Ayubu Anajibu Hoja Yote (continued)

2130 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ayubu 13–14

1 “Macho yangu yameona hili lote,

masikio yangu yamesikia na kulielewa.

2 Hayo mnayoyajua mimi pia ninayajua;

mimi si mtu duni kuliko ninyi.

3 Lakini ninayo shauku ya kuzungumza na Mwenyezi

na kuhojiana shauri langu na Mungu.

4 Ninyi, hata hivyo, hunipakaza uongo;

ninyi ni matabibu wasiofaa kitu, ninyi nyote!

5 Laiti wote mngenyamaza kimya!

Kwa kuwa kwenu hilo lingekuwa hekima.

6 Sikieni sasa hoja yangu;

sikilizeni kusihi kwangu.

7 Je, mtazungumza kwa uovu kwa niaba ya Mungu?

Je, mtazungumza kwa udanganyifu kwa niaba yake?

8 Mtamwonyesha upendeleo?

Mtamtetea Mungu kwenye mashtaka yake?

9 Je, ingekuwa vyema Mungu akiwahoji ninyi?

Je, mngeweza kumdanganya kama ambavyo mngeweza kuwadanganya wanadamu?

10 Hakika angewakemea

kama mkiwapendelea watu kwa siri.

11 Je, huo ukuu wake haungewatisha ninyi?

Je, hofu yake isingewaangukia ninyi?

12 Maneno yenu ni mithali za majivu;

utetezi wenu ni ngome za udongo wa mfinyanzi.

13 “Nyamazeni kimya nipate kusema;

kisha na yanipate yatakayonipata.

14 Kwa nini nijiweke mwenyewe kwenye hatari

na kuyaweka maisha yangu mikononi mwangu?

15 Ingawa ataniua, bado nitamtumaini;

hakika nitazitetea njia zangu mbele zake.

16 Naam, hili litanigeukia kuwa wokovu wangu,

kwa maana hakuna mtu asiyemcha Mungu

atakayethubutu kuja mbele yake!

17 Sikilizeni maneno yangu kwa makini;

nayo masikio yenu yaingize kile nisemacho.

18 Sasa kwamba nimekwisha kutayarisha mambo yangu,

ninajua mimi nitahesabiwa kuwa na haki.

19 Je, kuna yeyote anayeweza kuleta mashtaka dhidi yangu?

Kama ndivyo, nitanyamaza kimya na nife.

20 “Ee Mungu, unijalie tu mimi haya mambo mawili,

nami sitajificha uso wako:

21 Ondoa mkono wako uwe mbali nami,

nawe uache kuniogofya kwa hofu zako kuu.

22 Niite kwenye shauri nami nitajibu,

au niache niseme, nawe upate kujibu.

23 Ni makosa na dhambi ngapi nilizotenda?

Nionyeshe kosa langu na dhambi yangu.

24 Kwa nini kuuficha uso wako

na kunihesabu mimi kuwa adui yako?

25 Je, utaliadhibu jani lipeperushwalo na upepo?

Je, utayasaka makapi makavu?

26 Kwa kuwa unaandika mambo machungu dhidi yangu

na kunifanya nizirithi dhambi za ujana wangu.

27 Umeifunga miguu yangu kwenye pingu.

Unazichunga kwa makini njia zangu zote

kwa kutia alama kwenye nyayo za miguu yangu.

28 “Hivyo mwanadamu huangamia kama kitu kilichooza,

kama vazi lililoliwa na nondo.

14:1 “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke

siku zake ni chache nazo zimejaa taabu.

2 Huchanua kama ua kisha hunyauka;

huwa kama kivuli kipitacho upesi, wala hadumu.

3 Je, unamwekea jicho lako mtu kama huyo?

Je, utamleta mbele yako katika hukumu?

4 Ni nani awezaye kutoa kitu safi kutoka kitu najisi?

Hakuna awezaye!

5 Siku za mwanadamu zimewekewa mpaka;

umekwisha kutangaza idadi ya miezi yake

na kuweka mpaka ambao hawezi kuuvuka.

6 Hivyo angalia mbali umwache,

hadi awe amekamilisha muda wake

kama mtu aliyeajiriwa.

7 “Kwa maana lipo tumaini kwa mti;

kama ukikatwa utachipuka tena,

nayo machipukizi yake mapya hayatakoma.

8 Mizizi yake yaweza kuchakaa ardhini

na kisiki chake kufa udongoni,

9 lakini kwa kupata dalili ya maji utachipua

na kutoa machipukizi kama mche.

10 Lakini mwanadamu hufa, na huo ndio mwisho wake;

hutoa pumzi ya mwisho, naye hayuko tena!

11 Kama vile maji yatowekavyo katika bahari,

au mkondo wa mto ukaushwavyo na kuwa mkavu,

12 ndivyo mwanadamu alalavyo chini asiamke;

hadi mbingu zitakapokuwa hazipo tena,

wanadamu hawataamka au kuamshwa

kutoka kwenye usingizi wao.

13 “Laiti kama ungenificha kaburini,

na kunisitiri hadi hasira yako ipite!

Laiti ungeniwekea wakati,

na kisha ukanikumbuka!

14 Je, kama mtu akifa, aweza kuishi tena?

Siku zote za kazi zangu ngumu

nitangojea kufanywa upya kwangu.

15 Utaniita nami nitakuitika;

utakionea shauku kiumbe ambacho mikono yako ilikiumba.

16 Hakika ndipo utakapozihesabu hatua zangu,

lakini hutazifuatia dhambi zangu.

17 Makosa yangu yatafungiwa kwa lakiri kwenye mfuko,

nawe utazifunika dhambi zangu.

18 “Lakini kama mlima umomonyokavyo na kufikichika

na kama vile mwamba uondolewavyo mahali pake,

19 kama maji yamalizavyo mawe,

na mafuriko yachukuavyo udongo,

ndivyo unavyoharibu tegemeo la mwanadamu.

20 Humshinda mara moja kwa daima, naye hutoweka;

waibadilisha sura yake na kumwondoa.

21 Kama wanawe wakipewa heshima, yeye hafahamu;

kama wakidharauliwa, yeye haoni.

22 Yeye hasikii kingine isipokuwa maumivu ya mwili wake mwenyewe,

naye huomboleza kwa ajili yake mwenyewe.”