Petro Anatangaza Kristo Kuwa Mwokozi wa Wote
Petro anatangaza kwa mara ya kwanza kwamba Kristo ni Mwokozi wa wote wanaomwamini, hata watu wa Mataifa.
karibu 40 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
34 Ndipo Petro akafungua kinywa chake akasema, “Mungu hana upendeleo, 35 Lakini katika kila taifa, kila mtu amchaye na kutenda yaliyo haki hukubaliwa naye. 36 Ninyi mnajua ule ujumbe uliotumwa kwa Israeli, ukitangaza habari njema za amani kwa Yesu Kristo. Yeye ni Bwana wa wote. 37 Mnajua yale yaliyotukia katika Uyahudi wote kuanzia Galilaya baada ya mahubiri ya Yohana Mbatizaji: 38 Jinsi Mungu alivyomtia Yesu wa Nazareti mafuta katika Roho Mtakatifu na jinsi alivyokwenda huku na huko akitenda mema na kuponya wote waliokuwa wameonewa na nguvu za ibilisi, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye.
39 “Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyoyafanya katika Uyahudi na Yerusalemu. Wakamuua kwa kumtundika msalabani. 40 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu siku ya tatu na akamwezesha kuonekana na watu. 41 Hakuonekana kwa watu wote, lakini kwetu sisi tuliochaguliwa na Mungu kuwa mashahidi, ambao tulikula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. 42 Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote na kushuhudia kwamba ndiye alitiwa mafuta na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu. 43 Manabii wote walishuhudia juu yake kwamba kila mtu amwaminiye hupokea msamaha wa dhambi katika Jina lake.”
Kornelio na Rafiki Zake Wanampokea Roho
Kornelio na rafiki zake wanampokea Roho Mtakatifu na kubatizwa.
44 Wakati Petro alikuwa akisema maneno haya, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wakisikiliza ule ujumbe. 45 Wale wa tohara walioamini waliokuja na Petro walishangaa kwa kuona kuwa kipawa cha Roho Mtakatifu kimemwagwa juu ya watu wa Mataifa. 46 Kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha mpya na kumwadhimisha Mungu.
Ndipo Petro akasema, 47 “Je, kuna mtu yeyote anayeweza kuzuia watu hawa wasibatizwe kwa maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea.” 48 Kwa hiyo akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Wakamsihi Petro akae nao kwa siku chache.
Petro Anatetea Kumbatiza Kornelio
Petro anatetea alichofanya kwa kumtembelea na kumbatiza Kornelio.
1 Mitume na ndugu walioamini waliokuwa huko Uyahudi wakasikia kuwa watu wa Mataifa nao wamepokea neno la Mungu. 2 Hivyo Petro alipopanda Yerusalemu, wale wa tohara waliokuwa wameamini wakamshutumu, 3 wakisema, “Ulikwenda kwa watu wasiotahiriwa na kula pamoja nao.”
4 Ndipo Petro akaanza kuwaeleza kuhusu mambo yote yalivyotokea hatua kwa hatua akisema, 5 “Nilikuwa katika mji wa Yafa nikiomba, nami nikapitiwa na usingizi wa ghafula, nikaona maono. Kulikuwa na kitu kama nguo kubwa ikishuka kutoka mbinguni, ikishushwa kwa ncha zake nne, nayo ikanikaribia. 6 Nilipoangalia ndani yake kwa karibu niliona wanyama wenye miguu minne wa nchini, wanyama wa mwitu, watambaao na ndege wa angani. 7 Ndipo nikasikia sauti ikiniambia, ‘Petro, ondoka uchinje na ule.’
8 “Nikajibu, ‘La hasha Bwana! Kitu chochote kilicho najisi hakijaingia kinywani mwangu.’
9 “Sauti ikasema kutoka mbinguni mara ya pili, ‘Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.’ 10 Jambo hili lilitokea mara tatu, ndipo kile kitu kikavutwa tena mbinguni.
11 “Wakati ule ule watu watatu, waliokuwa wametumwa kutoka Kaisaria waliwasili katika nyumba niliyokuwa nikikaa. 12 Roho Mtakatifu akaniambia niende nao bila kuwa na ubaguzi kati yao na sisi. Hawa ndugu sita pia walifuatana nami, nasi tukaingia nyumbani mwa huyo Kornelio. 13 Akatuambia jinsi alivyoona malaika aliyekuwa amesimama katika nyumba yake na kusema, ‘Tuma watu waende Yafa wakamlete Simoni aitwaye Petro. 14 Yeye atakupa ujumbe ambao kwa huo wewe na wa nyumbani mwako wote mtaokoka.’
15 “Nami nilipoanza kusema, Roho Mtakatifu akashuka juu yao kama vile alivyotushukia sisi hapo mwanzo. 16 Nami nikakumbuka neno la Bwana alivyosema, ‘Yohana alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’ 17 Basi ikiwa Mungu aliwapa hawa watu kipawa kile kile alichotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani hata nifikirie kuwa ningeweza kumpinga Mungu?”
18 Waliposikia haya hawakuwa na la kupinga zaidi. Nao wakamwadhimisha Mungu wakisema, “Basi, Mungu amewapa hata watu wa Mataifa toba iletayo uzima wa milele.”
Waongofu Waliotawanyika Wanawahubiria Watu wa Mataifa Wacha Mungu 41 BK
Waongofu waliokuwa wametawanywa na mateso baada ya kifo cha Stefano, baada ya kusikia kuhusu maono ya Petro, wanawahubiria pia watu wa Mataifa wacha Mungu.
19 Basi wale waliotawanyika kwa ajili ya mateso yaliyotokana na kifo cha Stefano, wakasafiri hadi Foinike na Kipro na Antiokia. Nao hawakuhubiri lile Neno kwa mtu yeyote isipokuwa Wayahudi. 20 Lakini baadhi yao walikuwepo watu wa Kipro na Kirene, ambao walipokuja Antiokia walinena na Wayunani pia wakiwahubiria habari njema za Bwana Yesu. 21 Mkono wa Bwana ulikuwa pamoja nao, nayo idadi kubwa ya watu wakaamini na kumgeukia Bwana.