Sehemu ya 2: Mose Anapewa Utume
Mose apewa jukumu la kuwa mjumbe wa Mungu.
1491 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Basi Mose alikuwa anachunga mifugo ya Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani. Mose akapeleka mifugo mbali nyuma ya jangwa, naye akafika Horebu, mlima wa Mungu. 2 Huko malaika wa Bwana akamtokea Mose katika mwali wa moto kutoka kichakani. Mose akaona kwamba ingawa kile kichaka kilikuwa kinawaka moto, kilikuwa hakiteketei. 3 Ndipo Mose akawaza, “Nitageuka sasa nione kitu hiki cha ajabu, nami nione ni kwa nini kichaka hiki hakiteketei.”
4 Bwana alipoona kuwa amegeuka ili aone, Mungu akamwita kutoka ndani ya kile kichaka, “Mose! Mose!”
Naye Mose akajibu, “Mimi hapa.”
5 Mungu akamwambia, “Usikaribie zaidi. Vua viatu vyako, kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu.” 6 Kisha akamwambia, “Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo.” Mose aliposikia hayo, akafunika uso wake kwa sababu aliogopa kumtazama Mungu.
7 Bwana akamwambia, “Hakika nimeona mateso ya watu wangu katika Misri. Nimesikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao, nami naguswa na mateso yao. 8 Basi nimeshuka niwaokoe kutoka mkono wa Wamisri, niwatoe na kuwapandisha kutoka nchi hiyo, niwapeleke katika nchi nzuri na kubwa, nchi itiririkayo maziwa na asali, nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. 9 Sasa kilio cha Waisraeli kimenifikia, nami nimeona jinsi Wamisri wanavyowatesa. 10 Basi, sasa nenda. Ninakutuma kwa Farao ili kuwatoa watu wangu Waisraeli kutoka Misri.”
11 Lakini Mose akamwambia Mungu, “Mimi ni nani hata niende kwa Farao kuwatoa Waisraeli nchini Misri?”
12 Naye Mungu akasema, “Mimi nitakuwa pamoja nawe. Hii itakuwa ishara kwako kwamba ni Mimi nimekutuma: Hapo utakapokuwa umewatoa watu Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu.”
13 Mose akamwambia Mungu, “Ikiwa nitawaendea Waisraeli na kuwaambia, ‘Mungu wa baba zenu amenituma kwenu,’ nao wakiniuliza, ‘Jina lake ni nani?’ Nitawaambia nini?”
14 Mungu akamwambia Mose, “Mimi niko ambaye niko. Hivyo ndivyo utakavyowaambia Waisraeli: ‘Mimi niko amenituma kwenu.’ ”
15 Vilevile Mungu akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli, ‘Bwana, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo amenituma kwenu.’ Hili ndilo Jina langu milele, Jina ambalo mtanikumbuka kwalo kutoka kizazi hadi kizazi.
16 “Nenda, ukawakusanye wazee wa Israeli, uwaambie, ‘Bwana, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Abrahamu, Isaki na Yakobo, alinitokea akaniambia: Nimewatazama, nami nimeona mliyofanyiwa katika Misri. 17 Nami nimeahidi kuwapandisha kutoka mateso yenu katika nchi ya Misri, niwapeleke nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, nchi itiririkayo maziwa na asali.’
18 “Wazee wa Israeli watakusikiliza. Kisha wewe na wazee mtakwenda kwa mfalme wa Misri na kumwambia, ‘Bwana, Mungu wa Waebrania ametutokea. Turuhusu twende safari ya siku tatu huko jangwani kutoa dhabihu kwa Bwana Mungu wetu.’ 19 Lakini nafahamu kwamba mfalme wa Misri hatawaruhusu kwenda, mpaka mkono wenye nguvu umlazimishe. 20 Kwa hiyo nitaunyoosha mkono wangu na kuwapiga Wamisri kwa maajabu yote nitakayofanya miongoni mwao. Baada ya hayo, atawaruhusu mwondoke.
21 “Nami nitawapa hawa watu upendeleo mbele ya Wamisri, kwa hiyo mtakapoondoka nchini hamtaondoka mikono mitupu. 22 Kila mwanamke Mwisraeli atamwomba jirani yake Mmisri na mwanamke yeyote anayeishi nyumbani kwake ampe vyombo vya fedha, dhahabu na nguo, ambavyo mtawavika wana wenu na binti zenu. Hivyo mtawateka nyara Wamisri.”
4:1 Mose akamjibu, “Itakuwaje kama hawataniamini au kunisikiliza, waseme, ‘Bwana hakukutokea’?”
2 Ndipo Bwana akamwambia, “Ni nini hicho kilicho mkononi mwako?”
Akajibu, “Fimbo.”
