Kipindi cha 2: Tangu kutawanyika ulimwenguni hadi Kutoka

Sehemu ya 1: Lugha Zinavurugwa na Wanadamu Wanatawanywa

Mnara wa Babeli

2234 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mwanzo 11:1–9

1 Wakati huo dunia yote ilikuwa na lugha moja na msemo mmoja. 2 Watu walipoelekea upande wa mashariki, wakafika kwenye tambarare katika nchi ya Shinari nao wakaishi huko.

3 Wakasemezana wao kwa wao, “Njooni, tufyatue matofali na tuyachome vizuri kwa moto.” Walitumia matofali badala ya mawe, na lami kwa ajili ya kushikamanishia hayo matofali. 4 Ndipo wakasema, “Njooni, tujijengee mji wenye mnara ambao utafika hadi mbinguni, ili tujipatie jina tusije tukatawanyika usoni pa dunia yote.”

5 Lakini Bwana akashuka ili auone mji na mnara ambao wanadamu waliokuwa wanaujenga. 6 Bwana akasema, “Ikiwa kama taifa moja wanaozungumza lugha moja wameanza kufanya hili, basi hakuna lolote watakalopanga kufanya ambalo halitawezekana kwao. 7 Njooni, tushuke tuvuruge lugha yao ili wasielewane wao kwa wao.”

8 Hivyo Bwana akawatawanya kutoka mahali pale kwenda katika dunia yote, nao wakaacha kuujenga huo mji. 9 Ndiyo maana pakaitwa Babeli, kwa sababu hapo ndipo Bwana alipoivuruga lugha ya dunia nzima. Kutoka hapo Bwana akawatawanya katika uso wa dunia yote.

Orodha ya Mataifa

Mwanzo 10

1 Hawa ndio wazao wa Noa: Shemu, Hamu na Yafethi, ambao walizaa wana baada ya gharika.

2 Wana wa Yafethi walikuwa:

Gomeri, Magogu, Madai, Yavani, Tubali, Mesheki na Tirasi.

3 Wana wa Gomeri walikuwa:

Ashkenazi, Rifathi na Togarma.

4 Wana wa Yavani walikuwa:

Elisha, Tarshishi, Kitimu na Rodanimu. 5 (Kutokana na hawa mataifa ya Pwani yalienea katika nchi zao, kwa koo zao katika mataifa yao, kila moja kwa lugha yake.)

6 Wana wa Hamu walikuwa:

Kushi, Misraimu, Putu na Kanaani.

7 Wana wa Kushi walikuwa:

Seba, Havila, Sabta, Raama na Sabteka.

Wana wa Raama walikuwa:

Sheba na Dedani.

8 Kushi akamzaa Nimrodi, ambaye alikua akawa mtu shujaa duniani. 9 Alikuwa mwindaji hodari mbele za Bwana. Ndiyo sababu watu husema, “Kama Nimrodi, hodari wa kuwinda mbele za Bwana.” 10 Vituo vyake vya kwanza katika ufalme wake vilikuwa Babeli, Ereki, Akadi na Kalne katika Shinari. 11 Kutoka nchi ile alikwenda Ashuru, ambako alijenga Ninawi, Rehoboth-iri, Kala, 12 na Reseni, iliyo kati ya Ninawi na Kala; huo ndio mji mkubwa.

13 Misraimu alikuwa baba wa:

Waludi, Waanami, Walehabi, Wanaftuhi, 14 Wapathrusi, Wakasluhi (hao ndio asili ya Wafilisti), na Wakaftori.

15 Kanaani alikuwa baba wa:

Sidoni mzaliwa wake wa kwanza, Hethi, 16 Wayebusi, Waamori, Wagirgashi, 17 Wahivi, Waariki, Wasini, 18 Waarvadi, Wasemari na Wahamathi.

Baadaye koo za Wakanaani zilitawanyika, 19 na mipaka ya Kanaani ilienea kutoka Sidoni kuelekea Gerari hadi Gaza, kisha kuelekea Sodoma, Gomora, Adma na Seboimu, hadi kufikia Lasha.

20 Hawa ni wana wa Hamu kwa koo zao na lugha zao, katika nchi zao na mataifa yao.

21 Shemu ambaye ni ndugu mkubwa wa Yafethi, kwake kulizaliwa wana pia. Shemu alikuwa baba wa wana wote wa Eberi.

22 Wana wa Shemu walikuwa:

Elamu, Ashuru, Arfaksadi, Ludi na Aramu.

23 Wana wa Aramu walikuwa:

Usi, Huli, Getheri na Mesheki.

24 Arfaksadi alikuwa baba wa Shela,

naye Shela akamzaa Eberi.

25 Eberi akapata wana wawili:

Mmoja wao aliitwa Pelegi, kwa kuwa wakati wake ndipo dunia iligawanyika; nduguye aliitwa Yoktani.

26 Yoktani alikuwa baba wa:

Almodadi, Shelefu, Hasarmawethi, Yera, 27 Hadoramu, Uzali, Dikla, 28 Obali, Abimaeli, Sheba, 29 Ofiri, Havila na Yobabu. Hawa wote walikuwa wana wa Yoktani.

30 Nchi waliyoishi ilienea toka Mesha kuelekea Sefari kwenye nchi ya vilima iliyoko mashariki.

31 Hao ndio wana wa Shemu kwa koo zao na lugha zao, katika nchi zao na mataifa yao.

32 Hizi ndizo koo za wana wa Noa, kufuatana na vizazi vyao, katika mataifa yao. Kutokana na hawa mataifa yalienea duniani kote baada ya gharika.

Nasaba ya Shemu 2348 KK

Mwanzo 11:10–26

10 Hivi ndivyo vizazi vya Shemu.

Miaka miwili baada ya gharika, Shemu alipokuwa na miaka 100, akamzaa Arfaksadi. 11 Baada ya kumzaa Arfaksadi, Shemu aliishi miaka 500, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.

12 Wakati Arfaksadi alipokuwa na miaka thelathini na mitano, akamzaa Shela. 13 Baada ya Arfaksadi kumzaa Shela, aliishi miaka 403, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.

14 Shela alipokuwa na miaka thelathini, akamzaa Eberi. 15 Shela baada ya kumzaa Eberi, aliishi miaka 403, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.

16 Eberi alipokuwa na miaka thelathini na minne, akamzaa Pelegi. 17 Baada ya Eberi kumzaa Pelegi, aliishi miaka 430, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.

18 Pelegi alipokuwa na miaka thelathini, akamzaa Reu. 19 Baada ya Pelegi kumzaa Reu, aliishi miaka 209, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.

20 Reu alipokuwa na miaka thelathini na miwili, akamzaa Serugi. 21 Baada ya Reu kumzaa Serugi, aliishi miaka 207, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.

22 Serugi alipokuwa na miaka thelathini, akamzaa Nahori. 23 Baada ya Serugi kumzaa Nahori, aliishi miaka 200, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.

24 Nahori alipokuwa na miaka ishirini na tisa, akamzaa Tera. 25 Baada ya Nahori kumzaa Tera, aliishi miaka 119, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.

26 Tera alipokuwa na miaka sabini, akamzaa Abramu, Nahori na Harani.