Daudi Anakatazwa Kujenga Hekalu

1044 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Samweli 7

1 Baada ya mfalme kuingia rasmi katika jumba lake la kifalme, naye Bwana akiwa amemstarehesha pande zote mbali na adui zake, 2 akamwambia nabii Nathani, “Mimi hapa, ninaishi katika jumba la kifalme la mierezi, wakati Sanduku la Mungu limebaki katika hema.”

3 Nathani akamjibu mfalme, “Lolote ulilo nalo moyoni, endelea ukalifanye, kwa maana Bwana yu pamoja nawe.”

4 Usiku ule neno la Bwana likamjia Nathani, kusema:

5 “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Je, ewe ndiwe wa kunijengea mimi nyumba ili nikae ndani yake? 6 Sijakaa ndani ya nyumba tangu siku niliyowaleta Waisraeli kutoka Misri hadi leo. Nimekuwa nikitembea kutoka mahali pamoja hadi mahali pengine ndani ya hema kama makao yangu. 7 Popote nilipotembea pamoja na Waisraeli wote, je, nimewahi kumwambia kiongozi wao yeyote niliyemwamuru kuwachunga watu wangu Israeli, “Kwa nini hujanijengea nyumba ya mierezi?” ’

8 “Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: Nilikutoa wewe kutoka machungani na kutoka kuandama kundi la kondoo na mbuzi ili kuwaongoza watu wangu Israeli. 9 Nimekuwa pamoja nawe popote ulipokwenda, nami nimekuondolea mbali adui zako wote mbele yako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kuu kama majina ya watu walio wakuu sana duniani. 10 Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali niwapande humo ili kwamba wawe na nyumbani kwao wenyewe wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawaonea tena, kama walivyofanya mwanzoni, 11 na kama walivyofanya tangu mwanzo wakati nilipowaweka viongozi juu ya watu wangu Israeli. Pia nitawapa raha mbele ya adui zenu wote.

“ ‘Bwana akuambia kwamba Bwana mwenyewe atakujengea nyumba. 12 Siku zako zitakapokwisha nawe ulale pamoja na baba zako, nitainua mzao wako aingie mahali pako, ambaye atatoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake. 13 Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, nami nitaimarisha kiti cha enzi cha ufalme wake milele. 14 Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Atakapokosea nitamwadhibu kwa fimbo ya wanadamu, kwa adhabu ya kupigwa na wanadamu. 15 Lakini upendo wangu kamwe hautaondolewa kwake, kama nilivyouondoa kwa Sauli, niliyemwondoa atoke mbele yako. 16 Nyumba yako na ufalme wako utadumu milele mbele zangu, kiti chako cha enzi kitafanywa imara milele.’ ”

17 Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya.

18 Ndipo Mfalme Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za Bwana, akasema:

“Ee Bwana Mwenyezi, mimi ni nani, na jamaa yangu ni nini, hata umenileta mpaka hapa nilipo? 19 Naam, kana kwamba hili halitoshi machoni pako, Ee Bwana Mwenyezi, wewe umenena pia kuhusu siku zijazo za nyumba ya mtumishi wako. Je, hii ndiyo njia yako ya kawaida ya kushughulika na mwanadamu, Ee Bwana Mwenyezi?

20 “Je, Daudi aweza kukuambia nini zaidi? Kwa maana unamjua mtumishi wako, Ee Bwana Mwenyezi. 21 Kwa ajili ya neno lako na kwa mapenzi yako, umefanya jambo hili kubwa na kulifanya lijulikane na lifahamike kwa mtumishi wako.

22 “Tazama jinsi ulivyo mkuu, Ee Bwana Mwenyezi! Hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe, 23 Naye ni nani aliye kama watu wako Israeli, taifa pekee duniani ambalo Mungu alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe, na kujifanyia jina mwenyewe, kwa kufanya maajabu makubwa na ya kutisha kwa kuwafukuza mataifa na miungu yao mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri? 24 Umeimarisha watu wako Israeli hasa kama watu wako mwenyewe milele, nawe, Ee Bwana, umekuwa Mungu wao.

25 “Basi sasa, Bwana, ukaitimize ahadi uliyosema kuhusu mtumishi wako na nyumba yake milele. Fanya kama ulivyoahidi, 26 ili kwamba jina lako litukuke milele. Ndipo watu watasema, ‘Bwana Mwenye Nguvu Zote ni Mungu juu ya Israeli!’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itakuwa imara mbele zako.

27 “Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, umelifunua hili kwa mtumishi wako, ukisema, ‘Nitakujengea nyumba.’ Hivyo mtumishi wako amepata ujasiri kukuletea dua hii. 28 Ee Bwana Mwenyezi, wewe ndiwe Mungu! Maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidi mtumishi wako mambo haya mazuri. 29 Sasa naomba uwe radhi kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili idumu mbele zako milele, kwa maana wewe, Ee Bwana Mwenyezi, umesema, na kwa baraka zako nyumba ya mtumishi wako itaendelea kubarikiwa milele.”

