakapoelekezwa.

17 Mimi nami nitapiga makofi,

nayo ghadhabu yangu itapungua.

Mimi Bwana nimesema.”

18 Neno la Bwana likanijia kusema: 19 “Mwanadamu, weka alama njia mbili ambazo upanga wa mfalme wa Babeli utapitia, njia hizo zikianzia katika nchi hiyo hiyo. Weka kibao pale ambapo njia zinagawanyika kuelekea mjini. 20 Weka alama njia moja kwa ajili ya upanga upate kuja dhidi ya Raba ya Waamoni na nyingine upate kuja dhidi ya Yuda na Yerusalemu iliyozungushiwa ngome. 21 Kwa kuwa mfalme wa Babeli sasa amesimama katika njia panda, katika makutano ya njia mbili, akipiga ramli: anapiga kura kwa kutumia mishale, anataka shauri kwa sanamu zake, anachunguza maini ya wanyama. 22 Upande wake wa kuume inakuja kura ya Yerusalemu, ambapo ataweka vyombo vya kuvunjia boma, ili kuamrisha mauaji, kupiga ukelele wa vita, kuweka vyombo vya kuvunjia boma kwenye malango, kuweka jeshi kuzunguka na kufanya uzingiraji. 23 Itakuwa kama kupiga ramli kwa uongo kwa wale watu ambao wameapa kumtii yeye. Lakini mfalme wa Babeli atawakumbusha juu ya uovu wao na kuwachukua mateka.

24 “Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu enyi watu mmekumbusha uovu wenu kwa kuasi waziwazi, mkidhihirisha dhambi zenu katika yale yote mfanyayo, kwa kuwa mmefanya jambo hili, mtachukuliwa mateka.

25 “ ‘Ee mtawala kafiri na mwovu wa Israeli, ambaye siku yako imewadia, ambaye wakati wako wa adhabu umefikia kilele chake, 26 hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Vua kilemba, ondoa taji. Kwa kuwa mambo hayatakuwa kama yalivyokuwa. Aliye mnyonge atakwezwa na aliyekwezwa atashushwa. 27 Mahame! Mahame! Nitaufanya mji kuwa mahame! Hautajengwa upya mpaka aje yule ambaye ndiye mwenye haki nao; yeye ndiye nitakayempa.’

28 “Nawe, mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo kuhusu Waamoni na matukano yao.

“ ‘Upanga, upanga,

umefutwa kwa ajili ya kuua,

umesuguliwa ili kuangamiza

na unametameta kama umeme wa radi!

29 Wakati wakitoa maono ya uongo kwa ajili yako,

wanapobashiri uongo kwa ajili yako,

wanakuweka wewe kwenye shingo za watu wapotovu,

wale walio waovu,

wale ambao siku yao imewadia,

wakati wa adhabu yao ya mwisho.

30 Urudishe upanga kwenye ala yake!

Katika mahali ulipoumbiwa,

katika nchi ya baba zako,

huko nitakuhukumu.

31 Nitamwaga ghadhabu yangu juu yako

na kupuliza moto wa hasira yangu dhidi yako;

nitakutia mikononi mwa watu wakatili,

watu stadi katika kuangamiza.

32 Mtakuwa kuni za kuwashia moto,

damu yenu itamwagwa katika nchi yenu,

wala hamtakumbukwa tena;

kwa maana Mimi Bwana nimesema.’ ”

22:1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, je, wewe utauhukumu? Je, utauhukumu huu mji umwagao damu? Basi uujulishe juu ya matendo yake yote ya machukizo 3 uuambie: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ee mji ule ujileteao maangamizi wenyewe kwa kumwaga damu ndani yake na kujinajisi wenyewe kwa kutengeneza sanamu, 4 umekuwa na hatia kwa sababu ya damu uliyomwaga na umetiwa unajisi kwa sanamu ulizotengeneza. Umejiletea mwisho wa siku zako na mwisho wa miaka yako umewadia. Kwa hiyo nitakufanya kitu cha kudharauliwa kwa mataifa na kitu cha mzaha kwa nchi zote. 5 Wale walio karibu na wale walio mbali watakudhihaki, Ewe mji wenye sifa mbaya, uliyejaa ghasia.

