Uzinzi wa Daudi (continued)
1035 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Zaburi ya Daudi.
1 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Vyote vilivyomo ndani yangu
vilihimidi jina lake takatifu.
2 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
wala usisahau wema wake wote,
3 akusamehe dhambi zako zote,
akuponya magonjwa yako yote,
4 aukomboa uhai wako na kaburi,
akuvika taji ya upendo na huruma,
5 atosheleza mahitaji yako kwa vitu vyema,
ili ujana wako uhuishwe kama wa tai.
6 Bwana hutenda haki,
naye huwapa hukumu ya haki wote wanaoonewa.
7 Alijulisha Mose njia zake,
na wana wa Israeli matendo yake.
8 Bwana ni mwingi wa huruma na mwenye neema;
si mwepesi wa hasira, bali amejaa upendo.
9 Yeye hatalaumu siku zote,
wala haweki hasira yake milele,
10 yeye hatutendei kulingana na dhambi zetu
wala hatupatilizi kwa kadiri ya maovu yetu.
11 Kama vile mbingu zilivyo juu ya dunia sana,
ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha;
12 kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
ndivyo Mungu alivyoziweka dhambi zetu mbali nasi.
13 Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake,
ndivyo Bwana anavyowahurumia wale wanaomcha;
14 kwa kuwa anajua tulivyoumbwa,
anakumbuka kwamba sisi tu mavumbi.
15 Kuhusu mwanadamu, siku zake ni kama majani,
anachanua kama ua la shambani;
16 upepo huvuma juu yake nalo hutoweka,
mahali pake hapalikumbuki tena.
17 Lakini kutoka milele hata milele
upendo wa Bwana uko kwa wale wamchao,
nayo haki yake kwa watoto wa watoto wao:
18 kwa wale walishikao agano lake
na kukumbuka kuyatii mausia yake.
19 Bwana ameweka imara kiti chake cha enzi mbinguni,
ufalme wake unatawala juu ya vyote.
20 Mhimidini Bwana, enyi malaika zake,
ninyi mlio mashujaa mnaozitii amri zake,
ninyi mnaotii neno lake.
21 Mhimidini Bwana, ninyi jeshi lake lote la mbinguni,
ninyi watumishi wake mnaofanya mapenzi yake.
22 Mhimidini Bwana, kazi zake zote
kila mahali katika milki yake.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
16 Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto. Akafunga na akaingia ndani ya nyumba yake akawa siku zote analala sakafuni usiku kucha. 17 Wazee wa nyumbani mwake wakamwendea wakasimama karibu naye ili kumwamsha kutoka pale sakafuni, lakini akakataa, wala hakula chochote pamoja nao.
18 Kunako siku ya saba yule mtoto akafa. Watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia kuwa mtoto amekufa, kwa maana walifikiri, “Wakati mtoto alipokuwa angali hai, tulizungumza na Daudi lakini hakutusikiliza. Tutawezaje kumwambia kwamba mtoto amekufa? Anaweza kufanya kitu cha kujidhuru.”
19 Daudi akaona kuwa watumishi wake wananongʼonezana wenyewe, naye akatambua kuwa mtoto alikuwa amekufa. Akauliza “Je, ni kwamba huyo mtoto amekufa?”
Wakamjibu, “Ndiyo, mtoto amekufa.”
20 Basi Daudi akainuka kutoka pale sakafuni. Baada ya kuoga, akajipaka mafuta na kubadilisha nguo zake kisha akaenda ndani ya nyumba ya Bwana, akaabudu. Baada ya hapo akaenda nyumbani kwake kwa kutaka kwake, wakamwandalia chakula, naye akala.
21 Watumishi wake wakamuuliza, “Kwa nini unafanya hivi? Mtoto alipokuwa angali hai, ulifunga na kulia; lakini sasa mtoto amekufa, umeinuka na kula.”
22 Akajibu, “Wakati mtoto alipokuwa bado yungali hai, nilifunga na kulia. Nilifikiri, ‘Nani ajuaye? Bwana aweza kunirehemu ili kumwacha mtoto aishi.’ 23 Lakini sasa kwa kuwa amekufa, kwa nini nifunge? Je, naweza kumrudisha tena? Mimi nitakwenda kwake, lakini yeye hatanirudia mimi.”
26 Wakati huo Yoabu akapigana dhidi ya Raba jamii ya Waamoni na kuteka ngome la kifalme. 27 Kisha Yoabu akatuma wajumbe kwa Daudi, kusema, “Nimepigana dhidi ya Raba, nami nimetwaa chanzo chake cha maji. 28 Sasa kusanya vikosi vilivyobaki na ukauzingire mji kwa jeshi na kuuteka. La sivyo, nitauteka mimi, nao utaitwa kwa jina langu.”
29 Kwa hiyo Daudi akakusanya jeshi lote akaenda Raba, akaushambulia na kuuteka. 30 Akachukua taji kutoka kwa kichwa cha mfalme wao, lililokuwa na uzito wa talanta moja ya dhahabu, nayo ilizungushiwa vito vya thamani. Ikawekwa juu ya kichwa cha Daudi. Alichukua nyara nyingi kutoka mjini huo. 31 Akawatoa watu waliokuwa humo, akawaweka wafanye kazi kwa misumeno, sululu za chuma na mashoka, naye akawaweka kwenye kazi ya kutengeneza matofali. Akafanya hivi kwa miji yote ya Waamoni. Kisha Daudi na jeshi lake lote wakarudi Yerusalemu.
2 Daudi akachukua taji kutoka kwa kichwa cha mfalme wao, lililokuwa na uzito wa talanta moja ya dhahabu, nayo ilizungushiwa vito vya thamani. Ikawekwa juu ya kichwa cha Daudi. Alichukua nyara nyingi kutoka mjini huo. 3 Akawatoa watu waliokuwa humo, akawaweka wafanye kazi kwa misumeno, sululu za chuma na mashoka. Daudi akafanya hivi kwa miji yote ya Waamoni. Kisha Daudi na jeshi lake lote wakarudi Yerusalemu.