Huduma ya Paulo kwa Watu wa Mataifa na Mipango Yake

Akiwa sasa amekamilisha sehemu za barua yake zinazohusu mafundisho na maisha ya kila siku, Paulo anawageukia hasa watu wa Mataifa. Anasadiki kwamba wamejaa wema na ujuzi wa kusudi la Mungu kwao kiasi kwamba wanaweza kuonyana wao kwa wao. Hata hivyo, amewaandikia kwa ujasiri kwa sababu ya wadhifa wake wa utume, alioupokea kutoka kwa Mungu ili watu wa Mataifa waongoke, ambao sasa anawatoa kwa Mungu kama sadaka inayokubalika. Anajivunia mafanikio ya huduma yake mwenyewe, huku Kristo akifanya kazi pamoja naye na kuthibitisha mafundisho yake na utume wake kwa ishara na maajabu makuu, kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Hamu yake ya kuhubiri injili mahali ambapo ilikuwa bado haijajulikana ilikuwa imemzuia kutembelea Rumi, ambako ilikuwa tayari imepandwa. Lakini sasa, kwa kuwa hana kazi nyingine iliyobaki huko, anatumaini kuwaona akiwa njiani kwenda Hispania, na kufurahia kuwa pamoja nao katika safari hiyo. Anataja safari anayopanga kwenda Yerusalemu, ili kupeleka michango ya watu wa Mataifa walioongoka kupitia huduma yake kwa Wayahudi walioongoka huko Yerusalemu, akitumaini kwa njia hii kuwapatanisha: kwa kuwa watu wa Mataifa walipata kujua mambo ya kiroho kupitia Wayahudi, wana wajibu wa kuwalipa kwa vitu vya kimwili. Anarudia kwamba anakusudia kuwatembelea baada ya kukabidhi michango hiyo, akileta karama na baraka za injili ya Kristo. Anawahimiza wamwombee kwa bidii ili aokolewe kutoka kwa Wayahudi wasioamini, waliotaka kumwangamiza, na ili mchango wake ukubalike kwa Wayahudi Wakristo. Anamalizia kwa kueleza tumaini lake la kuwaona, ili wao na yeye waimarishwe kwa kushirikishana karama za kiroho, na kwa kuwapa baraka zake.

58 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Warumi 15:14–33

14 Ndugu zangu, mimi mwenyewe ninasadiki kwamba mmejaa wema na ufahamu wote, tena mnaweza kufundishana ninyi kwa ninyi. 15 Nimewaandikia kwa ujasiri vipengele kadha wa kadha katika waraka huu kama kuwakumbusha tena kwa habari ya ile neema Mungu aliyonipa, 16 ili kuwa mhudumu wa Kristo Yesu kwa watu wa Mataifa nikiwa na huduma ya kikuhani ya kutangaza Injili ya Mungu, ili watu wa Mataifa wapate kuwa dhabihu inayokubaliwa na Mungu, iliyotakaswa na Roho Mtakatifu.

17 Kwa hiyo ninajisifu katika Kristo Yesu, kwenye utumishi wangu kwa Mungu. 18 Kwa maana sitathubutu kusema kitu chochote zaidi ya kile ambacho Kristo amefanya kwa kunitumia mimi katika kuwaongoza watu wa Mataifa wamtii Mungu kwa yale niliyosema na kufanya, 19 kwa nguvu za ishara na miujiza, kwa uweza wa Roho wa Mungu, hivyo kuanzia Yerusalemu hadi maeneo yote ya kandokando yake mpaka Iliriko, nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa ukamilifu. 20 Hivyo ni nia yangu kuhubiri Habari Njema, si pale ambapo Kristo amekwisha kujulikana, ili nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine. 21 Lakini kama ilivyoandikwa:

“Wale ambao hawajahubiriwa habari zake wataona,

nao wale ambao hawajazisikia watafahamu.”

