Mgao wa Yosefu

1444 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yoshua 16–17

1 Mgawanyo wa Yosefu ulianzia Yordani ya Yeriko, mashariki mwa miji ya Yeriko na kutoka hapo ulipanda kupitia jangwani na kuingia katika nchi ya vilima ya Betheli. 2 Ukaendelea kutoka Betheli (ndiyo Luzu), ukavuka kuingia eneo la Waariki huko Atarothi, 3 ukateremkia kuelekea magharibi hadi eneo la Wayafleti ukienea hadi eneo la Beth-Horoni ya Chini hadi Gezeri, ukiishia baharini.

4 Kwa hiyo Manase na Efraimu, wazao wa Yosefu, walipokea urithi wao.

5 Hili ndilo lilikuwa eneo la Efraimu, ukoo kwa ukoo:

Mpaka wa urithi wao ulianzia Ataroth-Adari upande wa mashariki hadi Beth-Horoni ya Juu, 6 na kuendelea mpaka baharini. Kutoka Mikmeta upande wa kaskazini ulipinda kuelekea mashariki hadi Taanath-Shilo, ukiupita hadi Yanoa upande wa mashariki. 7 Kisha uliteremka kutoka Yanoa hadi Atarothi na Naara, ukagusa Yeriko na kutokea katika Mto Yordani. 8 Kutoka Tapua mpaka ulikwenda magharibi hadi Bonde la Kana na kuishia baharini. Huu ulikuwa ndio urithi wa kabila la Waefraimu, ukoo kwa ukoo. 9 Pia ulijumuisha miji yote na vijiji vyake ambavyo vilitengwa kwa ajili ya Waefraimu ndani ya urithi wa kabila la Manase.

10 Hawakuwatoa Wakanaani waishio Gezeri; mpaka leo Wakanaani wanaishi miongoni mwa watu wa Efraimu lakini wanatakiwa kufanya kazi ngumu za kulazimishwa.

17:1 Huu ndio mgawo wa kabila la Manase kama mzaliwa wa kwanza wa Yosefu, yaani kwa ajili ya Makiri, mzaliwa wa kwanza wa Manase. Makiri alikuwa baba wa Wagileadi, ambao walipokea Gileadi na Bashani kwa sababu Wamakiri walikuwa askari wakuu. 2 Kwa hiyo mgawo huu ulikuwa kwa ajili ya watu wa Manase waliokuwa wamebaki, ambao ni koo za Abiezeri, Heleki, Asirieli, Shekemu, Heferi na Shemida. Hawa ndio wanaume wale wengine wa uzao wa Manase mwana wa Yosefu kwa koo zao.

3 Basi Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase hakuwa na wana waume ila mabinti tu, ambao majina yao yalikuwa Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirsa. 4 Wakamwendea kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi, wakasema: “Bwana alimwagiza Mose atupatie urithi miongoni mwa ndugu zetu.” Kwa hiyo Yoshua akawapa urithi pamoja na ndugu wa baba yao, kufuatana na agizo la Bwana. 5 Fungu la Manase lilikuwa na sehemu kumi za nchi, licha ya Gileadi na Bashani mashariki mwa Yordani, 6 kwa sababu wale binti za kabila la Manase walipokea urithi miongoni mwa wana wa kiume. Nchi ya Gileadi ilikuwa mali ya wazao wa Manase waliobaki.

7 Eneo la Manase lilienea kuanzia Asheri hadi Mikmeta mashariki mwa Shekemu. Mpaka ule ulielekea upande wa kusini kutoka pale kujumuisha watu walioishi En-Tapua. 8 (Nchi ya Tapua ilikuwa mali ya Manase, lakini Tapua yenyewe iliyo mpakani mwa nchi ya Manase ilikuwa ya Waefraimu.) 9 Kisha mpaka ule uliendelea kuelekea kusini hadi Bonde la Kana. Kulikuwepo miji ya Efraimu iliyokuwa miongoni mwa miji ya Manase, lakini mpaka wa Manase ulikuwa upande wa kaskazini wa lile bonde na kuishia kwenye bahari. 10 Nchi ya kusini ilikuwa ya Efraimu, na ile iliyokuwa upande wa kaskazini ilikuwa ya Manase. Eneo la Manase lilifika bahari na ikapakana na Asheri upande wa kaskazini, na Isakari upande wa mashariki.

