Sheria za Dhabihu (continued)

1490 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Walawi 5–6

1 “ ‘Ikiwa mtu atakuwa ametenda dhambi kwa sababu hakusema alipotakiwa kutoa ushahidi hadharani kuhusu jambo aliloona au kujua habari zake, yeye anastahili adhabu.

2 “ ‘Au kama mtu akigusa kitu chochote ambacho ni najisi, iwe ni mizoga ya wanyama pori walio najisi, au ya wanyama wafugwao walio najisi, au ya viumbe vitambaavyo ardhini, hata akiwa hana habari, amekuwa najisi na mwenye hatia.

3 “ ‘Au kama akigusa kitu kilicho kichafu kinachotokana na binadamu, kitu chochote kile kinachoweza kumfanya awe najisi, hata akiwa hana habari, atakapofahamu atakuwa na hatia.

4 “ ‘Au kama mtu ameapa kufanya kitu chochote bila kufikiri, kiwe chema au kibaya, kwa vyovyote mtu aweza kuapa bila kujali, hata akiwa hana habari, atakapofahamu atakuwa na hatia.

5 “ ‘Wakati mtu yeyote atakapokuwa na hatia katika mojawapo ya haya, lazima akiri ni kwa njia gani ametenda dhambi, 6 na kama adhabu ya dhambi aliyoitenda, lazima alete kwa Bwana kondoo jike au mbuzi jike kutoka kwenye kundi lake kama sadaka ya dhambi; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi yake.

7 “ ‘Lakini huyo mtu kama hataweza kumtoa mwana-kondoo, ataleta hua wawili au makinda mawili ya njiwa kwa Bwana kuwa adhabu kwa ajili ya dhambi yake, mmoja wa hao ndege kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na wa pili kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. 8 Atawaleta kwa kuhani, ambaye atamtoa kwanza ndege mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Atamvunja shingo na kuacha kichwa chake kikiningʼinia, 9 naye atanyunyiza sehemu ya hiyo damu ya sadaka ya dhambi kwenye pembe za madhabahu. Damu iliyobaki lazima ichuruzwe chini ya madhabahu. Hii ni sadaka ya dhambi. 10 Kisha kuhani atamtoa yule ndege wa pili kama sadaka ya kuteketezwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa, na hivyo kufanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi aliyoitenda, naye atasamehewa.

11 “ ‘Ikiwa basi, hawezi kupata hua wawili au makinda mawili ya njiwa, ataleta sehemu ya kumi ya efa ya unga laini kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Kamwe asiweke mafuta wala uvumba juu yake, kwa sababu ni sadaka ya dhambi. 12 Atauleta unga kwa kuhani, ambaye atachukua konzi moja kama sehemu ya kumbukumbu na atauteketeza kwenye madhabahu juu ya sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto. Hii ni sadaka ya dhambi. 13 Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi yoyote ya hizo alizotenda, naye atasamehewa. Sadaka iliyobaki itakuwa ya kuhani, kama ilivyokuwa ile sadaka ya nafaka.’ ”

14 Bwana akamwambia Mose: 15 “Mtu anapokiuka na kutenda dhambi pasipo kukusudia kuhusu mojawapo ya mambo matakatifu ya Bwana, huyo mtu ataleta kwa Bwana kama adhabu kondoo dume mmoja kutoka kundi lake, asiye na dosari na mwenye thamani halisi kifedha, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu. Hii ni sadaka ya hatia. 16 Ni lazima alipe kwa yale aliyoshindwa kufanya kuhusu vitu vitakatifu, kwa kuongeza sehemu ya tano ya thamani ile na kuitoa yote kwa kuhani, ambaye atamfanyia upatanisho kwa huyo kondoo dume kama sadaka ya dhambi, naye atasamehewa.

17 “Kama mtu akifanya dhambi na kufanya yale yaliyokatazwa katika mojawapo ya amri za Bwana, hata ikiwa hajui, yeye ana hatia na anastahili adhabu. 18 Atamletea kuhani kama sadaka ya hatia kondoo dume kutoka kundi lake, kondoo asiye na dosari na mwenye thamani halisi kifedha. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa kosa alilotenda bila kukusudia, naye atasamehewa. 19 Hii ni sadaka ya hatia; amekuwa na hatia kwa kufanya kosa dhidi ya Bwana.”

6:1 Bwana akamwambia Mose: 2 “Kama mtu yeyote akitenda dhambi, naye si mwaminifu kwa Bwana kwa kumdanganya jirani yake kuhusu kitu fulani alichokabidhiwa, au kimeachwa chini ya utunzaji wake, au kimeibwa, au kama akimdanganya, 3 au akiokota mali iliyopotea na akadanganya, au kuapa kwa uongo, au kama akitenda dhambi yoyote ambayo watu waweza kuitenda; 4 wakati akitenda dhambi hizo na kuwa mwenye hatia, ni lazima arudishe kile alichokuwa amekiiba au amekichukua kwa dhuluma, au alichokuwa amekabidhiwa, au mali iliyokuwa imepotea akaipata, 5 au chochote alichokuwa amekiapia kwa uongo. Lazima akirudishe kikamilifu, na aongeze sehemu ya tano ya thamani yake, vyote ampe mwenye mali siku ile anapeleka sadaka yake ya hatia. 6 Kisha kama adhabu lazima amletee kuhani, yaani kwa Bwana, kama sadaka yake ya hatia, kondoo dume asiye na dosari na mwenye thamani kamili kutoka kundi lake. 7 Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana, naye atasamehewa kwa kosa lolote katika mambo hayo aliyoyatenda yaliyomfanya kuwa na hatia.”