1 Nyakati 17

1 Baada ya Daudi kuingia rasmi katika jumba lake la kifalme, akamwambia nabii Nathani, “Hebu tazama, mimi ninakaa kwenye nyumba nzuri iliyojengwa kwa mierezi, wakati Sanduku la Agano la Bwana liko ndani ya hema.”

2 Nathani akamjibu Daudi, “Lolote ulilo nalo moyoni mwako litende, kwa maana Mungu yu pamoja nawe.” 3 Usiku ule neno la Mungu likamjia Nathani, kusema:

4 “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Wewe hutanijengea mimi nyumba ili nikae humo. 5 Mimi sijakaa ndani ya nyumba tangu siku ile niliyowatoa Israeli kutoka Misri mpaka leo. Nimehama kutoka hema moja hadi jingine na kutoka mahali pamoja hadi pengine. 6 Je, popote nilipokwenda pamoja na Waisraeli wote, wakati wowote nilimwambia kiongozi yeyote niliyemwagiza kuwachunga watu wangu, kwa nini hujanijengea nyumba ya mierezi?’ 

7 “Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: Nilikuchukua machungani na kutoka kuandama kondoo ili uwatawale watu wangu Israeli. 8 Nimekuwa pamoja nawe popote ulipokwenda, nami nimekuondolea mbali adui zako wote mbele yako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kuu kama majina ya watu walio wakuu sana duniani. 9 Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali na nitawapa ili wawe na mahali pao wenyewe pa kuishi na wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawaonea tena, kama walivyofanya mwanzoni, 10 na ambavyo wamefanya siku zote tangu nilipowachagua viongozi kwa ajili ya watu wangu Israeli. Pia nitawatiisha adui zenu wote.

“ ‘Pamoja na hayo ninakuambia kwamba Bwana atakujengea nyumba: 11 Wakati wako utakapokuwa umekwisha, nawe ukawa umekwenda kukaa na baba zako, nitamwinua mzao wako aingie mahali pako kuwa mfalme, mmoja wa wana wako mwenyewe, nami nitaufanya imara ufalme wake. 12 Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili yangu, nami nitakifanya imara kiti cha ufalme wake milele. 13 Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Kamwe sitaondoa upendo wangu kwake, kama nilivyouondoa kwa yeye aliyekutangulia. 14 Nitamweka juu ya nyumba yangu na ufalme wangu milele; kiti chake cha enzi nitakifanya imara milele.’ ”

15 Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya.

16 Ndipo Mfalme Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za Bwana, akasema:

“Mimi ni nani, Ee Bwana Mungu, na jamaa yangu ni nini, hata umenileta mpaka hapa nilipo? 17 Kana kwamba hili halitoshi machoni pako, Ee Mungu, umenena pia kuhusu siku zijazo za nyumba ya mtumishi wako. Umeniangalia kama mtu aliyetukuka kuliko watu wote, Ee Bwana Mungu.

18 “Daudi aweza kukuambia nini zaidi kuhusu kumheshimu mtumishi wako? Kwa maana wewe unamjua mtumishi wako, 19 Ee Bwana Mungu. Kwa ajili ya mtumishi wako, tena sawasawa na mapenzi yako, umefanya jambo hili kubwa sana na kujulisha ahadi hizi zote zilizo kubwa sana.

20 “Hakuna aliye kama wewe, Ee Bwana Mungu, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe. 21 Naye ni nani aliye kama watu wako Israeli: taifa pekee duniani ambalo Mungu wake alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe na kujifanyia jina kwa ajili yake mwenyewe, kwa kufanya maajabu makubwa na ya kutisha kwa kuwafukuza mataifa mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri? 22 Uliwafanya watu wako Israeli kuwa watu wako wewe mwenyewe milele, nawe, Ee Bwana Mungu, umekuwa Mungu wao.

23 “Sasa basi, Bwana ahadi uliyoweka kuhusu mtumishi wako na nyumba yake na uithibitishe milele. Fanya kama ulivyoahidi, 24 ili ithibitike na jina lako litakuwa kuu milele. Kisha watu watasema, ‘Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu aliye juu ya Israeli, ndiye Mungu wa Israeli.’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itafanywa imara mbele zako.

25 “Wewe, Mungu wangu, umemfunulia mtumishi wako Daudi kwamba utamjengea yeye nyumba. Hivyo mtumishi wako amekuwa na ujasiri wa kukuomba maombi haya. 26 Ee Bwana, wewe ndiwe Mungu! Umemwahidi mtumishi wako mambo haya mazuri. 27 Basi imekupendeza kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili idumu milele machoni pako; kwa ajili yako, Ee Bwana, umeibariki, nayo itabarikiwa milele.”