22 Hii ndiyo sababu nimezuiliwa mara nyingi nisiweze kuja kwenu.

23 Lakini sasa kwa kuwa hakuna nafasi zaidi kwa ajili yangu katika sehemu hii, ninatamani kuja kwenu kama ambavyo nimekuwa na shauku kwa miaka mingi. 24 Nimekusudia kufanya hivyo nitakapokuwa njiani kwenda Hispania. Natarajia kuwaona katika safari yangu na kusafirishwa nanyi mpaka huko, baada ya kufurahia ushirika wenu kwa kitambo kidogo. 25 Sasa, niko njiani kuelekea Yerusalemu kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu huko. 26 Kwa kuwa imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya maskini walioko miongoni mwa watakatifu huko Yerusalemu. 27 Imewapendeza kufanya hivyo, naam, kwani ni wadeni wao. Kwa maana ikiwa watu wa Mataifa wameshiriki baraka za rohoni za Wayahudi, wao ni wadeni wa Wayahudi, ili Wayahudi nao washiriki baraka zao za mambo ya mwilini. 28 Kwa hiyo baada ya kukamilisha kazi hii na kuhakikisha kuwa wamepokea kila kitu kilichokusanywa, nitapitia kwenu nikiwa njiani kwenda Hispania. 29 Ninajua kwamba nitakapokuja kwenu, nitakuja na wingi wa baraka za Kristo.

30 Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa Jina la Bwana wetu Yesu Kristo na kwa upendo wa Roho Mtakatifu, kujiunga nami katika taabu zangu mkiniombea kwa Mungu. 31 Ombeni ili nipate kuokolewa mikononi mwa wale wasioamini walioko Uyahudi, na kwamba utumishi wangu upate kukubaliwa na watakatifu wa huko Yerusalemu, 32 ili kwa mapenzi ya Mungu niweze kuja kwenu kwa furaha, nami niburudishwe pamoja nanyi. 33 Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amen.

Paulo Anampendekeza Foibe na Kuwasalimu Rafiki Zake

Paulo anampendekeza Foibe, aliyeibeba barua hii, kwa Wakristo wa Rumi ili wamsaidie. Anawasalimu Akila na Prisila, anaowasifu sana, na kanisa lililo nyumbani kwao. Anawasalimu wengi wa rafiki zake Wakristo ambao sasa walikuwa wamekaa Rumi, na huenda baadhi yao walikuwa wameongoka kupitia yeye mwenyewe.

Warumi 16:1–16

1 Napenda kumtambulisha kwenu dada yetu Foibe, mtumishi katika kanisa la Kenkrea. 2 Naomba mpokeeni katika Bwana ipasavyo watakatifu na kumpa msaada wowote atakaohitaji kutoka kwenu, kwa maana yeye amekuwa msaada kwa watu wengi, mimi nikiwa miongoni mwao.

3 Wasalimuni Prisila na Akila, watumishi wenzangu katika Kristo Yesu. 4 Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu; wala si mimi tu ninayewashukuru bali pia makanisa yote ya watu wa Mataifa.

5 Lisalimuni pia kanisa linalokutana nyumbani mwao.

Msalimuni rafiki yangu mpendwa Epaineto, aliyekuwa mtu wa kwanza kumwamini Kristo huko Asia.

6 Msalimuni Maria, aliyefanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu.

7 Wasalimuni Androniko na Yunia, jamaa zangu ambao wamekuwa gerezani pamoja nami. Wao ni maarufu miongoni mwa mitume, nao walikuwa katika Kristo kabla yangu.

8 Msalimuni Ampliato, yeye nimpendaye katika Bwana.

9 Msalimuni Urbano, mtendakazi mwenzetu katika Kristo, pamoja na rafiki yangu mpendwa Stakisi.

10 Msalimuni Apele aliyejaribiwa na akaithibitisha imani yake katika Kristo.

Wasalimuni wote walio nyumbani mwa Aristobulo.

11 Msalimuni ndugu yangu Herodioni.

Wasalimuni wote walio nyumbani mwa Narkisi walio katika Bwana.

12 Wasalimuni Trifaina na Trifosa, wale wanawake wanaofanya kazi kwa bidii katika Bwana.

Msalimuni rafiki yangu mpendwa Persisi, mwanamke mwingine aliyefanya kazi kwa bidii katika Bwana.

