Mose Arudia Sheria ya Maadili (continued)
1451 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Haya ndiyo maagizo, amri na sheria ambazo Bwana Mungu wenu aliniagiza niwafundishe ninyi ili mpate kuyashika katika nchi ambayo ninyi mnavuka Yordani kuimiliki, 2 ili kwamba ninyi, watoto wenu na watoto wao baada yao wamche Bwana Mungu wenu siku zote kwa kushika amri na maagizo yake yote ninayowapa, ili mweze kuyafurahia maisha marefu. 3 Sikia, ee Israeli, nawe uwe mwangalifu kutii ili upate kufanikiwa na kuongezeka sana katika nchi itiririkayo maziwa na asali, kama Bwana, Mungu wa baba zenu, alivyowaahidi ninyi.
4 Sikia, ee Israeli: Bwana Mungu wako, Bwana ni mmoja. 5 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. 6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. 7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo. 8 Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako. 9 Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.
10 Wakati Bwana Mungu wako atakapokuleta katika nchi aliyowaapia baba zako, Abrahamu, Isaki na Yakobo, kukupa wewe, nchi kubwa, ina miji inayopendeza ambayo hukuijenga, 11 nyumba zilizojaa vitu vizuri vya aina nyingi ambavyo hukuvijaza, visima ambavyo hukuchimba, na mashamba ya mizabibu na mizeituni ambayo hukupanda wewe, basi, utakapokula na kushiba, 12 jihadhari usije ukamwacha Bwana, aliyekutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa.
13 Utamcha Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake na kuapa kwa jina lake. 14 Usifuate miungu mingine, miungu ya mataifa yanayokuzunguka; 15 kwa kuwa Bwana Mungu wako, ambaye yuko katikati yako, ni Mungu mwenye wivu na hasira yake itawaka dhidi yako, naye atakuangamiza kutoka uso wa nchi. 16 Usimjaribu Bwana Mungu wako kama ulivyofanya huko Masa. 17 Utayashika maagizo ya Bwana Mungu wako kwa bidii, na masharti na amri alizokupa. 18 Fanya lililo haki na jema mbele za Bwana, ili upate kufanikiwa, uweze kuingia na kuimiliki nchi nzuri ambayo Bwana aliahidi kwa kiapo kwa baba zako, 19 kuwafukuza kwa nguvu adui zako mbele yako kama Bwana alivyosema.
20 Siku zijazo, mtoto wako atakapokuuliza, “Ni nini maana ya masharti haya, amri na sheria hizi ambazo Bwana Mungu wako alikuagiza wewe?” 21 Mwambie: “Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri, lakini Bwana alitutoa sisi kutoka Misri kwa mkono wenye nguvu. 22 Bwana akapeleka mbele yetu ishara za miujiza na maajabu makubwa na ya kutisha mno juu ya Misri na Farao pamoja na nyumba yake yote. 23 Lakini Mungu akatutoa huko, akatuleta na kutupa nchi hii ambayo aliwaahidi baba zetu kwa kiapo. 24 Bwana akatuagiza tutii amri hizi zote na kumcha Bwana Mungu wetu, ili tupate kustawi na kuendelea kuwa hai kama ilivyo leo. 25 Kama tukizitii kwa bidii amri hizi zote mbele za Bwana Mungu wetu, kama alivyotuamuru sisi, hiyo itakuwa haki yetu.”
7:1 Bwana Mungu wako akuletapo katika nchi unayoingia kuimiliki, na awafukuzapo mbele yako mataifa mengi, yaani Wahiti, Wagirgashi, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, mataifa saba makubwa tena yenye nguvu kuliko wewe, 2 pia Bwana Mungu wako atakapowatia mkononi mwako na ukawashinda, basi ni lazima uwaangamize wote kabisa. Usifanye agano nao, wala usiwahurumie. 3 Usioane nao. Usimtoe binti yako kuolewa na mwanawe, au kumchukua binti yake aolewe na mwanao. 4 Kwa maana watamgeuza mwanao aache kunifuata, ili aitumikia miungu mingine, nayo hasira ya Bwana itawaka dhidi yako, naye atakuangamiza ghafula. 5 Hili ndilo utakalowafanyia: Vunja madhabahu yao, vunja mawe yao ya kuabudia, katakata nguzo zao za Ashera na kuchoma sanamu zao kwa moto. 6 Kwa kuwa wewe ni taifa takatifu kwa Bwana Mungu wako. Bwana Mungu wako amekuchagua wewe kutoka mataifa yote juu ya uso wa dunia kuwa watu wake, hazina yake ya thamani.
