Elihu Asema Mateso Hutoka kwa Mungu (continued)

Elihu, ambaye alikuwa amenyamaza hadi sasa, anaingia katika mabishano. Anaonyesha kwamba Mungu hutuma mateso kwa makusudi yenye hekima, ingawa hatuwezi kuyafahamu kikamilifu, na kwamba wajibu wa mwanadamu ni kunyenyekea.

2130 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ayubu 36–37

1 Elihu akaendelea kusema:

2 “Nivumilie kidogo zaidi nami nitakuonyesha

kwamba yako mengi zaidi ya kusemwa kwa ajili ya Mungu.

3 Ninayapata maarifa yangu kutoka mbali,

nami nitamhesabia haki Muumba wangu.

4 Uwe na hakika kwamba maneno yangu si ya uongo;

mmoja aliye mkamilifu katika maarifa yuko pamoja na wewe.

5 “Mungu ni mwenye nguvu, lakini hamdharau mwanadamu;

ni mwenye nguvu, naye ni thabiti katika shauri lake.

6 Hawaachi waovu waendelee kuishi,

bali huwapa walioteswa haki yao.

7 Yeye haondoi macho yake kwa wenye haki;

huwaketisha penye viti vya enzi pamoja na wafalme

na kuwatukuza milele.

8 Lakini ikiwa watu wamefungwa kwenye minyororo,

wakiwa wameshikiliwa na kamba za mateso,

9 huwaonyesha yale waliyoyatenda,

kwamba wametenda dhambi kwa majivuno.

10 Huwafanya wao kusikia maonyo,

na huwaagiza kutubu uovu wao.

11 Kama wakitii na kumtumikia,

wataishi siku zao zilizobaki katika mafanikio,

na miaka yao katika utoshelevu.

12 Lakini wasiposikiliza,

wataangamia kwa upanga,

nao watakufa pasipo maarifa.

13 “Wasiomcha Mungu moyoni mwao huficha chuki;

hata anapowafunga, hawamwombi msaada.

14 Wanakufa wangali vijana,

miongoni mwa wanaume hanithi wa mahali pa kuabudia miungu.

15 Bali wao wanaoteseka huwaokoa katika mateso yao,

na kuzungumza nao katika dhiki zao.

16 “Yeye anakubembeleza utoke katika mataya ya dhiki,

ili kukuweka mahali palipo na nafasi mbali na kizuizi,

hadi kwenye meza yako ya faraja iliyojaa vyakula vizuri.

17 Lakini sasa umelemewa na hukumu kwa ajili ya uovu;

hukumu na haki vimekukamata.

18 Uwe mwangalifu ili yeyote asikushawishi kwa utajiri;

usipotoshwe kwa fungu kubwa la rushwa.

19 Je, utajiri wako hata nguvu zako nyingi

vinaweza kukusaidia usiingie kwenye dhiki?

20 Usiutamani usiku uje,

ili uwaburute watu mbali na nyumba zao.

21 Jihadhari usigeukie uovu,

ambao unaupenda zaidi kuliko mateso.

22 “Mungu ametukuzwa katika nguvu zake.

Ni nani aliye mwalimu kama yeye?

23 Ni nani aliyemwelekeza katika njia zake,

au kumwambia, ‘Wewe umetenda yasiyo sawa’?

24 Kumbuka kuzitukuza kazi zake,

ambazo watu wamezisifu katika wimbo.

25 Wanadamu wote wameiona;

watu wanaikazia macho kwa mbali.

26 Tazama jinsi Mungu alivyo mkuu,

kupita ufahamu wetu!

Hesabu ya miaka yake haitafutiki.

27 “Yeye huvuta juu matone ya maji,

ayachujayo kama mvua kutoka kwenye vijito;

28 mawingu huangusha chini maji yake,

nayo mvua nyingi huwanyeshea wanadamu.

29 Ni nani ajuaye jinsi ayatandazavyo mawingu,

jinsi angurumavyo kutoka hemani mwake.

30 Tazama jinsi anavyotandaza umeme wa radi kumzunguka,

naye huvifunika vilindi vya bahari.

31 Hivi ndivyo atawalavyo mataifa,

na kuwapa chakula kwa wingi.

32 Huujaza mkono wake kwa umeme wa radi,

na kuuagiza kulenga shabaha yake.

33 Ngurumo zake hutangaza dhoruba inayokuja;

hata mifugo hujulisha kukaribia kwake.

37:1 “Kwa hili moyo wangu unatetemeka,

nao unaruka kutoka mahali pake.

2 Sikiliza! Sikiliza ngurumo ya sauti yake,

sauti ya ngurumo itokayo kinywani mwake.

3 Huuachilia umeme wake wa radi chini ya mbingu yote

na kuupeleka hata miisho ya dunia.

4 Baada ya hayo huja sauti ya ngurumo yake;

Mungu hunguruma kwa sauti yake ya fahari.

Wakati sauti yake ingurumapo tena,

huuachilia umeme wake wa radi.

5 Sauti ya Mungu hunguruma kwa namna za ajabu;

yeye hutenda mambo makuu kupita ufahamu wetu.

6 Huiambia theluji, ‘Anguka juu ya dunia,’

nayo manyunyu ya mvua, ‘Uwe mvua ya nguvu.’

7 Ili wanadamu wote aliowaumba wapate kujua kazi zake,

yeye humzuilia kila mtu shughuli zake.

8 Wanyama hujificha;

hubakia kwenye mapango yao.

9 Dhoruba hutoka katika chumba chake,

baridi hutoka katika upepo uendao kasi.

10 Pumzi ya Mungu hutoa barafu,

eneo kubwa la maji huganda.

11 Huyasheheneza mawingu kwa maji,

naye husambaza umeme wake wa radi kupitia hayo.

12 Nayo mawingu huzungukazunguka pande zote kwa amri yake,

juu ya uso wa dunia yote,

kufanya lolote ayaamuruyo.

13 Huleta mawingu ili kuadhibu wanadamu,

au kuinyeshea dunia yake na kuonyesha upendo wake.

14 “Ayubu, sikiliza hili;

nyamaza na uyafikiri maajabu ya Mungu.

15 Je, unajua jinsi Mungu anavyoyaongoza mawingu,

na kufanya umeme wake wa radi utoe mwanga?

16 Je, wajua jinsi mawingu yanavyokaa yakiwa yametulia,

hayo maajabu yake yeye aliye mkamilifu katika maarifa?

17 Wewe unayeshindwa na joto katika nguo zako

wakati nchi imenyamazishwa kimya bila upepo wa kusini,

18 je, waweza kuungana naye katika kuzitandaza anga,

zilizo ngumu kama kioo cha shaba ya kuyeyushwa?

19 “Tuambieni yatupasayo kumwambia;

hatuwezi kutayarisha shauri letu kwa sababu ya ujinga wetu.

20 Je, aambiwe kwamba nataka kuongea?

Je, yuko mtu ambaye angeomba kumezwa?

21 Basi hakuna awezaye kulitazama jua,

jinsi linavyongʼaa angani,

upepo ukishafagia mawingu.

22 Kutoka kaskazini yeye huja na fahari kuu;

Mungu huja katika utukufu wa kutisha.

23 Yeye Mwenyezi hatuwezi kumfikia, naye ametukuzwa katika uweza;

katika hukumu zake na haki yake kuu, hataonea.

24 Kwa hiyo, wanadamu mheshimuni,

kwa kuwa yeye hamstahi yeyote anayejidhania kuwa ana hekima.”