Unabii Dhidi ya Sedekia na Manabii wa Uongo (continued)
Unabii mbalimbali dhidi ya Sedekia, manabii wa uongo, Yerusalemu, na mataifa ya jamii ya Myahudi.
594 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Je, ninyi watu mna maana gani kutumia mithali hii inayohusu nchi ya Israeli:
“ ‘Baba wamekula zabibu zenye chachu,
nayo meno ya watoto yametiwa ganzi’?
3 “Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, hamtatumia tena mithali hii katika Israeli. 4 Kwa kuwa kila roho ni mali yangu, kama vile ilivyo roho ya baba, vivyo hivyo roho ya mtoto ni mali yangu. Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa.
5 “Mtu aweza kuwa ni mwenye haki
atendaye yaliyo haki na sawa.
6 Hakula katika mahali pa ibada za miungu
kwenye milima
wala hakuziinulia macho sanamu
za nyumba ya Israeli.
Hakumtia unajisi mke wa jirani yake,
wala hakukutana kimwili na mwanamke
wakati wa siku zake za hedhi.
7 Hamwonei mtu yeyote,
bali hurudisha kilichowekwa rehani kwake.
Hanyangʼanyi, bali huwapa wenye njaa chakula chake
na huwapa nguo walio uchi.
8 Hakopeshi kwa riba
wala hajipatii faida ya ziada.
Huuzuia mkono wake usifanye mabaya,
naye huhukumu kwa haki kati ya mtu na mtu.
9 Huzifuata amri zangu
na kuzishika sheria zangu kwa uaminifu.
Huyo mtu ni mwenye haki;
hakika ataishi,
asema Bwana Mwenyezi.
10 “Aweza kuwa ana mwana jeuri, amwagaye damu au atendaye mojawapo ya mambo haya 11 (ingawa baba yake hakufanya mojawapo ya haya):
“Hula katika mahali pa ibada za miungu kwenye milima.
Humtia unajisi mke wa jirani yake.
12 Huwaonea maskini na wahitaji.
Hunyangʼanyana.
Harudishi kile kilichowekwa rehani kwake.
Huziinulia sanamu macho.
Hufanya mambo ya machukizo.
13 Hukopesha kwa riba na kutafuta faida ya ziada.
Je, mtu wa namna hii ataishi? Hapana, hataishi! Kwa sababu amefanya mambo haya yote ya machukizo, hakika atauawa na damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe.
14 “Lakini yawezekana mwana huyo ana mwana aonaye dhambi hizi zote anazofanya baba yake, naye ingawa anaziona, yeye hafanyi mabaya kama haya:
15 “Hakula katika mahali pa ibada za miungu
kwenye milima,
wala hainulii macho sanamu
za nyumba ya Israeli.
Hakumtia unajisi
mke wa jirani yake.
16 Hakumwonea mtu yeyote
wala hakutaka rehani kwa ajili ya mkopo.
Hanyangʼanyi,
bali huwapa wenye njaa chakula chake
na huwapa nguo walio uchi.
17 Huuzuia mkono wake usitende dhambi,
hakopeshi kwa riba
wala hajipatii faida ya ziada.
Huzishika amri zangu
na kuzifuata sheria zangu.
Hatakufa kwa ajili ya dhambi za baba yake; hakika ataishi. 18 Lakini baba yake atakufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe, kwa sababu alitoza bei isiyo halali kwa nguvu, akamnyangʼanya ndugu yake na kufanya yaliyo mabaya miongoni mwa watu wake.
19 “Lakini mnauliza, ‘Kwa nini mwana asiadhibiwe kwa uovu wa baba yake?’ Kwa vile mwana ametenda yaliyo haki na sawa na amekuwa mwangalifu kuzishika amri zangu zote, hakika ataishi. 20 Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa. Mwana hataadhibiwa kwa ajili ya makosa ya baba yake, wala baba hataadhibiwa kwa ajili ya makosa ya mwanawe. Haki ya mtu mwenye haki itahesabiwa juu yake na uovu wa mtu mwovu utalipizwa juu yake.
21 “Lakini mtu mwovu akiacha dhambi zake zote alizozitenda na kushika amri zangu zote na kufanya lililo haki na sawa, hakika ataishi, hatakufa. 22 Hakuna kosa lolote alilotenda litakalokumbukwa juu yake. Kwa ajili ya mambo ya haki aliyoyatenda, ataishi. 23 Je, mimi ninafurahia kifo cha mtu mwovu? Asema Bwana Mwenyezi. Je, si mimi ninafurahi wanapogeuka kutoka njia zao mbaya na kuishi?