3 Bwana akasema, “Itupe chini.”
Mose akaitupa chini hiyo fimbo nayo ikawa nyoka, naye akaikimbia. 4 Kisha Bwana akamwambia, “Nyoosha mkono wako umkamate mkiani.” Basi Mose akanyoosha mkono akamkamata yule nyoka, naye akabadilika tena kuwa fimbo mkononi mwake. 5 Bwana akasema, “Hivi ndivyo Waisraeli watakavyoamini kuwa Bwana, Mungu wa baba zao, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo, amekutokea wewe.”
6 Kisha Bwana akamwambia, “Weka mkono wako ndani ya joho lako.” Basi Mose akaweka mkono wake ndani ya joho lake, naye alipoutoa, ulikuwa na ukoma, mweupe kama theluji.
7 Mungu akamwambia, “Sasa urudishe tena huo mkono ndani ya joho lako.” Basi Mose akaurudisha mkono wake ndani ya joho lake na alipoutoa, ulikuwa mzima, kama sehemu zingine za mwili wake.
8 Ndipo Bwana akamwambia, “Kama hawatakuamini wewe, au kutojali ishara ya kwanza, wataamini ishara ya pili. 9 Lakini kama hawataamini ishara hizi mbili au hawatawasikiliza ninyi, chukua kiasi cha maji kutoka Mto Naili uyamimine juu ya ardhi kavu. Maji mtakayotoa mtoni yatakuwa damu juu ya ardhi.”
10 Mose akamwambia Bwana, “Ee Bwana, kamwe sijapata kuwa msemaji kwa ufasaha wakati uliopita wala tangu ulipoanza kuzungumza na mtumishi wako. Ulimi wangu ni mzito kuzungumza.”
11 Bwana akamwambia, “Ni nani aliyempa mwanadamu kinywa? Ni nani aliyemfanya mtu kuwa kiziwi au bubu? Ni nani anayempa mtu kuona au upofu? Je, si mimi, Bwana? 12 Sasa nenda, nitakusaidia kusema, nami nitakufundisha jambo la kusema.”
13 Lakini Mose akasema, “Ee Bwana, tafadhali mtume mtu mwingine kufanya kazi hiyo.”
14 Ndipo hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Mose, akamwambia, “Vipi kuhusu ndugu yako, Aroni Mlawi? Ninajua yeye anaweza kuzungumza vizuri. Naye yuko tayari njiani kukulaki, na moyo wake utafurahi wakati atakapokuona. 15 Utazungumza naye na kuweka maneno kinywani mwake. Nitawasaidia ninyi wawili kusema, nami nitawafundisha jambo la kufanya. 16 Aroni ataongea na watu badala yako na itakuwa kwamba yeye amekuwa kinywa chako nawe utakuwa kama Mungu kwake. 17 Lakini chukua fimbo hii mkononi mwako ili uweze kuitumia kufanya ishara hizo za ajabu.”
18 Kisha Mose akarudi kwa Yethro mkwewe akamwambia, “Niruhusu nirudi kwa watu wangu Misri kuona kama yuko hata mmoja wao ambaye bado anaishi.”
Yethro akamwambia, “Nenda, nami nakutakia mema.”
19 Basi Bwana alikuwa amemwambia Mose huko Midiani, “Rudi Misri kwa maana watu wote waliotaka kukuua wamekufa.” 20 Basi Mose akamchukua mkewe na wanawe, akawapandisha juu ya punda na kuanza safari kurudi Misri. Naye akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake.
21 Bwana akamwambia Mose, “Utakaporudi Misri, hakikisha kwamba utafanya mbele ya Farao maajabu yote niliyokupa uwezo wa kuyafanya. Lakini nitafanya moyo wake kuwa mgumu ili kwamba asiwaruhusu watu waende. 22 Kisha mwambie Farao, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Israeli ni mwanangu mzaliwa wa kwanza, 23 nami nilikuambia, “Ruhusu mwanangu aondoke, ili aweze kuniabudu mimi.” Lakini ukakataa kumruhusu kwenda, basi nitaua mwana wako mzaliwa wa kwanza.’ ”
24 Mose alipokuwa mahali pa kulala wageni akiwa njiani kurudi Misri, Bwana akakutana naye, akataka kumuua. 25 Lakini Sipora akachukua jiwe gumu, akakata govi la mwanawe na kugusa nalo miguu ya Mose. Sipora akasema, “Hakika wewe ni bwana arusi wa damu kwangu.” 26 Sipora alipomwita Mose, “Bwana arusi wa damu,” alikuwa anamaanisha ile tohara. Baada ya hayo Bwana akamwacha.
27 Bwana akamwambia Aroni, “Nenda jangwani ukamlaki Mose.” Basi akakutana na Mose kwenye mlima wa Mungu, akambusu. 28 Kisha Mose akamwambia Aroni kila kitu Bwana alichomtuma kusema, vilevile habari za ishara na maajabu alizokuwa amemwamuru kufanya.