Safari ya Kumi: Kutoka Alushi hadi Refidimu

Manung’uniko ya Kutaka Maji, na Vita dhidi ya Amaleki

Watu wananung’unika wakitaka maji, na kuna vita dhidi ya Amaleki.

1491 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Hesabu 33:14

14 Wakaondoka Alushi, wakapiga kambi Refidimu, mahali ambapo hapakuwa na maji kwa ajili ya watu kunywa.

Kutoka 17

1 Jumuiya yote ya Israeli ikaondoka kutoka Jangwa la Sini, ikisafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kama Bwana alivyoagiza. Wakapiga kambi huko Refidimu, lakini hapakuwa na maji ya watu kunywa. 2 Kwa hiyo wakagombana na Mose wakisema, “Tupe maji ya kunywa.”

Mose akajibu, “Mbona mnagombana nami? Kwa nini mnamjaribu Bwana?”

3 Lakini watu walikuwa na kiu huko, wakanungʼunika dhidi ya Mose, wakisema, “Kwa nini ulitutoa kule Misri, ukatuleta hapa utuue kwa kiu sisi, watoto wetu na mifugo yetu?”

4 Kisha Mose akamlilia Bwana, akasema, “Niwafanyie nini watu hawa? Sasa wanakaribia kunipiga kwa mawe.”

5 Bwana akamjibu Mose, “Pita mbele ya watu. Wachukue pamoja nawe baadhi ya wazee wa Israeli, ichukue mkononi mwako ile fimbo uliyopiga nayo Mto Naili, nawe uende. 6 Huko nitasimama mbele yako karibu na mwamba wa Horebu. Uupige mwamba na maji yatatoka ndani yake kwa ajili ya watu kunywa.” Kwa hiyo Mose akafanya haya mbele ya wazee wa Israeli. 7 Naye akapaita mahali pale Masa, na Meriba kwa sababu Waisraeli waligombana na kumjaribu Bwana wakisema, “Je, Bwana yu pamoja nasi au la?”

8 Waamaleki wakaja na kuwashambulia Waisraeli huko Refidimu. 9 Mose akamwambia Yoshua, “Chagua baadhi ya watu wetu na uende kupigana na Waamaleki. Kesho nitasimama juu ya kilima nikiwa na fimbo ya Mungu mkononi mwangu.”

10 Kwa hiyo Yoshua akapigana na Waamaleki kama Mose alivyomwagiza, nao Mose, Aroni na Huri wakapanda juu ya kilima. 11 Ikawa wakati wote Mose alipokuwa amenyanyua mikono yake, Waisraeli walikuwa wakishinda, lakini kila aliposhusha mikono yake Waamaleki walishinda. 12 Mikono ya Mose ilipochoka, wakachukua jiwe na kumpa alikalie. Aroni na Huri wakaishikilia juu mikono ya Mose, mmoja upande huu na mwingine upande huu. Wakaitegemeza mikono yake ikabaki thabiti mpaka jua lilipozama. 13 Kwa hiyo Yoshua akalishinda jeshi la Waamaleki kwa upanga.

14 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Andika mambo haya katika kitabu ili yakumbukwe, na uhakikishe kwamba Yoshua amesikia, kwa sababu nitafuta kabisa kumbukumbu la Amaleki chini ya mbingu.”

15 Mose akajenga madhabahu na kuiita Yehova Nisi. 16 Mose akasema, “Kwa maana mikono iliinuliwa mpaka kwenye kiti cha enzi cha Bwana. Bwana atakuwa na vita dhidi ya Waamaleki kutoka kizazi hata kizazi.”

Safari ya Kumi na Moja: Kutoka Refidimu hadi Sinai

Kutolewa kwa Sheria

Hesabu 33:15

15 Wakaondoka Refidimu na kupiga kambi katika Jangwa la Sinai.

Kutoka 19

1 Mnamo mwezi wa tatu baada ya Waisraeli kuondoka Misri, siku kama iyo hiyo, wakafika katika Jangwa la Sinai. 2 Baada ya kuondoka Refidimu, waliingia katika Jangwa la Sinai na Israeli wakapiga kambi pale jangwani mbele ya mlima.

