Eliya Achukuliwa Kwenda Mbinguni
896 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Wakati Bwana alipokuwa karibu kumchukua Eliya mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Eliya na Elisha walikuwa njiani wakitoka Gilgali. 2 Eliya akamwambia Elisha, “Kaa hapa. Bwana amenituma Betheli.”
Lakini Elisha akasema, “Kwa hakika, kama Bwana aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Kwa hiyo wakaenda Betheli pamoja.
3 Wana wa manabii waliokuwako huko Betheli wakamjia Elisha na kumuuliza, “Je, unajua ya kwamba Bwana atakuondolea bwana wako leo?”
Elisha akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze juu ya jambo hilo.”
4 Kisha Eliya akamwambia, “Baki hapa, Elisha. Bwana amenituma Yeriko.”
Naye akajibu, “Kwa hakika kama Bwana aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wakaenda Yeriko.
5 Wana wa manabii waliokuwako huko Yeriko wakamwendea Elisha na kumuuliza, “Je, unajua ya kwamba Bwana atakuondolea bwana wako leo?”
Akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze juu ya jambo hilo.”
6 Kisha Eliya akamwambia, “Kaa hapa. Bwana amenituma kwenda Yordani.”
Naye akamjibu, “Kwa hakika kama Bwana aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wote wawili wakaendelea pamoja.
7 Wana hamsini wa manabii wakaenda na kusimama kwa mbali, kuelekea mahali ambapo Eliya na Elisha walikuwa wamesimama kando ya Mto Yordani. 8 Eliya akachukua vazi lake, akalisokota na kupiga nalo maji. Maji yakagawanyika upande wa kuume na upande wa kushoto, nao wawili wakavuka pakavu.
9 Walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, “Niambie, nikufanyie nini kabla sijaondolewa kutoka kwako?”
Elisha akajibu, “Naomba nirithi sehemu maradufu ya roho yako.”
10 Eliya akasema, “Umeomba jambo gumu. Lakini kama utaniona wakati ninapoondolewa kutoka kwako litakuwa lako. La sivyo, hautalipata.”
11 Walipokuwa wakitembea pamoja na kuzungumza, ghafula gari la moto na farasi wa moto vilitokea na kuwatenganisha wao wawili, naye Eliya akapanda mbinguni katika upepo wa kisulisuli. 12 Elisha aliona hili, naye akapaza sauti, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya Israeli na wapanda farasi wake!” Naye Elisha hakumwona tena. Kisha akazishika nguo zake mwenyewe na kuzirarua.
13 Akaliokota lile vazi lililoanguka kutoka kwa Eliya, kisha akarudi na kusimama ukingoni mwa Yordani. 14 Ndipo akalichukua lile vazi ambalo lilikuwa limeanguka kutoka kwa Eliya, naye akayapiga yale maji nalo. Akauliza, “Yuko wapi sasa Bwana, Mungu wa Eliya?” Elisha alipoyapiga maji, yakagawanyika kulia na kushoto, naye akavuka.
15 Wale wana wa manabii kutoka Yeriko waliokuwa wakitazama wakasema, “Roho wa Eliya inamkalia Elisha.” Nao wakaenda kumlaki na kusujudu hadi nchi mbele yake. 16 Wakasema, “Tazama, sisi watumishi wako tunao watu hamsini wenye uwezo. Waruhusu waende kumtafuta bwana wako. Labda Roho wa Bwana amemtwaa na kumweka katika mlima fulani au bonde fulani.”
Elisha akajibu, “Hapana, msiwatume.”
17 Lakini wakasisitiza, mpaka akaona aibu kuwakatalia. Hivyo akasema, “Watumeni.” Nao wakawatuma watu hamsini, wakamtafuta kwa siku tatu, lakini hawakumpata. 18 Walipomrudia Elisha, ambaye alikuwa akingojea huko Yeriko, akawaambia, “Je, sikuwaambia msiende?”
19 Watu wa mji wakamwambia Elisha, “Tazama, bwana wetu, mahali mji huu ulipojengwa ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo, lakini maji yake ni mabaya, na nchi haizai.”
20 Akasema, “Nileteeni bakuli mpya, mweke chumvi ndani yake.” Kwa hiyo wakamletea.
21 Kisha akaenda kwenye chemchemi na kuitupa ile chumvi ndani yake, akisema, “Hili ndilo asemalo Bwana: ‘Nimeyaponya maji haya. Kamwe hayatasababisha mauti tena wala kutozaa.’ ” 22 Nayo yale maji yakaponywa mpaka leo, sawasawa na neno la Elisha alilokuwa amesema.
23 Kutoka huko Elisha akakwea kwenda Betheli. Ikawa alipokuwa akitembea barabarani, baadhi ya vijana wakatoka mjini na kumfanyia mzaha. Wakasema, “Paa, wewe mwenye upaa! Paa, wewe mwenye upaa!” 24 Akageuka, akawatazama na kuwalaani kwa Jina la Bwana. Kisha dubu wawili wa kike wakatokea mwituni na kuwararua vijana arobaini na wawili miongoni mwao. 25 Naye akaondoka huko, akaenda Mlima Karmeli, na kutoka huko akarudi Samaria.