13 Msalimuni Rufo, mteule katika Bwana, pamoja na mama yake, ambaye amekuwa mama kwangu pia.

14 Wasalimuni Asinkrito, Flegoni, Herme, Patroba, Herma na ndugu wote walio pamoja nao.

15 Wasalimuni Filologo, Yulia, Nerea na dada yake, na Olimpa na watakatifu wote walio pamoja nao.

16 Salimianeni ninyi kwa ninyi kwa busu takatifu.

Makanisa yote ya Kristo yanawasalimu.

Waepukeni Wale Wanaosababisha Migawanyiko

Paulo anawaonya tena waepuke migawanyiko na watu wanaoisababisha. Watu hao hawamtumikii Kristo kwa kuhubiri mafundisho yake, bali wanatamani tu faida za kidunia; na kwa kuwa hawana karama za kiroho, wanadanganya au kupotosha mioyo ya waongofu Wakristo wasio na mashaka nao kwa maneno matamu na sifa za kujipendekeza. Anaufurahia utii wao wa sasa, na anawahimiza waendelee kutambua na kufanya yaliyo mema, na wawe safi, au wasio na hatia, kuhusu uovu: yaani, waepuke mafundisho yote ya uongo na mifano yote mibaya. Anatabiri kuangamizwa upesi kwa mawakala wa Shetani wanaoleta migawanyiko kanisani, na anamalizia kwa baraka yake.

Warumi 16:17–20

17 Ndugu zangu, nawasihi mjihadhari na kujiepusha na wale watu waletao matengano na kuweka vikwazo mbele yenu dhidi ya mafundisho mliyojifunza. 18 Kwa maana watu kama hao hawamtumikii Bwana Kristo, bali wanatumikia tamaa zao wenyewe. Kwa kutumia maneno laini na ya kubembeleza, hupotosha mioyo ya watu wajinga. 19 Kila mtu amesikia juu ya utii wenu, nami nimejawa na furaha tele kwa ajili yenu. Lakini nataka mwe na hekima katika mambo mema na bila hatia katika mambo maovu.

20 Mungu wa amani atamponda Shetani chini ya miguu yenu upesi.

Neema ya Bwana wetu Yesu iwe nanyi. Amen.

Salamu na Utukufu kwa Mungu Pekee Mwenye Hekima

Katika nyongeza ya barua, Paulo anatuma salamu za watu kadhaa waliokuwa pamoja naye. Anahitimisha yote kwa kumpa utukufu Mungu, ambaye peke yake ana uwezo wa kuwaimarisha katika imani ya kweli ya Kristo bila Sheria ya Mose. Hili hapo awali lilikuwa fumbo lililowekwa siri (ingawa kuitwa kwa watu wa Mataifa kulikuwa kumetabiriwa), lakini sasa limefahamishwa kwa amri ya Mungu wa milele iliyofunuliwa kwa Paulo, ili kwa mahubiri yake mataifa yote yapate kuujua utii wa imani, yaamini na kutii. “Kwa Mungu pekee mwenye hekima uwe utukufu milele.”

Warumi 16:21–27

21 Timotheo, mtendakazi mwenzangu anawasalimu. Vivyo hivyo Lukio, Yasoni, na Sosipatro, ndugu zangu.

22 Mimi, Tertio, niliye mwandishi wa waraka huu, nawasalimu katika Bwana.

23 Gayo, ambaye ni mwenyeji wangu na wa kanisa lote, anawasalimu.

Erasto, mweka hazina wa mji huu, pamoja na Kwarto ndugu yetu pia wanawasalimu.

[ 24 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi nyote. Amen.]

25 Sasa atukuzwe yeye awezaye kuwafanya ninyi imara kwa Injili yangu na kuhubiriwa kwa Yesu Kristo, kutokana na kufunuliwa siri zilizofichika tangu zamani za kale. 26 Lakini sasa siri hiyo imefunuliwa na kujulikana kupitia maandiko ya kinabii kutokana na amri ya Mungu wa milele, ili mataifa yote yaweze kumwamini na kumtii 27 Mungu aliye pekee, mwenye hekima, ambaye kwa njia ya Yesu Kristo utukufu ni wake milele na milele! Amen.