11 Katika Isakari na Asheri Manase alikuwa na miji pia: Beth-Shani, Ibleamu na watu wa Dori, Endori, Taanaki na Megido, pamoja na vijiji vyote vinavyohusika na miji hiyo (ya tatu katika orodha ni Nafothi).

12 Lakini Wamanase hawakuweza kuimiliki miji hii, kwa kuwa Wakanaani walikazana kuishi katika maeneo hayo. 13 Hata hivyo, Waisraeli walivyoendelea kupata nguvu waliwatumikisha Wakanaani na kuwatia katika kazi za kulazimishwa, lakini hawakuwafukuza kabisa.

14 Watu wa Yosefu wakamwambia Yoshua, “Kwa nini umetupa sisi mgawo mmoja tu na sehemu moja tu kuwa urithi? Sisi tu watu wengi sana, na Bwana ametubariki kwa wingi.”

15 Yoshua akajibu, “Kama ninyi ni wengi sana, na kama nchi ya vilima ya Efraimu ni ndogo sana kwenu, pandeni msituni mkafyeke eneo kwa ajili yenu wenyewe huko kwenye nchi ya Waperizi na Warefai.”

16 Watu wa Yosefu wakajibu, “Hiyo nchi ya vilima haitutoshi, nao Wakanaani wote wanaoishi katika tambarare wanayo magari ya vita ya chuma, wote wa Beth-Shani na miji yake, na wale walio katika Bonde la Yezreeli.”

17 Lakini Yoshua akanena na nyumba ya Yosefu, yaani Efraimu na Manase: “Ninyi ni wengi sana na wenye nguvu sana. Hamtakuwa na mgawo mmoja tu, 18 bali pia nchi hii ya kilima yenye msitu. Ifyekeni, nayo mipaka yake itakuwa yenu umbali mtakaoweza kufika. Ingawa Wakanaani wana magari ya chuma, nao wana nguvu, mwaweza kuwafukuza humo.”

Maskani Inasimamishwa

Yoshua 18:1–10

1 Kusanyiko lote la Waisraeli likakusanyika huko Shilo na kusimamisha Hema la Kukutania. Nchi ikawa chini ya utawala wao, 2 lakini palikuwa bado makabila saba ya Israeli ambayo yalikuwa hayajapokea urithi wao.

3 Hivyo Yoshua akawaambia Waisraeli, “Je, mtasubiri hata lini ili kuingia kumiliki nchi ambayo Bwana, Mungu wa baba zenu, amewapa? 4 Chagueni watu watatu kutoka kwenye kila kabila. Nitawatuma hao watu kukagua hiyo nchi na kuniandikia mapendekezo ya mgawanyo wa urithi wa kila kabila. Nao watanirudia. 5 Mtaigawanya hiyo nchi katika sehemu saba. Yuda atabaki katika eneo lake upande wa kusini na nyumba ya Yosefu katika nchi yake upande wa kaskazini. 6 Baada ya kuandika maelezo ya hizo sehemu saba za nchi, yaleteni kwangu, nami nitawapigia kura kwa kura mbele za Bwana Mungu wetu. 7 Hata hivyo, Walawi hawatakuwa na sehemu miongoni mwenu, kwa maana huduma ya ukuhani kwa Bwana ndio urithi wao. Nao Gadi, Reubeni na nusu ya kabila la Manase wameshapata urithi wao upande wa mashariki mwa Yordani, ambako Mose mtumishi wa Bwana aliwapa.”

8 Watu hao walipokuwa wanaondoka kwenda kuandika vizuri kuhusu hiyo nchi, Yoshua akawaagiza, “Nendeni mkakague hiyo nchi na mwandike maelezo kuihusu. Kisha mrudi kwangu, nami nitawapigia kura hapa Shilo mbele za Bwana.” 9 Ndipo hao watu walipoondoka na kupita katika ile nchi. Wakaandika maelezo yake kwenye kitabu, mji kwa mji, katika sehemu saba na kurudisha taarifa kwa Yoshua huko kambini Shilo. 10 Basi Yoshua akawapigia kura huko Shilo mbele za Bwana, na hapo akagawanya ile nchi kwa Waisraeli kufuatana na mgawanyo wa kabila zao.