Yehoramu Awashinda Wamoabu 895 KK
6 Kwa hiyo wakati ule Mfalme Yehoramu akaondoka kutoka Samaria na kukusanya Israeli yote tayari kwenda vitani. 7 Akapeleka pia ujumbe ufuatao kwa Yehoshafati mfalme wa Yuda: “Mfalme wa Moabu ameasi dhidi yangu. Je, utakwenda pamoja nami kupigana dhidi ya Moabu?”
Akajibu, “Nitakwenda pamoja nawe. Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako.”
8 Akauliza, “Je, tutashambulia kupitia njia gani?”
Akajibu, “Kupitia Jangwa la Edomu.”
9 Hivyo mfalme wa Israeli akaondoka akiwa pamoja na mfalme wa Yuda na mfalme wa Edomu. Baada ya kuzunguka kwa siku saba, jeshi likawa limeishiwa maji kwa matumizi yao na kwa ajili ya wanyama waliokuwa nao.
10 Mfalme wa Israeli akamaka, “Nini! Je, Bwana ametuita sisi wafalme watatu ili tu kututia mikononi mwa Moabu?”
11 Lakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii wa Bwana hapa, ili tuweze kumuuliza Bwana kupitia kwake?”
Afisa mmoja wa mfalme wa Israeli akajibu, “Elisha mwana wa Shafati yuko hapa. Ndiye alikuwa akimimina maji juu ya mikono ya Eliya.”
12 Yehoshafati akasema, “Neno la Bwana liko pamoja naye.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli na Yehoshafati pamoja na mfalme wa Edomu wakamwendea.
13 Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, “Nina nini mimi nawe? Nenda kwa manabii wa baba yako na manabii wa mama yako.”
Mfalme wa Israeli akajibu, “La hasha, kwa sababu ni Bwana ambaye ametuita pamoja sisi wafalme watatu ili atutie mikononi mwa Moabu.”
14 Elisha akasema, “Hakika, kama Bwana Mwenye Nguvu Zote aishivyo ambaye ninamtumikia, kama si kuheshimu Yehoshafati mfalme wa Yuda, nisingekutazama wala hata kukutupia jicho. 15 Lakini sasa, nileteeni mpiga kinubi.”
Mpiga kinubi alipokuwa akipiga, mkono wa Bwana ukaja juu ya Elisha, 16 naye akasema, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana, ‘Chimbeni bonde hili lijae mahandaki.’ 17 Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo Bwana: Hamtaona upepo wala mvua, lakini bonde hili litajaa maji, nanyi pamoja na ngʼombe wenu na wanyama wenu wengine mtakunywa. 18 Hili ni jambo rahisi machoni pa Bwana. Pia ataitia Moabu mikononi mwenu. 19 Mtaushinda kila mji wenye ngome na kila mji mkubwa. Mtakata kila mti ulio mzuri, mtaziba chemchemi zote, na kuharibu kila shamba zuri kwa mawe.”
20 Kesho yake asubuhi, karibu na wakati wa kutoa dhabihu ya asubuhi, tazama, maji yakawa yanatiririka kutoka upande wa Edomu! Nayo nchi ikajaa maji.
21 Basi Wamoabu wote walikuwa wamesikia kuwa wale wafalme wamekuja kupigana dhidi yao. Hivyo kila mtu, kijana na mzee, ambaye angeweza kushika silaha akaitwa na kuwekwa mpakani. 22 Walipoamka asubuhi na mapema, jua likawa linamulika juu ya maji. Wamoabu waliokuwa upande wa pili wakaona maji ni mekundu, kama damu. 23 Wamoabu wakasema, “Ile ni damu! Lazima hao wafalme wamepigana na kuchinjana wao kwa wao. Sasa Moabu, twendeni tukateke nyara!”
24 Lakini Wamoabu walipofika kwenye kambi ya Israeli, Waisraeli wakainuka na kuwapiga mpaka wakakimbia. Nao Waisraeli wakaivamia nchi na kuwachinja Wamoabu. 25 Wakaiharibu miji, kila mtu akatupa jiwe juu ya kila shamba zuri mpaka likafunikwa. Wakaziba chemchemi zote na kukata kila mti mzuri. Kir-Haresethi peke yake ndio uliobaki na mawe yake yakiwa mahali pake. Lakini hata hivyo watu waliokuwa na makombeo wakauzunguka na kuushambulia vilevile.
26 Mfalme wa Moabu alipoona kuwa vita vimekuwa vikali dhidi yake, akachukua watu 700 wenye panga ili kuingia kwa mfalme wa Edomu, lakini wakashindwa. 27 Ndipo akamchukua mwanawe mzaliwa wake wa kwanza, ambaye angekuwa mfalme baada yake, akamtoa kama dhabihu ya kuteketezwa juu ya ukuta wa mji. Ghadhabu ikawa kubwa dhidi ya Israeli; wakajiondoa kwake na kurudi katika nchi yao wenyewe.