Ayubu Anatangaza Kutokuwa na Hatia

2130 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ayubu 16–17

1 Kisha Ayubu akajibu:

2 “Nimepata kusikia mambo mengi kama haya,

nanyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha!

3 Je, maneno yenu mengi yasiyo na maana hayana mwisho?

Mna nini hata mwendelee kushindana kwa maneno?

4 Mimi pia ningeweza kuzungumza kama ninyi,

kama mngekuwa katika hali yangu;

ningeweza kutoa hotuba nzuri dhidi yenu,

na kuwatikisia ninyi kichwa changu.

5 Lakini kinywa changu kingewatia moyo;

faraja kutoka midomoni mwangu, ingewaletea nafuu.

6 “Lakini kama nikisema, maumivu yangu bado hayatulizwi;

nami kama nikijizuia, wala hayaondoki.

7 Ee Mungu, hakika umenichakaza;

umewaangamiza kabisa watu wa nyumbani mwangu wote.

8 Umenikunjakunja, nalo limekuwa ushahidi;

nako kukonda kwangu kumeongezeka sana na kushuhudia dhidi yangu.

9 Mungu amenishambulia na kunirarua katika hasira yake,

na kunisagia meno yake;

adui yangu hunikazia macho yake makali.

10 Watu wamenifumbulia vinywa vyao kunidhihaki;

hunipiga shavuni mwangu kwa dharau,

na kuungana pamoja dhidi yangu.

11 Mungu amenigeuzia kwa watu wabaya,

na kunitupa katika makucha ya waovu.

12 Mambo yote yalikuwa mazuri, lakini alinivunjavunja;

amenikamata shingo na kuniponda.

Amenifanya mimi kuwa shabaha yake;

13 wapiga upinde wake wananizunguka.

Bila huruma, huchoma figo zangu,

na kuimwaga nyongo yangu juu ya nchi.

14 Huniponda tena na tena;

hunishambulia kama shujaa wa vita.

15 “Nimejishonea nguo ya gunia juu ya mwili wangu

nami nimekizika kipaji cha uso wangu kwenye vumbi.

16 Uso wangu umekuwa mwekundu kwa kulia,

macho yangu yamepigwa na giza kuu.

17 Hata hivyo mikono yangu haijafanya jeuri,

na maombi yangu ni safi.

18 “Ee nchi, usiifunike damu yangu,

nacho kilio changu kisinyamazishwe kamwe.

19 Hata sasa shahidi wangu yuko mbinguni;

wakili wangu yuko juu.

20 Mwombezi wangu ni rafiki yangu

macho yangu yamwagapo machozi kwa Mungu;

21 kwa niaba ya mtu anamsihi Mungu

kama mtu anavyosihi kwa ajili ya rafiki yake.

22 “Ni miaka michache tu itapita

kabla sijaenda safari ambayo sitarudi.

17:1 Moyo wangu umevunjika,

siku zangu zimefupishwa,

kaburi linaningojea.

2 Hakika wenye mizaha wamenizunguka;

macho yangu yamebaki kutazama uadui wao.

3 “Ee Mungu, nipe dhamana unayodai.

Ni nani mwingine atakayeweka dhamana kwa ajili yangu?

4 Umezifunga akili zao zisipate ufahamu,

kwa hiyo hutawaacha wapate ushindi.

5 Kama mtu akiwashutumu rafiki zake ili apate ujira,

macho ya watoto wake yatashindwa kuona.

6 “Mungu amenifanya kitu cha dhihaka kwa kila mtu,

mtu ambaye watu humtemea mate usoni.

7 Macho yangu yamefifia kwa ajili ya majonzi;

umbile langu lote ni kama kivuli.

8 Watu wanyofu wanatishwa na hili;

watu wasio na hatia wanasimama dhidi ya wasiomcha Mungu.

9 Hata hivyo, waadilifu watazishika njia zao,

nao wale wenye mikono safi wataendelea kupata nguvu.

10 “Lakini ninyi njooni, ninyi nyote, jaribuni tena!

Sitampata mtu mwenye hekima miongoni mwenu.

11 Siku zangu zimepita, mipango yangu imevunjika,

vivyo hivyo shauku za moyo wangu.

12 Watu hawa hufanya usiku kuwa mchana,

kwenye giza wao husema, ‘Mwanga u karibu.’

13 Kama nyumba pekee ninayoitarajia ni kaburi,

kama nikikitandika kitanda changu gizani,

14 kama nikiuambia uharibifu, ‘Wewe u baba yangu,’

na kuliambia buu, ‘Wewe u mama yangu’ au ‘Dada yangu,’

15 liko wapi basi tarajio langu?

Ni nani awezaye kuona tarajio lolote kwa ajili yangu?

16 Je, litashuka chini hadi kwenye malango ya mauti?

Je, tutashuka pamoja mavumbini?”