Ibada ya Sanamu Inaanza Miongoni mwa Waisraeli

1413 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Waamuzi 2:6–13

6 Baada ya Yoshua kuwapa watu ruhusa waende zao, Waisraeli wakaenda kwenye urithi wao wenyewe ili kumiliki nchi yao. 7 Watu wakamtumikia Bwana siku zote za maisha ya Yoshua, na za hao wazee walioishi baada ya Yoshua kufa, waliokuwa wameona mambo makuu ambayo Bwana alikuwa ametenda kwa ajili ya Israeli.

8 Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana, akafa akiwa na umri wa miaka 110. 9 Wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Heresi katika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini ya Mlima Gaashi.

10 Baada ya kizazi kile chote kukusanywa pamoja na baba zao, kikainuka kizazi kingine baada yao ambacho hakikumjua Bwana, wala matendo yale aliyokuwa ametenda kwa ajili ya Waisraeli. 11 Kwa hiyo Waisraeli wakatenda maovu machoni pa Bwana na kuwatumikia Mabaali. 12 Wakamwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyekuwa amewatoa katika nchi ya Misri. Wakaifuata na kuiabudu miungu mbalimbali ya mataifa yanayowazunguka. Wakamkasirisha Bwana, 13 kwa sababu walimwacha na kutumikia Baali na Maashtorethi.

Waamuzi 17–18

1 Palikuwa na mtu aliyeitwa Mika ambaye aliishi katika vilima vya Efraimu. 2 Akamwambia mama yake, “Zile shekeli 1,100 za fedha zilizochukuliwa kwako, ambazo nilisikia ukizinenea maneno ya laana, hizi hapa; mimi ndiye niliyezichukua, lakini sasa ninakurudishia.”

Ndipo mama yake akamwambia, “Bwana na akubariki, mwanangu.”

3 Alipozirudisha zile shekeli 1,100 za fedha kwa mama yake, mama yake akamwambia, “Mimi nimeiweka fedha hii wakfu kwa Bwana kwa ajili ya mwanangu kutengenezea kinyago cha kuchonga na sanamu ya kusubu. Mimi nitakurudishia wewe.”

4 Hivyo akamrudishia mama yake ile fedha, naye mama yake akachukua shekeli mia mbili za hiyo fedha na kumpa mfua fedha, ambaye aliifanyiza kinyago na sanamu. Navyo vikawekwa ndani ya nyumba ya Mika.

5 Basi Mika alikuwa na mahali pa kuabudia miungu, akatengeneza naivera, pamoja na vinyago, na kumweka mmoja wa wanawe kuwa kuhani wake. 6 Katika siku hizo Israeli hawakuwa na mfalme, kila mmoja akafanya kama alivyoona vyema machoni pake mwenyewe.

7 Basi palikuwa na kijana mmoja wa Bethlehemu ya Yuda. Yeye alikuwa Mlawi aliyeishi miongoni mwa kabila la Yuda. 8 Huyu kijana akatoka katika mji huo wa Bethlehemu ya Yuda na kutafuta mahali pengine ambapo angeweza kuishi. Alipokuwa akisafiri, akafika nyumbani kwa Mika katika vilima vya Efraimu.

9 Mika akamuuliza, “Wewe umetoka wapi?”

Akamjibu, “Mimi ni Mlawi kutoka Bethlehemu ya Yuda, ninatafuta mahali pa kuishi.”

10 Ndipo Mika akamwambia, “Ishi pamoja nami, uwe baba yangu na kuhani wangu, nami nitakupa shekeli kumi za fedha, nguo na chakula.” 11 Hivyo yule Mlawi akakubali kuishi pamoja naye, naye huyo kijana akawa kwake kama mmoja wa wanawe. 12 Hivyo Mika akamweka wakfu huyo kijana Mlawi, naye huyo akawa kuhani wake na kuishi nyumbani mwake. 13 Ndipo Mika akasema, “Sasa najua Bwana atanitendea mema, kwa kuwa Mlawi huyu amekuwa kuhani wangu.”

18:1 Katika siku hizo Israeli walikuwa hawana mfalme.

Katika siku hizo kabila la Wadani walikuwa wanatafuta mahali pao wenyewe pa kuishi, kwa sababu walikuwa hawajafika kwenye urithi wao miongoni mwa makabila ya Israeli. 2 Hivyo Wadani wakatuma mashujaa watano kutoka Sora na Eshtaoli ili kupeleleza nchi na kuichunguza. Hawa watu waliwakilisha koo zao zote. Waliwaambia, “Nendeni mkaichunguze hiyo nchi.”

Watu hao wakaingia katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao wakafika nyumba ya Mika, ambako walilala usiku huo. 3 Walipofika karibu na nyumba ya Mika, waliitambua sauti ya yule kijana Mlawi; hivyo wakaingia humo na kumuuliza, “Ni nani aliyekuleta hapa? Unafanya nini mahali hapa? Kwa nini uko hapa?”

4 Akawaeleza yale Mika aliyomtendea, naye akasema, “Ameniajiri nami ni kuhani wake.”

5 Kisha wakamwambia, “Tafadhali tuulizie kwa Mungu kama safari yetu itafanikiwa.”

6 Yule kuhani akawajibu, “Enendeni kwa amani. Safari yenu ina kibali cha Bwana.”

7 Basi hao watu watano wakaondoka na kufika Laishi, mahali ambapo waliwakuta watu wanaishi salama, kama Wasidoni, kwa utulivu na bila mashaka. Nchi yao haikupungukiwa na kitu chochote, hivyo wakawa tajiri. Pia walikaa mbali sana na Wasidoni, wala hawakushughulika na mtu yeyote.

