Yeremia Atabiri Dhidi ya Jeshi la Neko

Unabii wa Yeremia dhidi ya jeshi la Farao Neko.

606 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yeremia 46:1–12

1 Hili ni neno la Bwana lililomjia nabii Yeremia kuhusu mataifa:

2 Kuhusu Misri:

Huu ni ujumbe dhidi ya jeshi la Farao Neko mfalme wa Misri, lililoshindwa huko Karkemishi kwenye Mto Frati na Nebukadneza mfalme wa Babeli, katika mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda:

3 “Wekeni tayari ngao zenu, kubwa na ndogo,

mtoke kwa ajili ya vita!

4 Fungieni farasi lijamu,

pandeni farasi!

Shikeni nafasi zenu

mkiwa mmevaa chapeo!

Isugueni mikuki yenu,

vaeni dirii vifuani!

5 Je, ninaona nini?

Wametiwa hofu,

wanarudi nyuma,

askari wao wameshindwa.

Wanakimbia kwa haraka

pasipo kutazama nyuma,

tena kuna hofu kuu kila upande,”

asema Bwana.

6 Walio wepesi na wenye mbio hawawezi kukimbia,

wala wenye nguvu hawawezi kutoroka.

Kaskazini, kando ya Mto Frati,

wanajikwaa na kuanguka.

7 “Ni nani huyu ajiinuaye kama Mto Naili,

kama mito yenye maji yanayofanya mawimbi?

8 Misri hujiinua kama Mto Naili,

kama mito yenye maji yanayofanya mawimbi.

Husema, ‘Nitainuka na kufunika dunia,

nitaiangamiza miji na watu wake.’

9 Songeni mbele, enyi farasi!

Endesheni kwa ukali, enyi magari ya farasi,

Endeleeni mbele, enyi mashujaa:

watu wa Kushi na Putu wachukuao ngao,

watu wa Ludi wavutao upinde.

10 Lakini ile siku ni ya Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote,

siku ya kulipiza kisasi,

kisasi juu ya adui zake.

Upanga utakula hata utakapotosheka,

hadi utakapozima kiu yake kwa damu.

Kwa maana Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, atatoa dhabihu

kwenye nchi ya kaskazini, kando ya Mto Frati.

11 “Panda hadi Gileadi ukapate zeri,

ee Bikira Binti wa Misri.

Lakini umetumia dawa nyingi bila mafanikio;

huwezi kupona.

12 Mataifa yatasikia juu ya aibu yako,

kilio chako kitaijaza dunia.

Shujaa mmoja atajikwaa juu ya mwingine,

nao wataanguka chini pamoja.”

Warekabi Wapata Kimbilio Yerusalemu

Warekabi wanapata kimbilio Yerusalemu wakilikimbia jeshi la Wakaldayo.

Yeremia 35

1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana, wakati wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda: 2 “Nenda kwa jamaa ya Warekabi, uwaalike waje kwenye moja ya vyumba vya pembeni vya nyumba ya Bwana, na uwape divai wanywe.”

3 Basi nikaenda kumwita Yaazania mwana wa Yeremia, mwana wa Habazinia, na ndugu zake na wanawe wote, yaani jamaa nzima ya Warekabi. 4 Nikawaleta katika nyumba ya Bwana, ndani ya chumba cha wana wa Hanani mwana wa Igdalia mtu wa Mungu. Kilikuwa karibu na chumba cha maafisa, ambacho kilikuwa juu ya kile cha Maaseya mwana wa Shalumu, aliyekuwa bawabu. 5 Kisha nikaweka mabakuli yaliyojaa divai na baadhi ya vikombe mbele ya watu wa jamaa ya Warekabi na kuwaambia, “Kunyweni divai.”

6 Lakini wao wakajibu, “Sisi hatunywi divai, kwa sababu baba yetu Yonadabu mwana wa Rekabu, alitupa agizo hili: ‘Ninyi wala wazao wenu kamwe msinywe divai. 7 Pia msijenge nyumba kamwe, wala kuotesha mbegu au kupanda mashamba ya mizabibu. Kamwe msiwe na kitu chochote katika hivi, lakini siku zote lazima muishi kwenye mahema. Ndipo mtakapoishi kwa muda mrefu katika nchi ambayo ninyi ni wahamiaji.’ 8 Tumetii kila kitu ambacho baba yetu Yonadabu mwana wa Rekabu alituamuru. Sisi wenyewe wala wake zetu wala wana wetu na binti zetu kamwe hatujanywa divai 9 wala kujenga nyumba za kuishi au kuwa na mashamba ya mizabibu, mashamba au mazao. 10 Tumeishi katika mahema na tumetii kikamilifu kila kitu alichotuamuru baba yetu Yonadabu. 11 Lakini wakati Nebukadneza mfalme wa Babeli alipoivamia nchi hii, tulisema, ‘Njooni, lazima twende Yerusalemu ili kukimbia majeshi ya Wakaldayo na ya Washamu.’ Kwa hiyo tumeishi Yerusalemu.”

12 Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia kusema: 13 “Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, aliye Mungu wa Israeli, asemalo: Nenda ukawaambie watu wa Yuda na watu wa Yerusalemu, ‘Je, hamwezi kujifunza kutoka kwa wana wa Rekabu, na kuyatii maneno yangu?’ asema Bwana. 14 ‘Yonadabu mwana wa Rekabu aliwaagiza wanawe wasinywe divai, na agizo hilo wamelishika mpaka leo hawanywi divai, kwa sababu wanatii amri ya baba yao. Lakini nimenena nanyi tena na tena, lakini hamkunitii mimi. 15 Tena na tena nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu. Wakasema, “Kila mmoja wenu ni lazima ageuke na kuacha njia zake mbaya, na kuyatengeneza matendo yake. Msifuate miungu mingine ili kuitumikia. Ndipo mtakapoishi katika nchi niliyowapa ninyi na baba zenu.” Lakini hamkujali wala kunisikiliza. 16 Wazao wa Yonadabu mwana wa Rekabu walitimiza amri ambayo baba yao aliwapa, lakini watu hawa hawakunitii mimi.’

17 “Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Sikilizeni! Nitaleta juu ya Yuda na juu ya kila mmoja aishiye Yerusalemu kila aina ya maafa niliyotamka dhidi yao. Nilinena nao, lakini hawakusikiliza. Niliwaita, lakini hawakujibu.’ ”

18 Kisha Yeremia akaiambia jamaa ya Warekabi, “Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: ‘Mmetii amri ya baba yenu Yonadabu, na mmefuata mafundisho yake yote na mmefanya kila kitu alichowaamuru.’ 19 Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Yonadabu mwana wa Rekabu hatakosa kamwe kuwa na mtu wa kunitumikia mimi.’ ”