Sheria Mbalimbali, za Maadili, na za Ibada
1490 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Bwana akamwambia Mose, 2 “Sema na Aroni na wanawe, pamoja na Waisraeli wote, uwaambie: ‘Hili ndilo Bwana aliloagiza: 3 Mwisraeli yeyote atakayetoa dhabihu ya maksai, mwana-kondoo au mbuzi ndani ya kambi au nje yake, 4 badala ya kuileta kwenye ingilio la Hema la Kukutania ili kuileta kama sadaka kwa Bwana mbele ya Maskani ya Bwana, mtu huyo atahesabiwa kuwa na hatia ya kumwaga damu; ni lazima akatiliwe mbali na watu wake. 5 Hii ni ili Waisraeli wamletee Bwana dhabihu wanazozifanya sasa mahali pa wazi mashambani. Ni lazima wazilete kwa makuhani, yaani kwa Bwana, katika ingilio la Hema la Kukutania, na kutoa dhabihu kama sadaka za amani. 6 Kuhani atanyunyiza damu kwenye madhabahu ya Bwana katika ingilio la Hema la Kukutania, na kuyateketeza mafuta ya hiyo dhabihu kuwa harufu nzuri ya kumpendeza Bwana. 7 Hawatatoa kamwe dhabihu zao kwa sanamu za mbuzi ambazo wamekuwa wakijifanyia nazo ukahaba. Hili litakuwa agizo la kudumu kwao na kwa ajili ya vizazi vijavyo.’
8 “Waambie: ‘Mwisraeli yeyote au mgeni yeyote anayeishi miongoni mwao atakayetoa sadaka ya kuteketezwa au dhabihu 9 bila kuileta kwenye ingilio la Hema la Kukutania ili kutoa dhabihu kwa Bwana, mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.
10 “ ‘Mwisraeli yeyote au mgeni anayeishi miongoni mwao ambaye atakunywa damu yoyote, nitakuwa kinyume cha mtu huyo atakayekunywa damu na kumkatilia mbali na watu wake. 11 Kwa kuwa uhai wa kiumbe uko ndani ya damu, nami nimewapa hiyo damu ili mfanyie upatanisho kwa ajili yenu wenyewe juu ya madhabahu; damu ndiyo ifanyayo upatanisho kwa ajili ya maisha ya mtu. 12 Kwa hiyo, ninawaambia Waisraeli, “Hakuna hata mmoja wenu anayeruhusiwa kunywa damu, wala mgeni anayeishi miongoni mwenu haruhusiwi kunywa damu.”
13 “ ‘Mwisraeli yeyote au mgeni anayeishi miongoni mwenu ambaye atamwinda mnyama au ndege anayeruhusiwa kuliwa ni lazima aimwage damu na kuifunika kwa udongo, 14 kwa sababu uhai wa kila kiumbe ni katika damu yake. Ndiyo sababu nimewaambia Waisraeli, “Kamwe msinywe damu ya kiumbe chochote, kwa sababu uhai wa kila kiumbe ni katika damu yake; yeyote atakayekunywa damu ni lazima akatiliwe mbali.”
15 “ ‘Mtu yeyote, awe mzawa au mgeni, ambaye atakula mzoga wa kitu chochote ama kilichouawa na wanyama mwitu ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi kwa kawaida ya ibada mpaka jioni, kisha atakuwa safi. 16 Lakini kama hakufua nguo zake na kuoga, atakuwa na hatia kwa kosa hilo.’ ”
18:1 Bwana akamwambia Mose, 2 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Mimi ndimi Bwana Mungu wenu. 3 Msifanye kama wafanyavyo huko Misri, mahali mlipokuwa mnaishi, wala msifanye kama wanavyofanya katika nchi ya Kanaani, mahali ninapowapeleka. Msifuate matendo yao. 4 Ni lazima mzitii sheria zangu, na mwe waangalifu kuzifuata amri zangu. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu. 5 Zishikeni amri zangu na sheria zangu, kwa maana mtu anayezitii ataishi kwa hizo. Mimi ndimi Bwana.
