Ukiwa na Kurejea kwa Hali Nzuri ya Uyahudi Vyatabiriwa

Unabii wa jumla kuhusu ukiwa na kurejea kwa hali nzuri ya Uyahudi.

714 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Isaya 24–25

1 Tazama, Bwana ataifanya dunia kuwa ukiwa

na kuiharibu,

naye atauharibu uso wake

na kutawanya wakaao ndani yake:

2 ndivyo itakavyokuwa

kwa makuhani na kwa watu,

kwa bwana na kwa mtumishi,

kwa bibi na kwa mtumishi wake wa kike,

kwa muuzaji na kwa mnunuzi,

kwa mkopaji na kwa mkopeshaji,

kwa mdaiwa na kwa mdai.

3 Dunia itaharibiwa kabisa

na kutekwa nyara kabisa.

Bwana amesema neno hili.

4 Dunia inakauka na kunyauka,

dunia inanyongʼonyea na kunyauka,

waliotukuzwa wa dunia wananyongʼonyea.

5 Dunia imetiwa unajisi na watu wake;

wameacha kutii sheria,

wamevunja amri

na kuvunja agano la milele.

6 Kwa hiyo laana inaiteketeza dunia,

watu wake lazima waichukue hatia yao.

Kwa hiyo wakazi wa dunia wameteketezwa,

nao waliosalia ni wachache sana.

7 Divai mpya inakauka na mzabibu unanyauka,

watu wote wafurahishao wanalia kwa huzuni.

8 Furaha ya matoazi imekoma,

kelele za wenye furaha zimekoma,

shangwe za kinubi zimenyamaza.

9 Hawanywi tena mvinyo pamoja na wimbo,

kileo ni kichungu kwa wanywaji wake.

10 Mji ulioharibiwa umekuwa ukiwa,

mlango wa kila nyumba umefungwa.

11 Barabarani wanalilia kupata mvinyo,

furaha yote imegeuka kuwa majonzi,

furaha yote imefukuziwa mbali na dunia.

12 Mji umeachwa katika uharibifu,

lango lake limevunjwa vipande.

13 Ndivyo itakavyokuwa duniani

na miongoni mwa mataifa,

kama vile wakati mzeituni upigwavyo,

au kama vile wakati masazo yabakiavyo baada ya zabibu kuvunwa.

14 Wanainua sauti zao, wanapiga kelele kwa furaha,

kutoka magharibi wanasifu kwa ukelele utukufu wa Bwana.

15 Kwa hiyo upande wa mashariki mpeni Bwana utukufu,

liadhimisheni jina la Bwana, Mungu wa Israeli,

katika visiwa vya bahari.

16 Kutoka miisho ya dunia tunasikia uimbaji:

“Utukufu kwa Yule Mwenye Haki.”

Lakini nilisema, “Ninadhoofika, ninadhoofika!

Ole wangu!

Watenda hila wanasaliti!

Kwa hila watenda hila wanasaliti!”

17 Hofu, shimo na mtego vinakungojea,

ewe mtu ukaaye duniani.

18 Kila akimbiaye asikiapo sauti ya hofu

atatumbukia shimoni,

naye yeyote apandaye kutoka shimoni,

atanaswa kwenye mtego.

Malango ya gharika ya mbinguni yamefunguliwa,

misingi ya dunia inatikisika.

19 Dunia imepasuka,

dunia imechanika,

dunia imetikiswa kabisa.

20 Dunia inapepesuka kama mlevi,

inayumbayumba kama kibanda kwenye upepo;

imelemewa sana na mzigo wa hatia ya uasi wake

na ikianguka kamwe haitainuka tena.

21 Katika siku ile Bwana ataadhibu

nguvu zilizoko mbinguni juu,

na wafalme walioko duniani chini.

22 Watakusanywa pamoja

kama wafungwa waliofungwa gerezani,

watafungiwa gerezani

na kuadhibiwa baada ya siku nyingi.

23 Mwezi utatiwa haya, nalo jua litaaibishwa;

kwa maana Bwana Mwenye Nguvu Zote atawala

juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu,

tena mbele ya wazee wake kwa utukufu.

25:1 Ee Bwana, wewe ni Mungu wangu,

nitakutukuza na kulisifu jina lako,

kwa maana katika ukamilifu wa uaminifu

umetenda mambo ya ajabu,

mambo yaliyokusudiwa tangu zamani.

2 Umeufanya mji kuwa lundo la kifusi,

mji wenye ngome kuwa magofu,

ngome imara ya wageni kuwa si mji tena,

wala hautajengwa tena kamwe.

3 Kwa hiyo mataifa yenye nguvu yatakuheshimu,

miji ya mataifa katili itakuheshimu wewe.

4 Umekuwa kimbilio la watu maskini,

kimbilio la mhitaji katika taabu yake,

hifadhi wakati wa dhoruba

na kivuli wakati wa hari.

Kwa maana pumzi ya wakatili

ni kama dhoruba ipigayo ukuta

5 na kama joto la jangwani.

Wewe wanyamazisha makelele ya wageni;

kama vile hari ipunguzwavyo na kivuli cha wingu,

ndivyo wimbo wa wakatili unyamazishwavyo.

6 Juu ya mlima huu Bwana Mwenye Nguvu Zote ataandaa

karamu ya vinono kwa mataifa yote,

karamu ya mvinyo wa zamani,

nyama nzuri sana na divai zilizo bora sana.

7 Juu ya mlima huu ataharibu

sitara ihifadhiyo mataifa yote,

kile kifuniko kifunikacho mataifa yote,

8 yeye atameza mauti milele.

Bwana Mwenyezi atafuta machozi katika nyuso zote;

ataondoa aibu ya watu wake duniani kote.

Bwana amesema hili.

9 Katika siku ile watasema,

“Hakika huyu ndiye Mungu wetu;

tulimtumaini, naye akatuokoa.

Huyu ndiye Bwana, tuliyemtumaini;

sisi tushangilie na kufurahia katika wokovu wake.”

10 Mkono wa Bwana utatulia juu ya mlima huu,

bali Moabu atakanyagwa chini

kama majani makavu yakanyagwavyo kwenye shimo la mbolea.

11 Watakunjua mikono yao katikati yake,

kama vile mwogeleaji akunjuavyo mikono yake ili aogelee.

Mungu atashusha kiburi chao

licha ya ujanja wa mikono yao.

12 Atabomoa kuta ndefu za maboma yako

na kuziangusha chini,

atazishusha chini ardhini,

mpaka mavumbini kabisa.