Daudi Anamshinda Goliathi (continued)

1063 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Samweli 18:1–4

1 Baada ya Daudi kumaliza kuongea na Sauli, roho ya Yonathani ikaambatana na roho ya Daudi, naye akampenda kama nafsi yake mwenyewe. 2 Kuanzia siku ile Sauli akamchukua Daudi naye hakumruhusu kurudi nyumbani kwa baba yake. 3 Yonathani akafanya agano na Daudi kwa sababu alimpenda kama nafsi yake mwenyewe. 4 Yonathani akavua joho alilokuwa amevaa na kumpa Daudi, pamoja na koti lake, silaha zake, hata pamoja na upanga wake, upinde wake na mshipi wake.

Zaburi Kuhusu Ushindi dhidi ya Goliathi

Zaburi 9

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa muth-labeni. Zaburi ya Daudi.

1 Ee Bwana, nitakutukuza kwa moyo wangu wote,

nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu.

2 Nitafurahi na kushangilia ndani yako.

Nitaliimbia sifa jina lako, Ewe Uliye Juu Sana.

3 Adui zangu wamerudi nyuma,

wamejikwaa na kuangamia mbele zako.

4 Kwa maana umetetea haki yangu na msimamo wangu;

umeketi kwenye kiti chako cha enzi,

ukihukumu kwa haki.

5 Umekemea mataifa na kuwaangamiza waovu;

umeyafuta majina yao milele na milele.

6 Uharibifu usiokoma umempata adui,

umeingʼoa miji yao;

hata kumbukumbu lao limetoweka.

7 Bwana anatawala milele,

ameweka kiti chake cha enzi apate kuhukumu.

8 Mungu atahukumu ulimwengu kwa haki,

atatawala mataifa kwa haki.

9 Bwana ni kimbilio la watu wanaoonewa,

ni ngome imara wakati wa shida.

10 Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe,

kwa maana wewe Bwana,

hujawaacha kamwe wakutafutao.

11 Mwimbieni Bwana sifa, amefanywa mtawala Sayuni,

tangazeni miongoni mwa mataifa, yale aliyoyatenda.

12 Kwa maana yeye alipizaye kisasi cha damu hukumbuka,

hapuuzi kilio cha wanaoonewa.

13 Ee Bwana, tazama jinsi walivyo wengi adui zangu wanaonitesa!

Nihurumie, uniinue kutoka malango ya mauti,

14 ili niweze kutangaza sifa zako

katika malango ya Binti Sayuni

na huko niushangilie wokovu wako.

15 Mataifa wameanguka kwenye shimo walilolichimba,

miguu yao imenaswa kwenye wavu waliouficha.

16 Bwana anajulikana kwa haki yake,

waovu wamenaswa katika kazi za mikono yao.

17 Waovu wataishia kuzimu,

naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu.

18 Lakini mhitaji hatasahaulika siku zote,

wala matumaini ya walioonewa hayatapotea.

19 Ee Bwana, inuka, usimwache binadamu ashinde.

Mataifa na yahukumiwe mbele zako.

20 Ee Bwana, wapige kwa hofu,

mataifa na yajue kuwa wao ni watu tu.