Yesu Anatabiri Kifo Chake na Kuwakemea Yakobo na Yohana
Yesu anawatabiria wanafunzi tena kuhusu kifo na ufufuo wake, na kukemea tamaa ya ubinafsi ya Yakobo na Yohana.
Yamkini huko Perea
29 hadi 30 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 20:17–28
20:17 Basi Yesu alipokuwa anapanda kwenda Yerusalemu, aliwachukua kando wale wanafunzi wake kumi na wawili na kuwaambia,
18 “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa viongozi wa makuhani na walimu wa sheria. Nao watamhukumu kifo
19 na kumtia mikononi mwa watu wa Mataifa ili wamdhihaki na kumpiga mijeledi na kumsulubisha msalabani. Naye atafufuliwa siku ya tatu!”
20 Kisha mama yao wana wa Zebedayo akamjia Yesu pamoja na wanawe, naye akapiga magoti mbele yake, akamwomba Yesu amfanyie jambo fulani.
21 Yesu akamuuliza, “Unataka nini?” Akajibu, “Tafadhali, wajalie wanangu hawa ili mmoja aketi upande wako wa kuume, na mwingine upande wako wa kushoto katika Ufalme wako.”
22 Yesu akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe nitakachonywea mimi?”
Wakajibu, “Tunaweza.”
23 Yesu akawaambia, “Kwa kweli kikombe changu mtakinywea, lakini kuketi upande wangu wa kuume au wa kushoto si langu mimi kuwapa. Nafasi hizo ni za wale ambao wameandaliwa na Baba yangu.”
24 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia haya, waliwakasirikia hao ndugu wawili.
25 Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, nao wenye vyeo huonyesha mamlaka yao.
26 Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu,
27 naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu hana budi kuwa mtumwa wenu:
28 kama vile ambavyo Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”
Marko 10:32–45
10:32 Walikuwa njiani wakipanda kwenda Yerusalemu, na Yesu alikuwa ametangulia. Wanafunzi wake walishangaa, nao watu waliowafuata walijawa na hofu. Yesu akawachukua tena wale wanafunzi wake kumi na wawili kando na kuwaambia yatakayompata.
33 Akasema, “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atasalitiwa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa sheria. Wao watamhukumu kifo na kumtia mikononi mwa watu wa Mataifa,
34 ambao watamdhihaki na kumtemea mate, watampiga na kumuua. Siku tatu baadaye atafufuka.”
35 Kisha Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, wakaja kwake na kumwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie lolote tutakalokuomba.”
36 Naye akawaambia, “Je, mwataka niwafanyie jambo gani?”
37 Wakamwambia, “Tupe kukaa mmoja upande wako wa kuume na mwingine upande wako wa kushoto katika utukufu wako.”
38 Lakini Yesu akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi?”
39 Wakajibu, “Tunaweza.”
Kisha Yesu akawaambia, “Kikombe nikinyweacho mtakinywea na ubatizo nibatizwao mtabatizwa,
40 lakini kuketi mkono wangu wa kuume au wa kushoto si juu yangu mimi kuwapa. Nafasi hizi ni kwa ajili ya wale walioandaliwa.”
41 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana.
42 Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa wale wanaodhaniwa kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala watu kwa nguvu, nao wenye vyeo huonyesha mamlaka yao.
43 Lakini isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu,
44 na yeyote anayetaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa mtumwa wa wote.
45 Kwa kuwa hata Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”
Luka 18:31–34
18:31 Yesu akawachukua wale wanafunzi wake kumi na wawili kando na kuwaambia, “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na kila kitu kilichoandikwa na manabii kumhusu Mwana wa Adamu kitatimizwa.
32 Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa watu wasiomjua Mungu, nao watamdhihaki, watamtukana na kumtemea mate, watampiga mijeledi na kumuua.
33 Naye siku ya tatu atafufuka.”
34 Wanafunzi wake hawakuelewa mambo haya, kwa kuwa maana yake ilikuwa imefichika kwao, nao hawakujua Yesu alikuwa anazungumzia nini.