8 Bwana akamwambia Mose: 9 “Mpe Aroni na wanawe agizo hili: ‘Haya ndiyo masharti kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa: Sadaka ya kuteketezwa itabaki kwenye moto juu ya madhabahu usiku kucha, mpaka asubuhi, nao moto lazima uwe unaendelea kuwaka juu ya madhabahu. 10 Kisha kuhani atavaa mavazi yake ya kitani, pamoja na nguo za ndani za kitani mwilini wake, na aondoe majivu ya sadaka ya kuteketezwa ambayo moto umeteketeza juu ya madhabahu, na kuyaweka kando ya madhabahu. 11 Kisha atayavua mavazi haya na kuvaa mengine, naye achukue yale majivu nje ya kambi na kuyapeleka mahali palipo safi kwa kawaida ya ibada. 12 Moto ulio juu ya madhabahu lazima uwe unaendelea kuwaka, kamwe usizimike. Kila asubuhi kuhani ataongeza kuni na kupanga sadaka ya kuteketezwa juu ya moto, na kuteketeza mafuta ya sadaka za amani juu yake. 13 Moto lazima uendelee kuwaka juu ya madhabahu mfululizo, kamwe usizimike.

14 “ ‘Haya ndiyo masharti ya sadaka ya nafaka: Wana wa Aroni wataileta mbele za Bwana, mbele za madhabahu. 15 Kuhani atachukua konzi ya unga laini na mafuta, pamoja na uvumba wote ulioko juu ya sadaka ya nafaka, ateketeze sehemu ya kumbukumbu juu ya madhabahu kama harufu nzuri ya kumpendeza Bwana. 16 Aroni na wanawe watakula sehemu iliyobaki, lakini italiwa bila kutiwa chachu mahali patakatifu, nao wataila kwenye ua wa Hema la Kukutania. 17 Kamwe haitaokwa na chachu; nimewapa kama fungu lao la sadaka iliyotolewa kwangu kwa moto. Ni takatifu sana, kama vile ilivyo sadaka ya dhambi na ya hatia. 18 Kila mwanaume mzao wa Aroni aweza kuila. Ni fungu lake la kawaida la sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto kwa vizazi vijavyo. Chochote kinachozigusa kitakuwa kitakatifu.’ ”

19 Tena Bwana akamwambia Mose, 20 “Hii ni sadaka ambayo Aroni na wanawe wanapaswa kuleta kwa Bwana siku atakapotiwa mafuta: sehemu ya kumi ya efa ya unga laini kama sadaka ya kawaida ya nafaka. Nusu yake ataitoa asubuhi na nusu nyingine jioni. 21 Iandae kwa mafuta kwenye kikaango; ilete ikiwa imechanganywa vizuri, na utoe hiyo sadaka ya nafaka ikiwa imevunjwa vipande vipande kuwa harufu nzuri ya kumpendeza Bwana. 22 Mwanawe atakayeingia mahali pake kama kuhani aliyetiwa mafuta ndiye atakayeiandaa. Ni fungu la kawaida la Bwana, nalo litateketezwa kabisa. 23 Kila sadaka ya nafaka ya kuhani itateketezwa kabisa; kamwe haitaliwa.”

24 Bwana akamwambia Mose, 25 “Mwambie Aroni na wanawe: ‘Haya ndiyo masharti kwa ajili ya sadaka ya dhambi: Sadaka ya dhambi itachinjiwa mbele za Bwana mahali sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa, ni takatifu sana. 26 Kuhani anayeitoa ndiye atakayeikula; itakuliwa katika mahali patakatifu, katika ua wa Hema la Kukutania. 27 Chochote kitakachogusa nyama yoyote ya hiyo sadaka kitakuwa kitakatifu, na kama hiyo damu itadondokea juu ya vazi, lazima uifulie mahali patakatifu. 28 Chungu cha udongo kitakachopikiwa nyama lazima kivunjwe, lakini kama imepikiwa kwenye chombo cha shaba, chombo hicho kitasuguliwa na kusuuzwa kwa maji. 29 Kila mwanaume katika familia ya kuhani aweza kula nyama hiyo; ni takatifu sana. 30 Lakini kila sadaka ya dhambi ambayo damu yake imeletwa ndani ya Hema la Kukutania kufanya upatanisho katika Mahali Patakatifu kamwe haitaliwa; lazima iteketezwe.