Mungu Anamjaribu Abrahamu
Kujaribiwa kwa Abrahamu.
1871 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Baadaye Mungu akamjaribu Abrahamu. Akamwambia, “Abrahamu!”
Abrahamu akajibu, “Mimi hapa.”
2 Kisha Mungu akamwambia, “Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, Isaki umpendaye, uende katika nchi ya Moria. Mtoe huko kama sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.”
3 Abrahamu akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, akamtayarisha punda wake. Akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaki mwanawe. Baada ya kuchanja kuni za kutosha kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka kuelekea mahali Mungu alipokuwa amemwambia. 4 Siku ya tatu Abrahamu akainua macho, akapaona mahali pale kwa mbali. 5 Akawaambia watumishi wake, “Kaeni hapa pamoja na punda, wakati mimi na kijana tunakwenda kule. Tutakwenda kuabudu na kisha tutawarudia.”
6 Abrahamu akachukua kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, akamtwika Isaki mwanawe, yeye mwenyewe akachukua moto na kisu. Walipokuwa wakienda pamoja, 7 Isaki akanena akamwambia Abrahamu baba yake, “Baba yangu!”
Abrahamu akaitika, “Mimi hapa, mwanangu.”
Isaki akasema, “Moto na kuni zipo, Je, yuko wapi mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa?”
8 Abrahamu akajibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atajipatia mwana-kondoo kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa.” Nao hawa wawili wakaendelea mbele pamoja.
9 Walipofika mahali pale alipokuwa ameambiwa na Mungu, Abrahamu akajenga madhabahu hapo, akaziweka kuni juu yake. Akamfunga Isaki mwanawe na akamlaza kwenye madhabahu, juu ya zile kuni. 10 Kisha akanyoosha mkono wake na akachukua kisu ili amchinje mwanawe. 11 Lakini malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akamwambia, “Abrahamu! Abrahamu!”
Akajibu, “Mimi hapa.”
12 Akamwambia, “Usimdhuru kijana, wala usimtendee jambo lolote. Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwa sababu hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee.”
13 Abrahamu akainua macho yake, akaona kondoo dume amenaswa pembe zake nyuma yake katika kichaka. Akaenda akamchukua huyo kondoo dume, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. 14 Abrahamu akapaita mahali pale Yehova-Yire. Mpaka siku ya leo inasemekana, “Katika mlima wa Bwana itapatikana.”
15 Basi malaika wa Bwana akamwita Abrahamu kutoka mbinguni mara ya pili, 16 akasema, “Ninaapa kwa nafsi yangu, asema Bwana, kwamba kwa sababu umefanya jambo hili na hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee, 17 hakika nitakubariki, na nitauzidisha uzao wako kama nyota za angani na kama mchanga ulioko pwani. Wazao wako watamiliki miji ya adui zao, 18 na kupitia uzao wako mataifa yote duniani yatabarikiwa, kwa sababu umenitii.”
19 Ndipo Abrahamu akawarudia watumishi wake, wakaondoka wakaenda wote pamoja mpaka Beer-Sheba. Abrahamu akaishi huko Beer-Sheba.
Kifo na Mazishi ya Sara 1859 KK
1 Sara aliishi akawa na umri wa miaka mia na ishirini na saba. 2 Sara akafa huko Kiriath-Arba (yaani Hebroni) katika nchi ya Kanaani, Abrahamu akamwombolezea na kumlilia Sara.
3 Ndipo Abrahamu akainuka kutoka pale penye maiti ya mke wake. Akazungumza na Wahiti, akasema, 4 “Mimi ni mpitaji na mgeni miongoni mwenu. Niuzieni sehemu ya ardhi yenu ili niweze kumzika maiti wangu.”
5 Wahiti wakamjibu Abrahamu, 6 “Bwana, tusikilize. Wewe ni mtawala mkuu sana miongoni mwetu. Zika maiti wako katika kaburi unalolipenda kati ya makaburi yetu. Hakuna mtu wa kwetu atakayekuzuia kaburi lake ili kuzika maiti wako.”
7 Abrahamu akainuka na akasujudu mbele ya wenyeji wa nchi, yaani Wahiti. 8 Akawaambia, “Kama mnaniruhusu kumzika maiti wangu, basi nisikilizeni mkamsihi Efroni mwana wa Sohari kwa niaba yangu 9 ili aniuzie pango la Makpela, lililo mali yake, nalo liko mwisho wa shamba lake. Mwambieni aniuzie kwa bei kamili atakayosema ili liwe mahali pangu pa kuzikia miongoni mwenu.”
10 Efroni Mhiti alikuwa ameketi miongoni mwa watu wake, akamjibu Abrahamu mbele ya Wahiti wote waliokuwepo katika lango la mji. 11 “La hasha, bwana wangu, nisikilize, nakupa shamba, pia nakupa pango lililomo ndani yake. Nakupa mbele ya watu wangu. Uzike maiti wako.”
12 Abrahamu akasujudu tena, mbele ya wenyeji wa nchi, 13 akamwambia Efroni wale watu wakiwa wanasikia, “Tafadhali nisikilize. Nitakulipa fedha za hilo shamba. Kubali kuzipokea ili niweze kumzika maiti wangu.”
14 Efroni akamjibu Abrahamu, 15 “Nisikilize, bwana wangu, thamani ya ardhi hiyo ni shekeli 400 za fedha, lakini hiyo ni nini kati yako na mimi? Mzike maiti wako.”
16 Abrahamu akakubali masharti ya Efroni, akampimia ile fedha aliyotaja masikioni mwa Wahiti: Shekeli 400 za fedha kulingana na viwango vya uzito vilivyokuwa vikitumika wakati huo na wafanyabiashara.
17 Hivyo shamba la Efroni huko Makpela karibu na Mamre, yaani shamba pamoja na pango lililokuwamo, nayo miti yote iliyokuwamo ndani ya mipaka ya shamba hilo, vilikabidhiwa, 18 kwa Abrahamu kuwa mali yake mbele ya Wahiti wote waliokuwa wamekuja kwenye lango la mji. 19 Baada ya hayo Abrahamu akamzika Sara mkewe kwenye pango ndani ya shamba la Makpela karibu na Mamre (huko Hebroni) katika nchi ya Kanaani. 20 Hivyo Wahiti wakamkabidhi Abrahamu shamba pamoja na pango lililokuwa humo kuwa mahali pa kuzikia.
Familia ya Rebeka
20 Baada ya muda, Abrahamu akaambiwa, “Milka pia amepata watoto, amemzalia ndugu yako Nahori wana: 21 Usi mzaliwa wake wa kwanza, Buzi nduguye, Kemueli (baba wa Aramu), 22 Kesedi, Hazo, Pildashi, Yidlafu na Bethueli.” 23 Bethueli akamzaa Rebeka. Milka alimzalia Nahori nduguye Abrahamu hao wana wanane. 24 Suria wake Nahori aliyeitwa Reuma pia alikuwa na wana: Teba, Gahamu, Tahashi na Maaka.