Sehemu ya 3: Mawaidha ya Mwisho na Kifo cha Yoshua
1443 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
43 Kwa hiyo Bwana akawapa Israeli nchi yote aliyokuwa ameapa kuwapa baba zao, nao wakaimiliki na kukaa humo. 44 Bwana akawapa pumziko kila upande, kama vile alivyokuwa amewaapia baba zao, hakuna hata mmoja wa adui zao aliyeweza kusimama mbele yao, Bwana akawatia adui zao wote mikononi mwao. 45 Hakuna hata mojawapo ya ahadi nzuri ya Bwana kwa nyumba ya Israeli ambayo haikutimia; kila moja ilitimia.
1 Baada ya muda mrefu kupita, naye Bwana akawa amewapa Israeli pumziko mbele ya adui zao wote waliowazunguka, Yoshua, wakati huo akiwa mzee na umri ukiwa umeendelea sana, 2 akawaita Israeli wote, wazee wao, viongozi, waamuzi na maafisa Yoshua akawaambia: “Mimi ni mzee na umri wangu umeendelea sana. 3 Ninyi wenyewe mmeona kila kitu Bwana Mungu wenu, alichowatendea mataifa haya yote kwa ajili yenu. Ilikuwa ni Bwana Mungu wenu aliyewapigania. 4 Kumbukeni jinsi nilivyowagawia kama urithi kwa makabila yenu yote nchi ya mataifa yaliyobaki, yaani mataifa niliyowashinda, kati ya Mto Yordani na Bahari kuu upande wa magharibi. 5 Bwana Mungu wenu mwenyewe atawaondoa watoke mbele yenu. Atawafukuza mbele yenu, nanyi mtamiliki nchi yao, kama vile Bwana Mungu wenu alivyowaahidi.
6 “Kuweni hodari sana, kuweni waangalifu kutii yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Sheria ya Mose, pasipo kugeuka upande wa kuume au kushoto. 7 Msishirikiane na mataifa yaliyobakia katikati yenu, wala msiombe kwa majina ya miungu yao au kuapa kwayo. Msiitumikie wala kuisujudia. 8 Bali mtashikamana kwa uthabiti na Bwana, Mungu wenu, kama vile ambavyo mmefanya mpaka sasa.
9 “Bwana amewafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu, mpaka siku ya leo hakuna yeyote aliyeweza kusimama mbele yenu. 10 Mtu mmoja miongoni mwenu anafukuza watu elfu, kwa kuwa Bwana Mungu wenu anawapigania, kama alivyoahidi. 11 Kwa hiyo kuweni waangalifu sana kumpenda Bwana Mungu wenu.
12 “Lakini ikiwa mtageuka na kushikamana na mabaki ya mataifa haya yaliyosalia katikati yenu na kama mtaoana na kushirikiana nao, 13 basi mwe na hakika kuwa Bwana Mungu wenu hatawafukuza tena mataifa hayo mbele yenu. Badala yake, watakuwa tanzi na mitego kwenu, mijeledi migongoni mwenu, na miiba machoni mwenu, mpaka mwangamie kutoka nchi hii nzuri, ambayo Bwana Mungu wenu amewapa.
14 “Sasa mimi ninakaribia kwenda katika njia ya watu wote wa dunia. Mnajua kwa mioyo yenu na roho zenu kwamba hakuna ahadi zozote njema Bwana Mungu wenu alizowaahidia, ambazo hazikutimia. Kila ahadi imetimizwa, hakuna hata moja ambayo haikutimia. 15 Lakini kama vile kila ahadi njema ya Bwana Mungu wenu imekuwa kweli, vivyo hivyo Bwana ataleta maovu yote kama alivyo onya, mpaka awe amewaangamiza kutoka nchi hii nzuri aliyowapa. 16 Kama mkilivunja agano la Bwana Mungu wenu, ambalo aliwaamuru ninyi, mkaenda na kuitumikia miungu mingine na kuisujudia, hasira ya Bwana itawaka dhidi yenu, nanyi mtaangamia kutoka nchi nzuri aliyowapa ninyi.”
24:1 Ndipo Yoshua akaita pamoja makabila yote ya Israeli huko Shekemu. Akawaita wazee, viongozi, waamuzi na maafisa wa Israeli, nao wakaja mbele za Mungu.
2 Yoshua akawaambia watu wote, “Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Hapo zamani baba zenu, pamoja na Tera baba yake Abrahamu na Nahori, waliishi ngʼambo ya Mto nao waliiabudu miungu mingine. 3 Lakini nilimwondoa baba yenu Abrahamu kutoka nchi hiyo ngʼambo ya Mto, nami nikamwongoza katika nchi yote ya Kanaani, nikampa wazao wengi. Nikampa Isaki, 4 naye Isaki nikampa Yakobo na Esau. Esau nikampa nchi ya vilima ya Seiri, lakini Yakobo pamoja na wanawe wakashuka Misri.
5 “ ‘Kisha nikawatuma Mose na Aroni, nami nikawapiga Wamisri kwa kile nilichokitenda huko, tena nikawatoa ninyi huko. 6 Nilipowatoa baba zenu Misri, mlifika kwenye bahari, nao Wamisri wakawafuatia baba zenu kwa magari na wapanda farasi mpaka kwenye Bahari ya Shamu. 7 Lakini wakamlilia Bwana wakitaka msaada, naye akaweka giza kati yenu na Wamisri, akaileta bahari juu yao ikawafunika. Ninyi mliona kwa macho yenu wenyewe kile nilichowatendea Wamisri. Kisha mliishi jangwani kwa muda mrefu.
