Isaya Anatabiri Adhabu na Kuongoka kwa Misri
Isaya anatabiri kurejeshwa kwa makabila kumi, adhabu ya Misri, na kuongoka kwa Misri na Ashuru.
721 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Ole kwa nchi ya mvumo wa mabawa,
kando ya mito ya Kushi,
2 iwapelekayo wajumbe wake kwa njia ya bahari
kwa mashua za mafunjo juu ya maji.
Nendeni, wajumbe wepesi,
kwa taifa la watu warefu wenye ngozi nyororo,
kwa taifa linaloogopwa mbali na karibu,
taifa gomvi lenye lugha ngeni,
ambalo nchi yao imegawanywa kwa mito.
3 Enyi mataifa yote ya ulimwengu,
ninyi mnaoishi duniani
wakati bendera itakapoinuliwa milimani,
mtaiona,
nayo tarumbeta itakapolia,
mtaisikia.
4 Hili ndilo Bwana aliloniambia:
“Nitatulia kimya na kutazama
kutoka maskani yangu,
kama joto linalometameta katika mwanga wa jua,
kama wingu la umande
katika joto la wakati wa mavuno.”
5 Kwa maana, kabla ya mavuno,
wakati wa kuchanua ukishapita
na maua yakawa zabibu zinazoiva,
atayakata machipukizi kwa mundu wa kupogolea matawi,
naye atakata na kuyaondoa matawi yaliyopanuka.
6 Yote yataachwa kwa ajili ya ndege wawindao wa mlimani
na wanyama pori,
ndege watajilisha juu yake wakati wote wa kiangazi,
nao wanyama pori wakati wote wa masika.
7 Wakati huo matoleo yataletwa kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote
kutoka kwa taifa la watu warefu wenye ngozi nyororo,
kutoka kwa taifa linaloogopwa mbali na karibu,
kutoka taifa gomvi lenye lugha ngeni,
ambalo nchi yao imegawanywa kwa mito,
matoleo yataletwa katika Mlima Sayuni, mahali pa Jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote.
19:1 Neno kuhusu Misri:
Tazama, Bwana amepanda juu ya wingu liendalo kwa haraka
naye anakuja Misri.
Sanamu za Misri zinatetemeka mbele yake,
nayo mioyo ya Wamisri inayeyuka ndani yao.
2 “Nitamchochea Mmisri dhidi ya Mmisri,
ndugu atapigana dhidi ya ndugu,
jirani dhidi ya jirani,
mji dhidi ya mji,
ufalme dhidi ya ufalme.
3 Wamisri watakufa moyo,
na nitaibatilisha mipango yao.
Watatafuta ushauri kwa sanamu na kwa roho za waliokufa,
kwa waaguzi na kwa wale waongeao na mizimu.
4 Nitawatia Wamisri
mikononi mwa bwana mkatili
na mfalme mkali atatawala juu yao,”
asema Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote.
5 Maji ya mito yatakauka,
chini ya mto kutakauka kwa jua.
6 Mifereji itanuka;
vijito vya Misri vitapungua
na kukauka.
Mafunjo na nyasi vitanyauka,
7 pia mimea iliyoko kando ya Mto Naili,
pale mto unapomwaga maji baharini.
Kila shamba lililopandwa kando ya Mto Naili litakauka,
litapeperushwa na kutoweka kabisa.
8 Wavuvi watalia na kuomboleza,
wale wote watupao ndoano katika Mto Naili,
watadhoofika kwa majonzi.
9 Wale watu wafanyao kazi ya kitani kilichochambuliwa watakata tamaa,
wafumaji wa kitani safi watavunjika moyo.
10 Wafanyao kazi ya kufuma nguo watahuzunishwa,
nao vibarua wataugua moyoni.
11 Maafisa wa Soani ni wapumbavu kabisa,
washauri wa Farao wenye busara wanatoa ushauri wa kijinga.
Unawezaje kumwambia Farao,
“Mimi ni mmojawapo wa watu wenye hekima,
mwanafunzi wa wafalme wa zamani”?
12 Wako wapi sasa watu wako wenye hekima?
Wao wakuonyeshe na kukufahamisha
ni nini Bwana Mwenye Nguvu Zote
amepanga dhidi ya Misri.
13 Maafisa wa Soani wamekuwa wapumbavu,
viongozi wa Memfisi wamedanganyika,
walio mawe ya pembe ya taifa lake
wameipotosha Misri.
14 Bwana amewamwagia
roho ya kizunguzungu;
wanaifanya Misri iyumbayumbe
katika yale yote inayoyafanya,
kama vile mlevi ayumbayumbavyo
katika kutapika kwake.
15 Misri haiwezi kufanya kitu chochote,
cha kichwa wala cha mkia,
cha tawi la mtende wala cha tete.
16 Katika siku ile Wamisri watakuwa kama wanawake. Watatetemeka kwa hofu mbele ya mkono wa Bwana Mwenye Nguvu Zote anaoinua dhidi yao. 17 Nayo nchi ya Yuda itawatia hofu Wamisri, kila mmoja atakayetajiwa Yuda ataingiwa na hofu, kwa sababu ya kile ambacho Bwana Mwenye Nguvu Zote anapanga dhidi yao.
18 Katika siku hiyo miji mitano ya Misri, itazungumza lugha ya Kanaani, na kuapa kumtii Bwana Mwenye Nguvu Zote. Mji mmojawapo utaitwa Mji wa Uharibifu.
19 Katika siku hiyo patakuwepo madhabahu ya Bwana katikati ya Misri na mnara wa kumbukumbu kwa Bwana kwenye mpaka wa Misri. 20 Itakuwa alama na ushahidi kwa ajili ya Bwana Mwenye Nguvu Zote katika nchi ya Misri. Watakapomlilia Bwana kwa sababu ya watesi wao, Mungu atawapelekea mwokozi na mtetezi, naye atawaokoa. 21 Hivyo Bwana atajijulisha mwenyewe kwa Wamisri, nao katika siku hiyo watamkubali Bwana. Wataabudu kwa kumtolea dhabihu na sadaka za nafaka, watamwekea Bwana nadhiri na kuzitimiza. 22 Bwana ataipiga Misri kwa tauni; atawapiga na kuwaponya. Watamgeukia Bwana, naye atayasikia maombi yao na kuwaponya.
23 Katika siku hiyo kutakuwepo na njia kuu kutoka Misri hadi Ashuru. Waashuru watakwenda Misri, na Wamisri watakwenda Ashuru. Wamisri na Waashuru wataabudu pamoja. 24 Katika siku hiyo Israeli itakuwa ya tatu, pamoja na Misri na Ashuru, nao watakuwa baraka kwa dunia. 25 Bwana Mwenye Nguvu Zote atawabariki, akisema, “Baraka iwe kwa Misri watu wangu, kwa Ashuru kazi ya mikono yangu, na kwa Israeli urithi wangu.”