Ugonjwa wa Hezekia

Ugonjwa wa Hezekia: utangulizi.

713 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Nyakati 32:24–26

24 Katika siku hizo, Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Akamwomba Bwana, ambaye alimjibu na kumpa ishara. 25 Lakini moyo wa Hezekia ukajaa majivuno na hakuonyesha itikio kwa wema aliotendewa, kwa hiyo ghadhabu ya Bwana ikawa juu yake na juu ya Yuda na Yerusalemu. 26 Ndipo Hezekia akatubu kwa ajili ya kiburi cha moyo wake, kama walivyofanya watu wa Yerusalemu, kwa hiyo ghadhabu ya Bwana haikuja juu yao katika siku za Hezekia.

2 Wafalme 20:1–11

1 Katika siku hizo, Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akaenda kwake na kumwambia, “Hili ndilo asemalo Bwana: Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.”

2 Hezekia akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana: 3 “Ee Bwana, kumbuka jinsi nilivyoenenda mbele zako kwa uaminifu na kujitoa kwa moyo wangu wote, na kufanya yaliyo mema machoni pako.” Naye Hezekia akalia kwa uchungu.

4 Kabla Isaya hajaondoka katika ua wa kati, neno la Bwana likamjia, akaambiwa: 5 “Rudi ukamwambie Hezekia, kiongozi wa watu wangu, ‘Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa baba yako Daudi: Nimeyasikia maombi yako na nimeona machozi yako; nitakuponya. Siku ya tatu kuanzia sasa utapanda kwenda Hekalu la Bwana. 6 Nitakuongezea miaka kumi na mitano katika maisha yako. Nami nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi!’ ”

7 Kisha Isaya akasema, “Tengenezeni dawa ya kubandika ya tini.” Wakafanya hivyo na kuiweka kwenye jipu, naye akapona.

8 Hezekia alikuwa amemuuliza Isaya, “Kutakuwa na ishara gani kwamba Bwana ataniponya mimi, na kwamba nitapanda kwenda Hekalu la Bwana siku ya tatu tangu leo?”

9 Isaya akajibu, “Hii ndiyo ishara ya Bwana kwako kwamba Bwana atafanya kile alichoahidi: Je, kivuli kiende hatua kumi mbele, au kivuli kirudi nyuma hatua kumi?”

10 Hezekia akasema, “Ni jambo rahisi kwa kivuli kutangulia mbele hatua kumi, kuliko kukifanya kirudi nyuma hatua kumi.”

11 Ndipo nabii Isaya akamwita Bwana, naye Bwana akakifanya kivuli kurudi nyuma hatua kumi ambazo kilikuwa kimeshuka kwenye ngazi ya Ahazi.

Isaya 32–33

1 Tazama, mfalme atatawala kwa uadilifu

na watawala watatawala kwa haki.

2 Kila mtu atakuwa kama kivuli cha kujificha kutokana na upepo

na kimbilio kutokana na dhoruba,

kama vijito vya maji jangwani

na kivuli cha mwamba mkubwa katika ardhi yenye kiu.

3 Ndipo macho ya wale wanaoona hayatafumbwa tena,

nayo masikio ya wale wanaosikia yatasikiliza.

4 Moyo wa mtu mwenye hamaki utafahamu na kuelewa,

nao ulimi wenye kigugumizi utanena kwa ufasaha.

5 Mpumbavu hataitwa tena muungwana,

wala mtu mbaya kabisa kupewa heshima ya juu.

6 Kwa kuwa mpumbavu hunena upumbavu,

moyo wake hushughulika na uovu:

Hutenda mambo yasiyo ya kumcha Mungu,

na hueneza habari za makosa kuhusu Bwana;

yeye huwaacha wenye njaa bila kitu,

na wenye kiu huwanyima maji.

7 Taratibu za mtu mbaya kabisa ni ovu,

hufanya mipango miovu

ili kumwangamiza maskini kwa uongo,

hata wakati ambapo hoja za mhitaji ni za haki.

8 Lakini mtu muungwana hufanya mipango ya kiungwana,

na kwa matendo ya kiungwana yeye hufanikiwa.

9 Enyi wanawake wenye kuridhika sana,

amkeni na mnisikilize.

Enyi binti mnaojisikia kuwa salama,

sikieni lile ninalotaka kuwaambia!

10 Muda zaidi kidogo ya mwaka mmoja,

ninyi mnaojisikia salama mtatetemeka,

mavuno ya zabibu yatakoma

na mavuno ya matunda hayatakuwepo.

11 Tetemekeni, enyi wanawake wenye kuridhika,

tetemekeni kwa hofu, enyi binti mnaojisikia salama!

Vueni nguo zenu,

vaeni nguo ya gunia viunoni mwenu.

12 Pigeni matiti yenu kwa ajili ya mashamba mazuri,

kwa ajili ya mizabibu iliyozaa vizuri

13 na kwa ajili ya nchi ya watu wangu,

nchi ambayo miiba na michongoma imemea:

naam, ombolezeni kwa ajili ya nyumba zote za furaha

na kwa ajili ya mji huu wenye kufanya sherehe.

14 Ngome itaachwa,

mji wenye kelele nyingi utahamwa,

ngome ndani ya mji na mnara wa ulinzi vitakuwa ukiwa milele,

mahali pazuri pa punda na malisho ya makundi ya kondoo,

15 mpaka Roho amwagwe juu yetu kutoka juu,

nalo jangwa kuwa shamba lenye rutuba,

na shamba lenye rutuba kuwa kama msitu.