8 “ ‘Nikawaleta katika nchi ya Waamori ambao waliishi mashariki mwa Yordani. Wakapigana nanyi, lakini nikawatia mikononi mwenu. Nikawaangamiza mbele yenu nanyi mkaimiliki nchi yao. 9 Wakati Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, alipojiandaa kupigana dhidi ya Israeli, alimwita Balaamu mwana wa Beori apate kuwalaani. 10 Lakini sikumkubali Balaamu, kwa hiyo aliwabariki tena na tena, nami niliwaokoa toka mkononi mwake.
11 “ ‘Ndipo mlipovuka Yordani mkafika Yeriko. Raiya wa Yeriko wakapigana nanyi, kama walivyofanya Waamori, Waperizi, Wakanaani, Wahiti, Wagirgashi, Wahivi na Wayebusi, lakini niliwatia mikononi mwenu. 12 Nikatuma manyigu mbele yenu, ambao pia waliwafukuza mbele yenu, hao wafalme wawili wa Waamori. Siyo upanga au upinde wenu wenyewe vilivyowapatia ushindi. 13 Hivyo nikawapa ninyi nchi ambayo hamkuitaabikia na miji ambayo hamkuijenga na mnaishi ndani yake na kula toka kwa mashamba ya mizabibu na mizeituni msiyoipanda.’
14 “Sasa basi mcheni Bwana na kumtumikia kwa uaminifu wote. Itupeni mbali miungu ambayo baba zenu waliiabudu huko ngʼambo ya Mto Frati na huko Misri, nanyi mtumikieni Bwana. 15 Lakini msipoona vyema kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia, kama ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ngʼambo Frati, au miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Bwana.”
16 Ndipo hao watu wakajibu, “Hili jambo liwe mbali nasi la kumsahau Bwana na kuitumikia miungu mingine! 17 Bwana Mungu wetu mwenyewe ndiye alitutoa sisi na baba zetu akatupandisha kutoka Misri, kutoka nchi ile ya utumwa, na kutenda zile ishara kubwa mbele ya macho yetu. Ndiye aliyetulinda katika safari yetu yote na kutokana na mataifa yote ambayo tulipita katikati yao. 18 Bwana akayafukuza mbele yetu mataifa yote pamoja na Waamori, walioishi katika nchi hii. Hivyo sisi nasi tutamtumikia Bwana kwa kuwa yeye ndiye Mungu wetu.”
19 Yoshua akawaambia watu, “Hamwezi kumtumikia Bwana. Yeye ni Mungu Mtakatifu, ni Mungu mwenye wivu. Hatasamehe uasi wenu na dhambi zenu. 20 Ikiwa mkimwacha Bwana na kuitumikia miungu migeni, atageuka na kuwaleteeni maafa na kuwaangamiza, baada ya kuwa mwema kwenu.”
21 Lakini watu wakamwambia Yoshua, “Sivyo! Sisi tutamtumikia Bwana.”
22 Ndipo Yoshua akawaambia, “Ninyi mmekuwa mashahidi juu yenu wenyewe kuwa mmechagua kumtumikia Bwana.”
Nao wakajibu, “Ndiyo, tu mashahidi.”
23 Yoshua akawaambia, “Sasa basi, itupeni mbali hiyo miungu migeni iliyo katikati yenu, nanyi mtoleeni Bwana, Mungu wa Israeli, mioyo yenu.”
24 Nao watu wakamwambia Yoshua, “Tutamtumikia Bwana Mungu wetu na kumtii yeye.”
25 Siku ile Yoshua akafanya agano kwa ajili ya watu na hapo Shekemu ndipo alipowaandikia amri na sheria. 26 Naye Yoshua akayaandika mambo haya katika Kitabu cha Sheria ya Mungu. Ndipo akalitwaa jiwe kubwa, akalisimamisha huko chini ya mwaloni, karibu na mahali patakatifu pa Bwana.
27 Yoshua akawaambia watu wote, “Angalieni! Jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu. Limesikia maneno yote Bwana aliyotuambia. Litakuwa shahidi juu yenu kama mtakuwa waongo kwa Mungu wenu.”
28 Basi Yoshua akawatuma watu kila mmoja aende katika urithi wake mwenyewe.
29 Baada ya mambo haya, Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana akafa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi. 30 Nao wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Sera katika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini ya Mlima wa Gaashi.
31 Israeli wakamtumikia Bwana siku zote za maisha ya Yoshua, na za hao wazee walioishi baada ya Yoshua kufa, ambao waliona kila kitu Bwana alichowatendea Israeli.
32 Nayo ile mifupa ya Yosefu, ambayo Waisraeli waliipandisha kutoka huko Misri, wakaizika huko Shekemu kwenye eneo, ambalo Yakobo alilinunua kwa wana wa Hamori baba yake Shekemu, kwa vipande mia vya fedha. Eneo hili likawa ni urithi wa uzao wa Yosefu.
33 Naye Eleazari mwana wa Aroni akafariki akazikwa huko Gibea, mlima aliokuwa amepewa mtoto wake Finehasi, kwenye nchi ya vilima ya Efraimu.