Unabii Dhidi ya Sedekia na Manabii wa Uongo (continued)

Unabii mbalimbali dhidi ya Sedekia, manabii wa uongo, Yerusalemu, na mataifa ya jamii ya Myahudi.

594 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ezekieli 13–15

1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, tabiri dhidi ya manabii wa Israeli wanaotabiri sasa. Waambie hao ambao hutabiri kutokana na mawazo yao wenyewe: ‘Sikia neno la Bwana! 3 Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ole wao manabii wapumbavu wafuatao roho yao wenyewe na wala hawajaona chochote! 4 Manabii wako, ee Israeli, ni kama mbweha katikati ya magofu. 5 Hamjakwea kwenda kuziba mahali palipobomoka katika ukuta ili kuukarabati kwa ajili ya nyumba ya Israeli, ili kwamba isimame imara kwenye vita katika siku ya Bwana. 6 Maono yao ni ya uongo na ubashiri wao ni wa udanganyifu. Wao husema, “Bwana amesema,” wakati Bwana hakuwatuma, bado wakitarajia maneno yao kutimizwa. 7 Je, hamjaona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu hapo msemapo, “Bwana asema,” lakini Mimi sijasema?

8 “ ‘Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ya uongo wa maneno yenu na kwa madanganyo ya maono yenu, Mimi ni kinyume na ninyi, asema Bwana Mwenyezi. 9 Mkono wangu utakuwa dhidi ya manabii ambao huona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu. Hawatakuwa katika baraza la watu wangu au kuandikwa katika kumbukumbu ya nyumba ya Israeli wala hawataingia katika nchi ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mwenyezi.

10 “ ‘Kwa sababu ni kweli wanapotosha watu wangu, wakisema, “Amani,” wakati ambapo hakuna amani, pia kwa sababu, wakati ukuta dhaifu unapojengwa, wanaufunika kwa kupaka chokaa, 11 kwa hiyo waambie hao wanaoupaka chokaa isiyokorogwa vyema kwamba ukuta huo utaanguka. Mvua kubwa ya mafuriko itanyesha, nami nitaleta mvua ya mawe inyeshe kwa nguvu, nao upepo wa dhoruba utavuma juu yake. 12 Wakati ukuta utakapoanguka, je, watu hawatawauliza, “Iko wapi chokaa mliyopaka ukuta?”

13 “ ‘Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Katika ghadhabu yangu nitauachia upepo wa dhoruba, pia katika hasira yangu mvua ya mawe na mvua ya mafuriko itanyesha ikiwa na ghadhabu ya kuangamiza. 14 Nitaubomoa ukuta mlioupaka chokaa na kuuangusha chini ili msingi wake uachwe wazi. Utakapoanguka, mtaangamizwa ndani yake, nanyi mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana. 15 Hivyo ndivyo nitakavyoitimiza ghadhabu yangu dhidi ya huo ukuta na dhidi yao walioupaka chokaa. Nitawaambia ninyi, “Ukuta umebomoka na vivyo hivyo wale walioupaka chokaa, 16 wale manabii wa Israeli waliotabiri juu ya Yerusalemu na kuona maono ya amani kwa ajili yake wakati kulipokuwa hakuna amani, asema Bwana Mwenyezi.” ’

17 “Sasa, mwanadamu, kaza uso wako dhidi ya binti za watu wako wanaotabiri mambo kutoka mawazo yao wenyewe. Tabiri dhidi yao 18 na useme, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ole wao wanawake washonao hirizi za uchawi juu ya viwiko vyao vyote na kutengeneza shela za urefu wa aina mbalimbali kwa ajili ya kufunika vichwa vyao kwa makusudi ya kuwanasa watu. Je, mtatega uhai wa watu wangu lakini ninyi mponye wa kwenu? 19 Ninyi mmeninajisi miongoni mwa watu wangu kwa ajili ya konzi chache za shayiri na chembe za mkate. Kwa kuwaambia uongo watu wangu, wale ambao husikiliza uongo, mmewaua wale watu ambao wasingekufa na kuwaacha hai wale ambao wasingeishi.

20 “ ‘Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mimi niko kinyume na hizo hirizi zenu za uchawi ambazo kwa hizo mnawatega watu kama ndege, nami nitazirarua kutoka mikononi mwenu, nitawaweka huru watu wale mliowatega kama ndege. 21 Nitazirarua shela zenu na kuwaokoa watu wangu kutoka mikononi mwenu, nao hawatakuwa tena mawindo ya nguvu zenu. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana. 22 Kwa sababu mliwavunja moyo wenye haki kwa uongo wenu, wakati mimi sikuwaletea huzuni na kwa kuwa mliwatia moyo waovu ili wasiziache njia zao mbaya na hivyo kuokoa maisha yao, 23 kwa hiyo hamtaona tena maono ya uongo wala kufanya ubashiri. Nitawaokoa watu wangu kutoka mikononi mwenu. Nanyi ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.’ ”

14:1 Baadhi ya wazee wa Israeli walinijia na kuketi mbele yangu. 2 Ndipo neno la Bwana likanijia kusema: 3 “Mwanadamu, watu hawa wameweka sanamu katika mioyo yao na kuweka vitu viovu vya kukwaza mbele ya macho yao. Je, kweli niwaruhusu waniulize jambo lolote? 4 Kwa hiyo sema nao uwaambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Wakati Mwisraeli yeyote anapoweka sanamu moyoni mwake na kuweka kitu kiovu cha kukwaza mbele ya macho yake na kisha akaenda kwa nabii, Mimi Bwana nitamjibu peke yangu sawasawa na ukubwa wa ibada yake ya sanamu. 5 Nitafanya jambo hili ili kukamata tena mioyo ya watu wa Israeli, ambao wote wameniacha kwa ajili ya sanamu zao.’