16 Haki itakaa katika jangwa,

na uadilifu utakaa katika shamba lenye rutuba.

17 Matunda ya haki yatakuwa amani,

matokeo ya haki yatakuwa utulivu

na matumaini milele.

18 Watu wangu wataishi katika makao ya mahali pa amani,

katika nyumba zilizo salama,

katika mahali pa kupumzika pasipo na usumbufu.

19 Hata kama mvua ya mawe iangushe msitu

na mji ubomolewe kabisa,

20 tazama jinsi utakavyobarikiwa,

ukipanda mbegu yako katika kila kijito,

na kuwaacha ngʼombe wako

na punda wajilishe kwa uhuru.

33:1 Ole wako wewe, ee mharabu,

wewe ambaye hukuharibiwa!

Ole wako, ee msaliti,

wewe ambaye hukusalitiwa!

Utakapokwisha kuharibu,

utaharibiwa;

utakapokwisha kusaliti,

utasalitiwa.

2 Ee Bwana, uturehemu,

tunakutamani.

Uwe nguvu yetu kila asubuhi

na wokovu wetu wakati wa taabu.

3 Kwa ngurumo ya sauti yako, mataifa yanakimbia;

unapoinuka, mataifa hutawanyika.

4 Mateka yenu, enyi mataifa, yamevunwa kama vile wafanyavyo madumadu,

kama kundi la nzige watu huvamia juu yake.

5 Bwana ametukuka, kwa kuwa anakaa mahali palipoinuka,

ataijaza Sayuni kwa haki na uadilifu.

6 Atakuwa msingi ulio imara kwa wakati wenu,

ghala za wokovu tele, hekima na maarifa;

kumcha Bwana ni ufunguo wa hazina hii.

7 Angalia, watu wake mashujaa wanapiga kelele kwa nguvu barabarani,

wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu.

8 Njia kuu zimeachwa,

hakuna wasafiri barabarani.

Mkataba umevunjika,

mashahidi wake wamedharauliwa,

hakuna yeyote anayeheshimiwa.

9 Ardhi inaomboleza na kuchakaa,

Lebanoni imeaibika na kunyauka,

Sharoni ni kama Araba,

nayo Bashani na Karmeli

wanapukutisha majani yao.

10 “Sasa nitainuka,” asema Bwana.

“Sasa nitatukuzwa;

sasa nitainuliwa juu.

11 Mlichukua mimba ya makapi,

mkazaa mabua,

pumzi yenu ni moto uwateketezao.

12 Mataifa yatachomwa kama ichomwavyo chokaa,

kama vichaka vya miiba vilivyokatwa ndivyo watakavyochomwa.”

13 Ninyi mlio mbali sana, sikieni lile nililofanya;

ninyi mlio karibu, tambueni uweza wangu!

14 Wenye dhambi katika Sayuni wametiwa hofu,

kutetemeka kumewakumba wasiomcha Mungu:

“Ni nani miongoni mwetu awezaye kuishi na moto ulao?

Ni nani miongoni mwetu awezaye kuishi na moto unaowaka milele?”

15 Yeye aendaye kwa uadilifu

na kusema lililo haki,

yeye anayekataa faida ipatikanayo kwa dhuluma

na kuizuia mikono yake isipokee rushwa,

yeye azuiaye masikio yake dhidi ya mashauri ya mauaji,

na yeye afumbaye macho yake yasitazame sana uovu:

16 huyu ndiye mtu atakayeishi mahali pa juu,

ambaye kimbilio lake litakuwa ngome ya mlimani.

Atapewa mkate wake,

na maji yake hayatakoma.

17 Macho yenu yatamwona mfalme katika uzuri wake

na kuiona nchi inayoenea mbali.

18 Katika mawazo yenu mtaifikiria hofu iliyopita:

“Yuko wapi yule afisa mkuu?

Yuko wapi yule aliyechukua ushuru?

Yuko wapi afisa msimamizi wa minara?”

19 Hutawaona tena wale watu wenye kiburi,

wale watu wenye usemi wa mafumbo,

wenye lugha ngeni, isiyoeleweka.

20 Mtazame Sayuni, mji wa sikukuu zetu;

macho yenu yatauona Yerusalemu,

mahali pa amani pa kuishi, hema ambalo halitaondolewa,

nguzo zake hazitangʼolewa kamwe,

wala hakuna kamba yake yoyote itakayokatika.

21 Huko Bwana atakuwa Mwenye Nguvu wetu.

Patakuwa kama mahali pa mito mipana na vijito.

Hakuna jahazi lenye makasia litakalopita huko,

wala hakuna meli yenye nguvu itakayopita huko.

22 Kwa kuwa Bwana ni mwamuzi wetu,

Bwana ndiye mtoa sheria wetu,

Bwana ni mfalme wetu,

yeye ndiye atakayetuokoa.

23 Kamba zenu za merikebu zimelegea:

Mlingoti haukusimama imara,

nalo tanga halikukunjuliwa.

Wingi wa mateka yatagawanywa,

hata yeye aliye mlemavu atachukua nyara.

24 Hakuna yeyote aishiye Sayuni atakayesema, “Mimi ni mgonjwa”;

nazo dhambi za wale waishio humo zitasamehewa.