24 “Lakini kama mtu mwenye haki akiacha haki yake na kutenda dhambi na kufanya mambo ya machukizo ambayo mtu mwovu hufanya, Je, ataishi? Hakuna hata mojawapo ya matendo ya haki aliyotenda litakalokumbukwa. Kwa sababu ya kukosa uaminifu kwake anayo hatia na kwa sababu ya dhambi alizozitenda, atakufa.
25 “Lakini mnasema, ‘Njia ya Bwana si ya haki.’ Sikia, ee nyumba ya Israeli: Njia yangu siyo iliyo ya haki? Je, si njia zenu ndizo ambazo si za haki? 26 Kama mtu mwenye haki akiacha haki yake na kutenda dhambi, atakufa kwa ajili ya dhambi yake, kwa sababu ya dhambi alizotenda, atakufa. 27 Lakini mtu mwovu akigeuka kutoka maovu aliyoyatenda na kufanya yaliyo haki na sawa, ataokoa maisha yake. 28 Kwa kuwa anayafikiria na kugeuka kutoka makosa yake yote aliyoyatenda na kuyaacha, hakika ataishi, hatakufa. 29 Lakini nyumba ya Israeli inasema, ‘Njia za Bwana si haki.’ Je, njia zangu si za haki, ee nyumba ya Israeli? Je, si njia zenu ndizo ambazo si za haki?”
30 “Kwa hiyo, ee nyumba ya Israeli, nitawahukumu, kila mmoja sawasawa na njia zake, asema Bwana Mwenyezi. Tubuni! Geukeni kutoka makosa yenu yote, ndipo dhambi haitakuwa anguko lenu. 31 Tupilieni mbali makosa yenu yote mliyoyatenda, nanyi mpate moyo mpya na roho mpya. Kwa nini mfe, ee nyumba ya Israeli? 32 Kwa maana sifurahii kifo cha mtu awaye yote afaye katika uovu, asema Bwana Mwenyezi. Tubuni basi, mkaishi!
19:1 “Wewe fanya maombolezo kuhusu wakuu wa Israeli 2 na useme:
“ ‘Tazama jinsi gani mama yako alivyokuwa simba jike
miongoni mwa simba!
Alilala katikati ya wana simba
na kulisha watoto wake.
3 Alimlea mmoja wa watoto wake,
naye akawa simba mwenye nguvu.
Akajifunza kurarua mawindo
naye akala watu.
4 Mataifa wakasikia habari zake,
naye akanaswa katika shimo lao.
Wakamwongoza kwa ndoana
mpaka nchi ya Misri.
5 “ ‘Mama yake alipongoja na kuona tumaini lake halitimiziki,
nayo matarajio yake yametoweka,
akamchukua mwanawe mwingine
na kumfanya simba mwenye nguvu.
6 Alizungukazunguka miongoni mwa simba,
kwa kuwa sasa alikuwa simba mwenye nguvu.
Akajifunza kurarua mawindo
naye akala watu.
7 Akabomoa ngome zao
na kuiharibu miji yao.
Nchi na wote waliokuwa ndani yake
wakatiwa hofu kwa kunguruma kwake.
8 Kisha mataifa wakaja dhidi yake
kutoka sehemu zilizomzunguka.
Wakatanda nyavu zao kwa ajili yake,
naye akanaswa katika shimo lao.
9 Kwa kutumia ndoana wakamvutia kwenye tundu
na kumleta mpaka kwa mfalme wa Babeli.
Wakamtia gerezani, hivyo kunguruma kwake
hakukusikika tena
katika milima ya Israeli.
10 “ ‘Mama yako alikuwa kama mzabibu
katika shamba lako la mizabibu
uliopandwa kando ya maji,
ukiwa unazaa sana na wenye matawi mengi
kwa sababu ya wingi wa maji.
11 Matawi yake yalikuwa na nguvu,
yaliyofaa kuwa fimbo ya enzi ya mtawala.
Ulikuwa mrefu kupita miti mingine
katikati ya matawi manene;
ulionekana kwa urahisi
kwa ajili ya urefu wake
na wingi wa matawi yake.
12 Lakini ulingʼolewa kwa hasira kali
na kutupwa chini.
Upepo wa mashariki uliufanya usinyae,
matunda yake yakapukutika,
matawi yake yenye nguvu yakanyauka
na moto ukayateketeza.
13 Sasa umepandwa jangwani
katika nchi kame na ya kiu.
14 Moto ulienea kuanzia katika mmojawapo ya matawi yake makubwa
na kuteketeza matunda yake.
Hakuna tawi lenye nguvu lililobaki juu yake
lifaalo kuwa fimbo ya enzi ya mtawala.’
Hili ndilo ombolezo, na litumike kama ombolezo.”