7 Bwana hakuweka upendo wake juu yenu na kuwachagua kwa sababu mlikuwa wengi mno kuliko watu wengine, kwa maana ninyi ndio mliokuwa wachache sana kuliko mataifa yote. 8 Lakini ni kwa sababu Bwana aliwapenda ninyi na kutunza kiapo alichowaapia babu zenu kwamba atawatoa ninyi kwa mkono wenye nguvu na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa, kutoka nguvu za Farao mfalme wa Misri. 9 Basi ujue kwamba Bwana Mungu wako ndiye Mungu; ni Mungu mwaminifu, anayetunza Agano la upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanaompenda na kuzishika amri zake. 10 Lakini
kwa wale wanaomchukia
atawalipiza kwenye nyuso zao
kwa maangamizi;
hatachelewa kuwalipiza kwenye nyuso zao
wale wamchukiao.
11 Kwa hiyo, kuweni waangalifu kufuata maagizo, amri na sheria ninazowapa leo.
12 Kama mkizingatia sheria hizi na kuzifuata kwa uangalifu, basi Bwana Mungu wenu atatunza Agano lake la upendo nanyi, kama alivyowaapia baba zenu. 13 Atawapenda ninyi na kuwabariki na kuongeza idadi yenu. Atabariki uzao wa tumbo lenu, mazao ya nchi yenu, nafaka, divai mpya na mafuta, ndama za ngʼombe wa makundi yenu, na kondoo za makundi yenu katika nchi ile aliyoapa kuwapa baba zenu. 14 Mtabarikiwa kuliko mataifa mengine yote, hakuna wanaume wala wanawake kwenu watakaokosa watoto, wala mifugo yenu haitakuwa tasa. 15 Bwana atawakinga na kila ugonjwa. Mungu hatatia juu yenu ugonjwa wowote mbaya mlioufahamu huko Misri, lakini atatia ugonjwa juu ya wale wote wanaokuchukia. 16 Ni lazima mwangamize watu wote ambao Bwana Mungu wenu atawatia mikononi mwenu. Msiwatazame kwa kuwahurumia na msiitumikie miungu yao, kwa kuwa itakuwa mtego kwenu.
17 Mnaweza kujiuliza wenyewe “Mataifa haya ni yenye nguvu kuliko sisi. Tutawezaje kuwafukuza?” 18 Lakini msiwaogope. Kumbukeni vyema jinsi Bwana Mungu wenu alivyofanya kwa Farao na kwa wote huko Misri. 19 Mliona kwa macho yenu wenyewe majaribu makubwa, ishara za miujiza na maajabu, mkono wenye nguvu na ulionyooshwa, ambao kwa huo Bwana Mungu wenu aliwatoa mtoke Misri. Bwana Mungu wenu atawafanyia hivyo watu wote ambao mnawaogopa sasa. 20 Zaidi ya hayo, Bwana Mungu wenu atatuma manyigu miongoni mwao hadi yale mabaki watakaojificha waangamie. 21 Msiingiwe na hofu kwa sababu yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu, ambaye yupo miongoni mwenu ni mkuu naye ni Mungu wa kutisha. 22 Bwana Mungu wenu atawafukuza mataifa hayo mbele yenu kidogo kidogo. Hamtaruhusiwa kuwaondoa wote kwa mara moja, la sivyo wanyama mwitu wataongezeka na kuwa karibu nanyi. 23 Lakini Bwana Mungu wenu atawatia watu hao mikononi mwenu, akiwatia katika kuchanganyikiwa kukubwa mpaka wawe wameangamizwa. 24 Atawatia wafalme wao mikononi mwenu, nanyi mtayafuta majina yao chini ya mbingu. Hakuna hata mmoja atakayeweza kusimama dhidi yenu bali mtawaangamiza. 25 Vinyago vya miungu yao mtavichoma moto. Msitamani fedha wala dhahabu iliyo juu yao, wala msizichukue kwa ajili yenu, la sivyo mtakuwa mmetekwa navyo. Kwa kuwa ni chukizo kwa Bwana Mungu wenu. 26 Msilete vitu vya machukizo katika nyumba zenu kwani ninyi, mtatengwa kama vitu hivyo kwa maangamizo. Ukichukie kabisa kitu hicho kwa kuwa kimetengwa kwa maangamizo.