Festo Anamweleza Agripa Mashtaka Dhidi ya Paulo

Festo anampa Agripa maelezo ya ajabu kuhusu mashtaka dhidi ya Paulo.

60 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Matendo 25:13–22

13 Baada ya siku kadhaa Mfalme Agripa na Bernike wakapanda kuja Kaisaria kumsalimu Festo. 14 Kwa kuwa walikuwa wakae huko Kaisaria kwa siku nyingi, Festo alijadili shauri la Paulo na mfalme, akisema, “Kuna mtu mmoja hapa ambaye Feliksi alimwacha gerezani. 15 Nilipokuwa huko Yerusalemu, viongozi wa makuhani na wazee wa Wayahudi walinijulisha habari zake na wakaomba hukumu dhidi yake.

16 “Lakini mimi nikawaambia kwamba si desturi ya Kirumi kumtoa mtu yeyote auawe kabla mshtakiwa kuonana uso kwa uso na washtaki wake, naye awe amepewa nafasi ya kujitetea kuhusu mashtaka anayoshutumiwa. 17 Hivyo walipokutana hapa, sikukawia, kesho yake niliitisha baraza, nikaketi penye kiti changu cha hukumu, nikaagiza huyo mtu aletwe. 18 Washtaki wake waliposimama, hawakushtaki kwa uhalifu wowote niliokuwa ninatarajia. 19 Badala yake walikuwa na vipengele fulani vya kutokukubaliana naye kuhusu dini yao na juu ya mtu mmoja aitwaye Yesu, ambaye alikufa, lakini yeye Paulo alidai kwamba yu hai. 20 Kwa kuwa sikujua jinsi ya kupeleleza jambo hili, nilimuuliza kama angependa kwenda Yerusalemu na kuhojiwa huko kuhusu mashtaka haya. 21 Lakini Paulo alipoomba afadhiliwe ili rufaa yake isikilizwe na Mfalme Agusto, nilimwamuru alindwe mpaka nitakapoweza kumpeleka kwa Kaisari.”

22 Ndipo Agripa akamwambia Festo, “Ningependa kumsikiliza mtu huyo mimi mwenyewe.”

Yeye akajibu, “Kesho utamsikia.”

Paulo Anajitetea Mbele ya Festo na Agripa

Paulo anatetea kesi yake mbele ya Festo na Agripa, na wanachofanya baada ya kuisikia.

Matendo 25:23–26:32

23 Siku iliyofuata Agripa na Bernike walifika kwa fahari kubwa wakaingia katika ukumbi wa mahakama, pamoja na majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa mji. Ndipo kwa amri ya Festo, Paulo akaletwa ndani. 24 Festo akasema, “Mfalme Agripa, nanyi nyote mlio hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu! Jumuiya yote ya Kiyahudi wamenilalamikia kuhusu mtu huyu huko Yerusalemu na hapa Kaisaria, wakipiga kelele kwamba haimpasi kuendelea kuishi. 25 Sikuona kwamba ametenda jambo lolote linalostahili kifo, ila kwa kuwa alikuwa ameomba rufaa yake kwa mfalme, niliamua kumpeleka Rumi. 26 Lakini mimi sina kitu maalum cha kumwandikia Bwana Mtukufu kumhusu mtu huyu. Kwa hiyo nimemleta mbele yenu ninyi nyote, hasa mbele yako, Mfalme Agripa, ili kutokana na matokeo ya uchunguzi huu, niweze kupata kitu cha kuandika. 27 Kwa kuwa naona hakuna sababu ya kumpeleka mfungwa bila kuainisha mashtaka dhidi yake.”

26:1 Ndipo Agripa akamwambia Paulo, “Unayo ruhusa kujitetea.”

Hivyo Paulo akawaashiria kwa mkono wake, akaanza kujitetea, akasema: 2 “Mfalme Agripa, najiona kuwa na heri kusimama mbele yako leo ninapojitetea kuhusu mashtaka yote ya Wayahudi, 3 hasa kwa sababu unajua vyema desturi zote za Kiyahudi na ya kuwa wewe unajua kwa undani mila na masuala ya mabishano. Kwa hiyo, nakusihi unisikilize kwa uvumilivu.

4 “Wayahudi wote wanajua jinsi nilivyoishi tangu nilipokuwa mtoto, kuanzia mwanzo wa maisha yangu katika nchi yangu na pia huko Yerusalemu. 5 Wao wamefahamu kwa muda mrefu na wanaweza kushuhudia kama wakipenda, ya kwamba kutokana na misimamo mikali sana ya dhehebu letu kwenye dini yetu, niliishi nikiwa Farisayo. 6 Nami sasa ni kwa sababu ya tumaini langu katika kile ambacho Mungu aliwaahidi baba zetu, ninashtakiwa leo. 7 Hii ndiyo ahadi ambayo makabila yetu kumi na mawili yanatarajia kuiona ikitimizwa wanapomtumikia Mungu kwa bidii usiku na mchana. Ee mfalme, ninashtakiwa na Wayahudi kwa ajili ya tumaini hili. 8 Kwa nini yeyote miongoni mwenu afikiri kwamba ni jambo lisilosadikika Mungu kufufua wafu?

