Maria Aimba Magnificat

Nchi ya milima ya Uyahudi

7 au 6 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Luka 1:46–56

1:46 Naye Maria akasema:

“Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,

47 nayo roho yangu inamfurahia

Mungu Mwokozi wangu,

48 kwa kuwa ameangalia kwa fadhili

unyonge wa mtumishi wake.

Hakika tangu sasa vizazi vyote vitaniita aliyebarikiwa,

49 kwa maana yeye Mwenye Nguvu

amenitendea mambo ya ajabu:

jina lake ni takatifu.

50 Rehema zake huwaendea wale wamchao,

kutoka kizazi hadi kizazi.

51 Kwa kuwa ametenda mambo ya ajabu kwa mkono wake;

amewatawanya wale wenye kiburi

ndani ya mioyo yao.

52 Amewashusha watawala toka kwenye viti vyao vya enzi,

lakini amewainua wanyenyekevu.

53 Amewashibisha wenye njaa kwa vitu vizuri,

bali matajiri amewafukuza mikono mitupu.

54 Amemsaidia mtumishi wake Israeli,

kwa kukumbuka ahadi yake ya kumrehemu

55 Abrahamu na uzao wake milele,

kama alivyowaahidi baba zetu.”

56 Maria akakaa na Elizabeti karibu miezi mitatu, kisha akarudi nyumbani kwake.

Kuzaliwa, Utoto, na Maisha ya Yohana Jangwani

Kuzaliwa na utoto wa Yohana Mbatizaji, na maisha yake jangwani.

Milima ya Uyahudi. 7 au 6 KK

Luka 1:57–80

1:57 Ulipowadia wakati wa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto mwanaume. 58 Majirani zake na jamii zake wakasikia jinsi Bwana alivyomfanyia rehema kuu, nao wakafurahi pamoja naye.

59 Siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto, wakataka yule mtoto aitwe Zekaria, ambalo ndilo jina la baba yake. 60 Lakini mama yake akakataa na kusema, “Hapana! Jina lake ataitwa Yohana.”

61 Wakamwambia, “Hakuna mtu yeyote katika jamaa yako mwenye jina kama hilo.”

62 Basi wakamfanyia Zekaria baba yake ishara ili kujua kwamba yeye angependa kumpa mtoto jina gani. 63 Akaomba wampe kibao cha kuandikia na kwa mshangao wa kila mtu akaandika: “Jina lake ni Yohana.” 64 Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake ukaachiwa, akawa anaongea akimsifu Mungu. 65 Majirani wote wakajawa na hofu ya Mungu, na katika nchi yote ya vilima vya Uyahudi watu walikuwa wakinena juu ya mambo haya yote. 66 Kila aliyesikia habari hizi alishangaa akauliza, “Je, mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.

67 Zekaria, baba yake, akajazwa na Roho Mtakatifu, naye akatoa unabii, akisema:

68 “Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli,

kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa.

69 Naye ametusimamishia pembe ya wokovu

katika nyumba ya Daudi mtumishi wake,

70 kama alivyonena kwa vinywa vya manabii

wake watakatifu tangu zamani,

71 kwamba atatuokoa kutoka kwa adui zetu,

na kutoka mikononi mwao wote watuchukiao:

72 ili kuonyesha rehema kwa baba zetu

na kukumbuka Agano lake takatifu,

73 kiapo alichomwapia baba yetu Abrahamu:

74 kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu,

tupate kumtumikia yeye pasipo hofu

75 katika utakatifu na haki mbele zake,

siku zetu zote.

76 “Nawe mtoto wangu, utaitwa nabii wa Aliye Juu Sana;

kwa kuwa utamtangulia Bwana

na kuandaa njia kwa ajili yake,

77 kuwajulisha watu wake juu ya wokovu

utakaopatikana kwa kusamehewa dhambi zao,

78 kwa ajili ya wingi wa rehema za Mungu wetu,

nuru itokayo juu itatuzukia

79 ili kuwaangazia wale waishio gizani

na katika uvuli wa mauti,

kuiongoza miguu yetu katika njia ya amani.”

80 Yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu katika roho; akaishi nyikani hadi siku ile alipojionyesha hadharani kwa Waisraeli.