6 “Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Tubuni! Geukeni kutoka kwenye sanamu zenu na mkatae matendo yenu yote ya machukizo!

7 “ ‘Mwisraeli yeyote au mgeni yeyote anayeishi katika Israeli anapojitenga nami na kujiwekea sanamu katika moyo wake na kwa hivyo kuweka kitu kiovu cha kukwaza mbele ya macho yake na kisha akamwendea nabii kuuliza shauri kwangu, mimi Bwana nitamjibu mwenyewe. 8 Nitaukaza uso wangu dhidi ya mtu huyo na kumwadhibu na kumfanya ishara kwa watu. Nitamkatilia mbali kutoka watu wangu. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.

9 “ ‘Naye nabii kama atakuwa ameshawishika kutoa unabii, Mimi Bwana nitakuwa nimemshawishi nabii huyo, nami nitaunyoosha mkono wangu dhidi yake na kumwangamiza kutoka miongoni mwa watu wangu Israeli. 10 Watachukua hatia yao, nabii atakuwa na hatia sawa na yule mtu aliyekuja kuuliza neno kwake.

11 “ ‘Ndipo watu wa Israeli hawataniacha tena, wala kujitia unajisi tena kwa dhambi zao zote. Ndipo watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao, asema Bwana Mwenyezi.’ ”

12 Neno la Bwana likanijia kusema, 13 “Mwanadamu, kama nchi itanitenda dhambi kwa kutokuwa waaminifu nami nikinyoosha mkono wangu dhidi yake kukatilia mbali upatikanaji wake wa chakula na kuipelekea njaa na kuua watu wake na wanyama wao, 14 hata kama watu hawa watatu: Noa, Danieli na Ayubu wangekuwa ndani ya nchi hiyo, ndio hao tu wangeweza kujiokoa wenyewe kwa uadilifu wao, asema Bwana Mwenyezi.

15 “Au kama nikipeleka wanyama pori katika nchi hiyo yote na kuifanya isiwe na watoto, nayo ikawa ukiwa kwamba hakuna mtu apitaye katika nchi hiyo kwa sababu ya wanyama pori, 16 hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, hata kama watu hawa watatu wangekuwa humo ndani yake, wasingeweza kuokoa wana wao wala binti zao. Wao peke yao wangeokolewa, lakini nchi ingekuwa ukiwa.

17 “Au kama nikileta upanga dhidi ya nchi hiyo na kusema, ‘Upanga na upite katika nchi yote,’ nami nikiua watu wake na wanyama wao, 18 hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, hata kama watu hawa watatu wangekuwa humo ndani yake, wasingeweza kuokoa wana wao wala binti zao. Wao wenyewe tu wangeokolewa.

19 “Au kama nikipeleka tauni katika nchi hiyo na kumwaga ghadhabu yangu juu yake kwa njia ya kumwaga damu, kuua watu wake na wanyama wao, 20 hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, hata kama Noa, Danieli na Ayubu wangekuwa humo ndani yake, wasingeweza kumwokoa mwana wala binti. Wao wangeweza kujiokoa wenyewe tu kwa uadilifu wao.

21 “Kwa maana hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Itakuwa vibaya kiasi gani nitakapopeleka dhidi ya Yerusalemu hukumu zangu nne za kutisha, yaani, upanga, njaa, wanyama pori na tauni, ili kuua watu wake na wanyama wao! 22 Lakini watakuwepo wenye kuokoka, wana na binti wataletwa kutoka nje ya nchi hiyo. Watawajia ninyi, nanyi mtakapoona mwenendo wao na matendo yao, mtafarijika kuhusu maafa niliyoleta juu ya Yerusalemu, kwa ajili ya yale yote niliyoleta juu yake. 23 Mtafarijika wakati mtakapoona mwenendo wao na matendo yao, kwa kuwa mtajua kwamba sikufanya lolote ndani yake bila sababu, asema Bwana Mwenyezi.”

15:1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, je, ni vipi mti wa mzabibu unaweza kuwa bora zaidi kuliko tawi la mti mwingine wowote ndani ya msitu? 3 Je, mti wake kamwe huchukuliwa na kutengeneza chochote cha manufaa? Je, watu hutengeneza vigingi vya kuningʼinizia vitu kutokana na huo mti wake? 4 Nao baada ya kutiwa motoni kama nishati na moto ukateketeza ncha zote mbili na kuunguza sehemu ya kati, je, unafaa kwa lolote? 5 Kama haukufaa kitu chochote ulipokuwa mzima, je, si zaidi sana sasa ambapo hauwezekani kufanyishwa chochote cha kufaa baada ya moto kuuchoma na kuuunguza?

6 “Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kama nilivyoutoa mti wa mzabibu miongoni mwa miti ya msituni kuwa nishati kwa ajili ya moto, hivyo ndivyo nitakavyowatendea watu waishio Yerusalemu. 7 Nitaukaza uso wangu dhidi yao. Ingawa watakuwa wameokoka kwenye moto, bado moto utawateketeza. Nami nitakapoukaza uso wangu dhidi yao, ninyi mtajua kwamba Mimi ndimi Bwana. 8 Nitaifanya nchi kuwa ukiwa kwa sababu wamekuwa si waaminifu, asema Bwana Mwenyezi.”