9 “Mimi pia nilikuwa nimeshawishika kwamba imenipasa kufanya yote yale yaliyowezekana kupinga Jina la Yesu wa Nazareti. 10 Nami hayo ndiyo niliyoyafanya huko Yerusalemu. Kwa mamlaka ya viongozi wa makuhani, niliwatia wengi wa watakatifu gerezani na walipokuwa wakiuawa, nilipiga kura yangu kuunga mkono. 11 Mara nyingi nilikwenda kutoka sinagogi moja hadi ingine nikiamuru waadhibiwe, nami nilijaribu kuwalazimisha wakufuru. Katika shauku yangu dhidi yao, hata nilikwenda miji ya kigeni ili kuwatesa.

12 “Siku moja nilipokuwa katika mojawapo ya safari hizi nikiwa ninakwenda Dameski, nilikuwa na mamlaka na agizo kutoka kwa kiongozi wa makuhani. 13 Ilikuwa yapata adhuhuri, ee mfalme, nilipokuwa njiani, niliona nuru kutoka mbinguni kali kuliko jua, ikingʼaa kunizunguka pande zote mimi na wale niliokuwa pamoja nao. 14 Wote tulipokuwa tumeanguka chini, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya Kiebrania, ‘Sauli, Sauli, mbona unanitesa? Ni vigumu kwako kuupiga teke mchokoo.’

15 “Nikauliza, ‘Ni nani wewe, Bwana?’

“Naye Bwana akajibu, ‘Ni Mimi Yesu unayemtesa. 16 Sasa inuka usimame kwa miguu yako. Nimekutokea ili nikuteue uwe mtumishi na shahidi wa mambo ambayo umeyaona, na yale nitakayokuonyesha. 17 Nitakuokoa kutoka kwa watu wako na watu wa Mataifa ambao ninakutuma kwao, 18 uyafumbue macho yao ili wageuke kutoka gizani waingie nuruni, na kutoka kwenye nguvu za Shetani wamgeukie Mungu, ili wapate msamaha wa dhambi na sehemu miongoni mwa wale waliotakaswa kwa kuniamini mimi.’

19 “Hivyo basi, Mfalme Agripa, sikuacha kuyatii yale maono yaliyotoka mbinguni, 20 bali niliyatangaza kwanza kwa wale wa Dameski, kisha Yerusalemu na katika vijiji vyote vya Uyahudi na pia kwa watu wa Mataifa, kwamba inawapasa kutubu na kumgeukia Mungu na kuthibitisha toba yao kwa matendo yao. 21 Ni kwa sababu hii Wayahudi walinikamata nilipokuwa Hekaluni, wakataka kuniua. 22 Hadi leo nimepata msaada kutoka kwa Mungu, na hivyo nasimama hapa nikishuhudia kwa wakubwa na wadogo. Sisemi chochote zaidi ya yale ambayo manabii na Mose walisema yatatukia: 23 kwamba Kristo atateswa, na kwamba yeye atakuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu, na atatangaza nuru kwa watu wake na kwa watu wa Mataifa.”

24 Paulo alipokuwa akifanya utetezi huu, Festo akasema kwa sauti kubwa, “Paulo, wewe umerukwa na akili! Kusoma kwingi kunakufanya uwe kichaa!”

25 Lakini Paulo akajibu, “Mimi sijarukwa na akili, mtukufu sana Festo, bali nanena kweli nikiwa na akili zangu timamu. 26 Naam, Mfalme anajua kuhusu mambo haya yote, nami nasema naye kwa uhuru. Kwa sababu nina hakika kwamba hakuna hata mojawapo ya mambo haya asilolijua, kwa kuwa hayakufanyika mafichoni. 27 Mfalme Agripa, je, unaamini manabii? Najua kuwa unaamini.”

28 Agripa akamwambia Paulo, “Je, unanishawishi kwa haraka namna hii niwe Mkristo?”

29 Paulo akasema, “Ikiwa ni kwa haraka au la, namwomba Mungu, si wewe peke yako bali pia wale wote wanaonisikiliza leo, wawe kama mimi nilivyo, kasoro minyororo hii.”

30 Baada ya kusema hayo, mfalme akainuka pamoja na mtawala na Bernike na wale waliokuwa wameketi pamoja nao. 31 Walipokuwa wakiondoka, wakaambiana, “Mtu huyu hafanyi jambo lolote linalostahili kufa au kufungwa.”

32 Agripa akamwambia Festo, “Mtu huyu angeachwa huru kama hangekuwa amekata rufaa kwa Kaisari.”

Paulo Anakabidhiwa kwa Akida

Paulo anakabidhiwa kwa akida akiwa mfungwa, na hivyo anazuiwa kukamilisha safari hii kwa kurudi Antiokia, kama alivyokuwa akifanya kwa kawaida.

Matendo 27:1

1 Ilipoamuliwa kwamba tungesafiri kwa njia ya bahari kwenda Italia, Paulo na wafungwa wengine wakakabidhiwa kwa kiongozi mmoja wa askari aliyeitwa Juliasi, aliyekuwa wa Kikosi cha Walinzi wa Kaisari.