Daudi Hadi Alipokimbia kutoka Makao ya Kifalme ya Sauli (continued)
1063 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Sauli akamwambia mwanawe Yonathani na watumishi wake wote wamuue Daudi. Lakini Yonathani mwana wa Sauli alimpenda sana Daudi. 2 Yonathani akamwonya Daudi, akisema, “Baba yangu Sauli anatafuta nafasi ya kukuua. Ujilinde kesho asubuhi, nenda mahali pa siri na ukae huko. 3 Nitatoka na kukaa na baba yangu shambani mahali uliko. Nitazungumza naye juu yako, nami nitakueleza nitakachogundua.”
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
1 Kwa Bwana ninakimbilia,
unawezaje basi kuniambia:
“Ruka kama ndege kwenye mlima wako.
2 Hebu tazama, waovu wanapinda pinde zao,
huweka mishale kwenye uzi wake,
wakiwa gizani ili kuwapiga
wale wanyofu wa moyo.
3 Wakati misingi imeharibiwa,
mwenye haki anaweza kufanya nini?”
4 Bwana yuko ndani ya Hekalu lake takatifu;
Bwana yuko kwenye kiti chake cha enzi mbinguni.
Huwaangalia wana wa watu,
macho yake yanawajaribu.
5 Bwana huwajaribu wenye haki,
lakini waovu na wanaopenda jeuri,
nafsi yake huwachukia.
6 Atawanyeshea waovu makaa ya moto mkali
na kiberiti kinachowaka,
upepo wenye joto kali ndio fungu lao.
7 Kwa kuwa Bwana ni mwenye haki,
yeye hupenda haki.
Wanyofu watauona uso wake.
4 Yonathani akanena mema juu ya Daudi kwa Sauli baba yake na kumwambia, “Mfalme asitende mabaya kwa mtumishi wake Daudi; hajakukosea, aliyoyafanya yamekuwa ya faida sana kwako. 5 Alihatarisha maisha yake alipomuua yule Mfilisti. Bwana akajipatia ushindi mkubwa kwa ajili ya Israeli wote, nawe uliuona na ukafurahi. Kwa nini basi utende mabaya kwa mtu asiye na hatia kama Daudi kwa kumuua bila sababu?”
6 Sauli akamsikiliza Yonathani na kuapa hivi: “Hakika kama Bwana aishivyo, Daudi hatauawa.”
7 Basi Yonathani akamwita Daudi na kumweleza mazungumzo yote. Akamleta kwa Sauli, naye Daudi akawa pamoja na Sauli kama kwanza.
8 Vita vilitokea tena, naye Daudi akatoka na kupigana na Wafilisti. Akawapiga kwa nguvu nyingi hata wakakimbia mbele yake.
9 Lakini roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Bwana ikaja juu ya Sauli alipokuwa ameketi katika nyumba yake akiwa na mkuki mkononi mwake. Daudi alipokuwa anampigia kinubi, 10 Sauli akajaribu kumchomea Daudi ukutani kwa huo mkuki wake, lakini Daudi akauhepa huo mkuki wa Sauli ukakita ukutani. Usiku ule ule Daudi akakimbia na kuokoka.
11 Sauli akatuma watu nyumbani mwa Daudi wailinde hiyo nyumba na kumuua asubuhi. Lakini Mikali, mkewe Daudi, akamwonya akisema, “Kama hukukimbia kuokoa maisha yako usiku huu, kesho yake utauawa.” 12 Basi Mikali akamteremsha Daudi kupitia dirishani, naye akakimbia na kuokoka. 13 Kisha Mikali akachukua kinyago, akakilaza kitandani, akakifunika kwa vazi na kukiwekea singa za mbuzi kichwani.
14 Sauli alipotuma watu kumkamata Daudi, Mikali akasema, “Yeye ni mgonjwa.”
15 Kisha Sauli akatuma watu tena kumwona Daudi naye akawaambia, “Mleteni kwangu juu ya kitanda chake ili nipate kumuua.” 16 Lakini wale watu walipoingia, kumbe ni kinyago tu kilichokuwa kitandani na kwenye kichwa kulikuwepo na singa za mbuzi.
17 Sauli akamwambia Mikali, “Kwa nini umenidanganya mimi hivi na kumwacha adui yangu aende zake ili apate kuokoka?”
Mikali akamwambia, “Yeye aliniambia, ‘Niache niende zangu. Kwa nini nikuue?’ ”
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi. Wakati Sauli alipotuma wapelelezi nyumbani mwa Daudi ili wamuue.
1 Ee Mungu, uniokoe na adui zangu,
unilinde kutokana na hao wanaoinuka dhidi yangu.
2 Uniponye na watu watendao mabaya,
uniokoe kutokana na wamwagao damu.
3 Tazama wanavyonivizia!
Watu wakali wananifanyia hila,
ingawa Ee Bwana, mimi sijakosea
wala kutenda dhambi.
4 Sijatenda kosa; hata hivyo wako tayari kunishambulia.
Inuka unisaidie, uone hali yangu mbaya!
5 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli!
Zinduka uyaadhibu mataifa yote,
usionyeshe huruma kwa wasaliti.
6 Hurudi wakati wa jioni,
wakibweka kama mbwa,
wakiuzurura mji.
7 Tazama yale wanayotema kutoka vinywa vyao,
hutema upanga kutoka midomo yao,
nao husema, “Ni nani atakayetusikia?”
8 Lakini wewe, Bwana, uwacheke;
unayadharau mataifa hayo yote.
9 Ee nguvu yangu, ninakutazama wewe,
wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,
10 Mungu wangu unipendaye.
Mungu atanitangulia,
naye atanifanya niwachekelee
wale wanaonisingizia.
11 Lakini usiwaue, Ee Bwana, ngao yetu,
au sivyo watu wangu watasahau.
Katika uwezo wako wafanye watangetange
na uwashushe chini.
12 Kwa ajili ya dhambi za vinywa vyao,
kwa ajili ya maneno ya midomo yao,
waache wanaswe katika kiburi chao.
Kwa ajili ya laana na uongo wanaotamka,
13 wateketeze katika ghadhabu,
wateketeze hadi wasiwepo tena.
Ndipo itakapofahamika katika miisho ya dunia
kwamba Mungu anatawala juu ya Yakobo.
14 Hurudi jioni,
wakibweka kama mbwa,
wakiuzurura mji.
15 Wanatangatanga wakitafuta chakula,
wasipotosheka hubweka kama mbwa.
16 Lakini mimi nitaziimba nguvu zako,
asubuhi nitaimba juu ya upendo wako;
kwa maana wewe ndiwe ngome yangu
na kimbilio langu wakati wa shida.
17 Ee uliye Nguvu zangu, ninakuimbia sifa.
Wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,
Mungu unipendaye.