Ayubu Anamjibu Bildadi: Mateso Hayathibitishi Uovu

Ayubu anamjibu Bildadi, na kudai kwamba mateso si uthibitisho wa uovu.

2130 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ayubu 9–10

1 Kisha Ayubu akajibu:

2 “Naam, najua hili ni kweli.

Lakini mwanadamu awezaje kuwa mwadilifu mbele za Mungu?

3 Ingawa mtu angetaka kushindana naye,

asingaliweza kumjibu Mungu hata mara moja miongoni mwa elfu moja.

4 Hekima yake ni kubwa sana na ana uwezo mwingi mno.

Ni nani aliyempinga naye akawa salama?

5 Aiondoa milima bila yenyewe kujua

na kuipindua kwa hasira yake.

6 Aitikisa dunia kutoka mahali pake

na kuzifanya nguzo zake zitetemeke.

7 Husema na jua, nalo likaacha kuangaza;

naye huizima mianga ya nyota.

8 Yeye peke yake huzitandaza mbingu

na kuyakanyaga mawimbi ya bahari.

9 Yeye ndiye Muumba wa nyota za Dubu, na Orioni,

Kilimia, na makundi ya nyota za kusini.

10 Hutenda maajabu yasiyopimika,

miujiza isiyoweza kuhesabiwa.

11 Anapopita karibu nami, siwezi kumwona;

apitapo mbele yangu, simtambui.

12 Anapochukua kwa ghafula, ni nani awezaye kumzuia?

Ni nani awezaye kumwambia, ‘Unafanya nini?’

13 Mungu hataizuia hasira yake;

hata jeshi kubwa la Rahabu lenye nguvu

linajikunyata miguuni pake.

14 “Ni vipi basi mimi nitaweza kubishana naye?

Nawezaje kupata maneno ya kuhojiana naye?

15 Ingawa sikuwa na hatia, sikuweza kumjibu;

ningeweza tu kumsihi Mhukumu wangu anihurumie.

16 Hata kama ningemwita kwenye shauri, naye akakubali,

siamini kama angenisikiliza.

17 Yeye angeniangamiza kwa dhoruba

na kuongeza majeraha yangu pasipo na sababu.

18 Asingeniacha nipumue

bali angenifunika kabisa na huzuni kuu.

19 Kama ni suala la nguvu, yeye ni mwenye nguvu!

Kama ni suala la haki, ni nani awezaye kumwita mahakamani?

20 Hata kama sikuwa na hatia, kinywa changu kingenihukumu;

kama sikuwa na kosa, kingenitangaza kuwa mwenye hatia.

21 “Ingawa mimi sina kosa,

haileti tofauti katika nafsi yangu;

nauchukia uhai wangu.

22 Hayo yote ni sawa; ndiyo sababu nasema,

‘Yeye huwaangamiza wasio na makosa pamoja na waovu.’

23 Wakati pigo liletapo kifo cha ghafula,

yeye hudhihaki kule kukata tamaa kwa yule asiye na kosa.

24 Wakati nchi inapoangukia mikononi mwa waovu,

yeye huwafunga macho mahakimu wake.

Kama si yeye, basi ni nani?

25 “Siku zangu zapita mbio kuliko mkimbiaji;

zinapita upesi bila kuona furaha hata kidogo.

26 Zinapita upesi kama mashua ya mafunjo,

mfano wa tai ayashukiaye mawindo kwa ghafula.

27 Kama nikisema, ‘Nitayasahau malalamiko yangu,

nitabadili sura ya uso wangu na kutabasamu,’

28 bado ninahofia mateso yangu yote,

kwa kuwa ninajua hutanihesabu kuwa sina hatia.

29 Kwa kuwa nimeonekana mwenye hatia,

kwa nini basi nitaabishwe bure?

30 Hata kama ningejiosha kwa sabuni

na kutakasa mikono yangu kwa magadi,

31 wewe ungenitupa kwenye shimo la utelezi

kiasi kwamba hata nguo zangu zingenichukia sana.

32 “Yeye si mwanadamu kama mimi ili niweze kumjibu,

ili kwamba tuweze kushindana naye mahakamani.

33 Laiti angelikuwepo mtu wa kutupatanisha kati yetu,

aweke mkono wake juu yetu sote wawili,

34 mtu angeliiondoa fimbo ya Mungu juu yangu,

ili utisho wake usiendelee kunitia hofu.

35 Ndipo ningenena naye, bila kumwogopa,

lakini kama ilivyo kwangu sasa, sitaweza.

10:1 “Nayachukia sana haya maisha yangu;

kwa hiyo nitatoa malalamiko yangu kwa wazi bila kujizuia,

nami nitanena kutokana na uchungu wa moyo wangu.

2 Nitamwambia Mungu: Usinihukumu,

bali niambie una mashtaka gani dhidi yangu.

3 Je, inakupendeza wewe kunionea,

kuikataa kwa dharau kazi ya mikono yako,

huku wewe ukitabasamu juu ya mipango ya waovu?

4 Je, wewe una macho ya kimwili?

Je, wewe huona kama mwanadamu aonavyo?

5 Je, siku zako ni kama zile za mwanadamu,

au miaka yako ni kama ile ya mtu,

6 ili kwamba utafute makosa yangu

na kuichunguza dhambi yangu;

7 ingawa wajua kuwa mimi sina hatia,

na hakuna awezaye kunitoa mkononi mwako?

8 “Mikono yako ndiyo iliyoniumba na kunifanya.

Je, sasa utageuka na kuniangamiza?

9 Kumbuka kuwa ulinifinyanga kama udongo wa mfinyanzi.

Je, sasa utanifanya kuwa mavumbi tena?

10 Je, wewe hukunimimina mimi kama maziwa,

na kunigandisha kama jibini,

11 ukanivika ngozi na nyama,

na kuniunga pamoja kwa mifupa na mishipa?

12 Umenipa uhai na kunitendea wema,

katika uangalizi wako umeilinda roho yangu.

13 “Lakini hili ndilo ulilolificha moyoni mwako,

nami ninajua kuwa hili lilikuwa katika nia yako:

14 Kama nilifanya dhambi, ungekuwa umeniona,

wala usingeacha kosa langu lipite bila kuadhibiwa.

15 Kama nina hatia, ole wangu!

Hata kama ningekuwa sina hatia,

siwezi kukiinua kichwa changu,

kwa kuwa nimejawa na aibu,

na kuzama katika mateso yangu.

16 Kama nikiinua kichwa changu juu, unaninyatia kama simba,

na kuonyesha tena uwezo wa kutisha dhidi yangu.

17 Wewe waleta mashahidi wapya dhidi yangu

na kuzidisha hasira yako juu yangu;

nazo nguvu zako zinanijia wimbi moja baada ya jingine.

18 “Kwa nini basi ulinitoa tumboni?

Ninatamani ningekufa kabla jicho lolote halijaniona.

19 Laiti nisingekuwako kamwe,

au ningekuwa nimechukuliwa moja kwa moja

kutoka tumboni kwenda kaburini!

20 Je, siku zangu chache si zimekaribia kuisha?

Niachie ili niweze kupata muda mfupi wa kufurahi

21 kabla sijaenda mahali ambapo hakuna kurudi tena,

katika nchi ya giza na uvuli wa mauti,

22 nchi ya giza kuu sana,

yenye uvuli wa giza na machafuko,

mahali ambapo hata nuru ni giza.”