6 “ ‘Ona jinsi kila mkuu wa Israeli aliyeko ndani yako anavyotumia nguvu zake kumwaga damu. 7 Ndani yako wamewadharau baba na mama, ndani yako wamewatendea wageni udhalimu na kuwaonea yatima na wajane. 8 Mmedharau vitu vyangu vitakatifu na kuzinajisi Sabato zangu. 9 Ndani yako wako watu wasingiziaji, watu walio tayari kumwaga damu, ndani yako wako wale wanaokula vyakula vilivyotolewa mahali pa ibada za miungu kwenye milima, na kutenda matendo ya uasherati. 10 Ndani yako wako wale wanaovunjia heshima vitanda vya baba zao, ndani yako wamo wale wanaowatendea wanawake jeuri wakiwa katika hedhi, wakati wakiwa si safi. 11 Ndani yako mtu hufanya mambo ya machukizo na mke wa jirani yake, mwingine kwa aibu kubwa hukutana kimwili na mke wa mwanawe, mwingine humtenda jeuri dada yake, binti wa baba yake hasa. 12 Ndani yako watu hupokea rushwa ili kumwaga damu, mnapokea riba na faida ya ziada na kupata faida isiyokuwa halali kutoka kwa jirani ili kupata faida kubwa kupita kiasi. Nawe umenisahau mimi, asema Bwana Mwenyezi.

13 “ ‘Hakika nitapiga makofi kwa ajili ya faida isiyo halali uliyojipatia na kwa damu uliyoimwaga ndani yako. 14 Je, ujasiri wako utadumu au mikono yako itakuwa na nguvu siku hiyo nitakapokushughulikia? Mimi Bwana nimesema na nitalifanya. 15 Nitakutawanya miongoni mwa mataifa na kukutapanya katika nchi mbalimbali nami nitakomesha unajisi wako. 16 Ukiisha kunajisika mbele ya mataifa, utajua kuwa Mimi ndimi Bwana.’ ”

17 Ndipo neno la Bwana likanijia kusema: 18 “Mwanadamu, nyumba ya Israeli imekuwa kwangu takataka ya chuma, wote kwangu wamekuwa shaba, bati, chuma na risasi iliyoachwa kalibuni. Wao ni taka ya madini ya fedha tu. 19 Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: ‘Kwa kuwa wote mmekuwa takataka ya chuma, nitawakusanya Yerusalemu. 20 Kama vile watu wakusanyavyo fedha, shaba, chuma, risasi na bati kalibuni ili kuyeyusha kwa moto mkali, ndivyo nitakavyowakusanya katika hasira yangu na ghadhabu yangu kuwaweka ndani ya mji na kuwayeyusha. 21 Nitawakusanya na kupuliza juu yenu moto wa hasira yangu na ghadhabu yangu nanyi mtayeyushwa ndani ya huo mji. 22 Kama fedha iyeyukavyo kalibuni, ndivyo mtakavyoyeyuka ndani ya huo mji, nanyi mtajua kuwa Mimi Bwana nimemwaga ghadhabu yangu juu yenu.’ ”

23 Neno la Bwana likanijia tena kusema: 24 “Mwanadamu, iambie nchi, ‘Wewe ni nchi ambayo haijapata mvua wala manyunyu katika siku ya ghadhabu.’ 25 Kuna hila mbaya ya wakuu ndani yake kama simba angurumaye akirarua mawindo yake, wanakula watu, wanachukua hazina na vitu vya thamani na kuongeza idadi ya wajane ndani yake. 26 Makuhani wake wameihalifu sheria yangu na kunajisi vitu vyangu vitakatifu, hawatofautishi kati ya vitu vitakatifu na vitu vya kawaida. Wanafundisha kuwa hakuna tofauti kati ya vitu vilivyo najisi na visivyo najisi, nao wanafumba macho yao katika kutunza Sabato zangu, hivyo katikati yao nimetiwa unajisi. 27 Maafisa wake walioko ndani yake ni kama mbwa mwitu wararuao mawindo yao, wanamwaga damu na kuua watu ili kupata faida ya udhalimu. 28 Manabii wake wanapaka chokaa matendo haya kwa maono ya uongo na utabiri wa udanganyifu. Wanasema, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo,’ wakati Bwana hajasema. 29 Watu wa nchi wanatoza kwa nguvu na kufanya unyangʼanyi, wanawatenda jeuri maskini na wahitaji na kuwaonea wageni, wakiwanyima haki.

30 “Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, ambaye angejenga ukuta na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka kwa ajili ya watu wa nchi ili nisije nikaiangamiza, lakini sikumwona mtu yeyote. 31 Hivyo nitaimwaga ghadhabu yangu juu yao na kuwateketeza kwa moto wa hasira yangu, nikiyaleta juu ya vichwa vyao yale yote waliyotenda, asema Bwana Mwenyezi.”