6 “ ‘Hakuna mtu awaye yote atakayemsogelea ndugu wa karibu ili kukutana naye kimwili. Mimi ndimi Bwana.
7 “ ‘Usimvunjie heshima baba yako kwa kukutana kimwili na mama yako. Yeye ni mama yako; usiwe na mahusiano kama hayo naye.
8 “ ‘Usikutane kimwili na mke wa baba yako; hiyo itamvunjia heshima baba yako.
9 “ ‘Usikutane kimwili na dada yako, wala binti wa baba yako, au binti wa mama yako, awe amezaliwa katika nyumba hiyo au mahali pengine.
10 “ ‘Usikutane kimwili na binti wa mwanao ama binti wa binti yako; utajivunjia heshima.
11 “ ‘Usikutane kimwili na binti wa mke wa baba yako, aliyezaliwa na baba yako; huyo ni dada yako.
12 “ ‘Usikutane kimwili na dada wa baba yako; ni ndugu wa karibu wa baba yako.
13 “ ‘Usikutane kimwili na dada wa mama yako, kwa sababu ni ndugu wa mama yako wa karibu.
14 “ ‘Usimvunjie heshima ndugu wa baba yako, kwa kukutana kimwili na mke wake; yeye ni shangazi yako.
15 “ ‘Usikutane kimwili na mkwe wako, yeye ni mke wa mwanao; usiwe na mahusiano kama hayo naye.
16 “ ‘Usikutane kimwili na mke wa kaka yako; utamvunjia heshima kaka yako.
17 “ ‘Usikutane kimwili na mwanamke kisha na binti yake. Usikutane kimwili na binti wa mwanawe au binti wa binti yake; hao ni ndugu zake wa karibu. Huo ni uovu.
18 “ ‘Usimchukue dada wa mke wako kuwa mke mwenza, na kukutana naye kimwili wakati bado mke wako anaishi.
19 “ ‘Usimsogelee mwanamke ili kukutana naye kimwili wakati wa unajisi wa siku zake za mwezi.
20 “ ‘Usikutane kimwili na mke wa jirani yako na kujitia naye unajisi.
21 “ ‘Usimtoe mtoto wako yeyote awe kafara kwa mungu Moleki, kwani hutalinajisi kamwe jina la Mungu wako. Mimi ndimi Bwana.
22 “ ‘Usikutane kimwili na mwanaume kama mtu akutanaye na mwanamke; hilo ni chukizo.
23 “ ‘Usikutane kimwili na mnyama na kujitia unajisi kwake. Mwanamke asijipeleke kwa mnyama ili kukutana naye kimwili; huo ni upotovu.
24 “ ‘Msijitie unajisi kwa njia yoyote katika hizi, kwa sababu hivi ndivyo mataifa nitakayoyafukuza mbele yenu yalivyojitia unajisi. 25 Hata nchi ilitiwa unajisi, hivyo nikaiadhibu kwa dhambi zake, nayo nchi ikawatapika wakazi wake. 26 Lakini ni lazima uzitunze amri zangu na sheria zangu. Mzawa na wageni waishio miongoni mwenu kamwe wasifanye mambo yoyote ya machukizo haya, 27 kwa kuwa mambo haya yote yalifanywa na watu walioishi katika nchi hii kabla yenu, na nchi ikawa najisi. 28 Kama mkiinajisi nchi, itawatapika kama ilivyowatapika mataifa yaliyowatangulia.
29 “ ‘Kila mtu atakayefanya mojawapo ya machukizo haya, watu hao ni lazima wakatiliwe mbali na watu wao. 30 Shikeni maagizo yangu, wala msifuate desturi za machukizo yoyote yaliyofanywa kabla hamjafika katika nchi hii, na kujitia unajisi kwa hayo. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.’ ”