8 Waliporudi kwa ndugu zao huko Sora na Eshtaoli, ndugu zao wakawauliza, “Mlionaje mambo huko?”

9 Wakajibu, “Twendeni, tukapigane nao! Tumeona kuwa nchi ni nzuri sana. Je, hamtafanya chochote? Msisite kupanda ili kuimiliki. 10 Mtakapokwenda huko mtakuta watu waliotulia walio salama, nayo nchi hiyo ni kubwa na Mungu ameitia mikononi mwenu, nayo ni nchi ambayo haikupungukiwa na kitu chochote kilicho duniani.”

11 Ndipo watu 600 toka ukoo wa Wadani, waliojifunga silaha za vita, wakaondoka Sora na Eshtaoli. 12 Walipokuwa wakisafiri wakapiga kambi huko Kiriath-Yearimu katika Yuda. Hii ndiyo sababu sehemu ya magharibi ya Kiriath-Yearimu inaitwa Mahane-Dani mpaka leo. 13 Kutoka hapo wakaendelea mbele mpaka nchi ya vilima ya Efraimu na kufika katika nyumba ya Mika.

14 Ndipo wale watu watano waliopeleleza nchi ya Laishi wakawaambia ndugu zao, “Je, mwajua kuwa mojawapo ya nyumba hizi kuna naivera, sanamu ndogo za nyumbani, sanamu ya kuchonga na sanamu ya kusubu? Sasa basi fikirini mtakalofanya.” 15 Basi wakaingia humo na kwenda kwenye nyumba ya yule kijana Mlawi katika nyumba ya Mika na kumsalimu. 16 Wale Wadani 600, waliovaa silaha za vita, wakasimama penye ingilio la lango. 17 Wale watu watano waliokwenda kupeleleza nchi wakaingia ndani na kuchukua ile sanamu ya kuchonga, ile naivera, na zile sanamu nyingine ndogo za nyumbani pamoja na ile sanamu ya kusubu, wakati yule kuhani akiwa amesimama pale penye ingilio la lango pamoja na wale watu 600 waliokuwa wamejifunga silaha za vita.

18 Hao watu walipoingia katika nyumba ya Mika na kuchukua ile sanamu ya kuchonga, ile naivera, na zile sanamu nyingine ndogo za nyumbani, pamoja na ile sanamu ya kusubu, yule kuhani akawauliza, “Mnafanya nini?”

19 Wakamjibu, “Nyamaza kimya! Weka mkono wako juu ya kinywa chako na ufuatane nasi, uwe baba yetu na kuhani wetu. Si ni afadhali utumikie kabila na ukoo katika Israeli kama kuhani kuliko kumtumikia mtu mmoja na watu wa nyumbani mwake?” 20 Yule kuhani akafurahi. Akachukua ile naivera, zile sanamu nyingine ndogo za nyumbani, na sanamu ya kuchonga, naye akaenda pamoja na wale watu. 21 Ndipo wakageuka na kuondoka wakiwatanguliza mbele watoto wao wadogo, wanyama wao wa kufugwa na mali zao.

22 Walipokuwa wamesafiri umbali kidogo toka nyumbani kwa Mika, watu walioishi karibu na Mika wakaitwa wakakusanyika pamoja, nao wakawafikia Wadani. 23 Walipofuatilia wakipiga kelele Wadani wakawageukia na kumwambia Mika, “Una nini wewe hata ukaja na kundi la watu namna hii ili kupigana?”

24 Akawajibu, “Mmechukua miungu yote niliyoitengeneza, mkachukua na kuhani wangu, nanyi mkaondoka. Nimebaki na nini kingine? Mnawezaje kuniuliza, ‘Una nini wewe?’ ”

25 Wadani wakamjibu, “Usibishane na sisi, la sivyo watu wenye hasira kali watakushambulia, nawe na watu wa nyumbani mwako mtapoteza maisha.” 26 Basi Wadani wakaenda zao, naye Mika alipoona kuwa wana nguvu kumliko yeye, akageuka na kurudi nyumbani kwake.

27 Kisha wakachukua vile Mika alivyokuwa ametengeneza, na kuhani wake, wakaendelea hadi Laishi, dhidi ya watu walio na amani, wasiokuwa na wasiwasi. Wakawashambulia kwa upanga na kuuteketeza mji wao kwa moto. 28 Hapakuwa na yeyote wa kuwaokoa, kwa kuwa kulikuwa mbali sana na Sidoni na hawakuwa na ushirikiano na mtu mwingine yeyote. Mji ulikuwa kwenye bonde karibu na Beth-Rehobu.

Wadani wakaujenga upya huo mji na kuishi humo. 29 Wakauita ule mji Dani kwa kufuata jina la baba yao aliyezaliwa na Israeli, ingawa mji huo ulikuwa ukiitwa Laishi hapo kwanza. 30 Kisha Wadani wakajisimamishia sanamu ile ya kuchonga, naye Yonathani mwana wa Gershomu, mwana wa Mose pamoja na wanawe walikuwa makuhani wa kabila la Wadani mpaka nchi hiyo ilipotekwa. 31 Wakaisimamisha na kuiabudu hiyo sanamu ya kuchonga ya Mika aliyokuwa ameitengeneza, wakati wote ule nyumba ya Mungu ilipokuwa huko Shilo.