3 Kisha Mose akakwea kwenda kwa Mungu, naye Bwana akamwita kutoka kwenye ule mlima akasema, “Hivi ndivyo utakavyosema na nyumba ya Yakobo na utakachowaambia watu wa Israeli: 4 ‘Ninyi wenyewe mmeona nililofanya huko Misri, jinsi nilivyowabeba kwenye mbawa za tai na kuwaleta kwangu. 5 Sasa kama mkinitii kikamilifu na kutunza Agano langu, basi ninyi mtakuwa mali yangu ya thamani kubwa miongoni mwa mataifa yote. Ijapokuwa dunia yote ni mali yangu, 6 ninyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani na taifa takatifu.’ Haya ndiyo maneno utakayosema kwa wana wa Israeli.”

7 Kwa hiyo Mose akarudi, akawaita wazee wa watu na kuwaambia maneno yote ambayo Bwana alikuwa amemwamuru ayaseme. 8 Watu wote wakajibu kwa pamoja, “Tutafanya kila kitu Bwana alichokisema.” Naye Mose akarudisha majibu yao kwa Bwana.

9 Bwana akamwambia Mose, “Nitakujia katika wingu zito, ili watu wanisikie nikinena nawe na kila mara waweke tumaini lao kwako.” Kisha Mose akamwambia Bwana yale ambayo watu walikuwa wamesema.

10 Naye Bwana akamwambia Mose, “Nenda kwa watu ukawaweke wakfu leo na kesho. Waambie wafue nguo zao 11 na wawe tayari siku ya tatu, kwa sababu siku hiyo, Bwana atashuka juu ya mlima Sinai machoni pa watu wote. 12 Weka mipaka kuzunguka mlima kwa ajili ya watu, uwaambie, ‘Mwe waangalifu, msije mkapanda mlimani au kuugusa. Yeyote atakayeugusa mlima hakika atauawa. 13 Hakika atapigwa mawe au kupigwa mishale; mkono wa mtu hautamgusa. Akiwa mwanadamu au mnyama, hataruhusiwa kuishi.’ Ila tu wakati baragumu itakapopigwa kwa mfululizo, ndipo watu wote watakapopanda mlimani.”

14 Baada ya Mose kushuka kutoka mlimani akawaendea watu na kuwaweka wakfu, wakafua nguo zao. 15 Kisha akawaambia watu, “Jitayarisheni kwa ajili ya siku ya tatu. Mwanaume yeyote asimkaribie mwanamke.”

16 Asubuhi ya siku ya tatu kulikuwa na ngurumo na radi pamoja na wingu nene juu ya mlima na mlio mkubwa sana wa tarumbeta. Kila mmoja aliyekuwa kambini akatetemeka. 17 Kisha Mose akawaongoza watu kutoka kambini kukutana na Mungu, nao wakasimama chini ya mlima. 18 Mlima Sinai ulikuwa umefunikwa na moshi, kwa sababu Bwana alishuka juu yake katika moto. Moshi wa moto huo ulipanda juu kama moshi kutoka kwenye tanuru kubwa na mlima wote ukatetemeka kwa nguvu nyingi, 19 nayo sauti ya tarumbeta ikawa kubwa zaidi na zaidi. Kisha Mose akazungumza na sauti ya Bwana ikamjibu.

20 Bwana akashuka juu ya Mlima Sinai na akamwita Mose apande juu mlimani. Kwa hiyo Mose akapanda juu, 21 naye Bwana akamwambia Mose, “Shuka ukawaonye watu ili wasijipenyeze kutafuta kumwona Bwana na wengi wao wakafa. 22 Hata makuhani, watakaomkaribia Bwana ni lazima wajiweke wakfu, la sivyo Bwana atawaadhibu.”

23 Mose akamwambia Bwana, “Watu hawawezi kupanda mlima Sinai kwa sababu wewe mwenyewe ulituonya ukisema, ‘Wekeni mipaka kuuzunguka mlima na kuutenga kama patakatifu.’ ”

24 Bwana akajibu, “Shuka ukamlete Aroni pamoja nawe. Lakini makuhani pamoja na watu wasije wakalazimisha kuja kwa Bwana, nisije nikawaadhibu.”

25 Basi Mose akashuka kwa watu na kuwaambia lile aliloambiwa.